Bunge hili aibu


editor's picture

Na editor - Imechapwa 25 July 2012

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

HISTORIA ya mabunge duniani inaliumbua bunge la Jamhuri. Ni kwa sababu, bunge hili limegeuza taasisi ya Bunge kuwa sehemu ya kuminya demokrasia. Limejisahau. Limejifunga mnyororo.

Ni tofauti na Bunge lililopita lililokuwa chini ya Spika Samwel Sitta.

Ni jambo la kusikitisha kuona ushahidi ukijionesha kiwango cha uwajibikaji serikalini kikishuka, Bunge likitumika kuiokoa.

Hakuna asiyejua kuwa serikali imeshindwa kuafikiana na madaktari. Bunge linagoma kujadili suala hilo. Kiongozi wa madaktari ametekwa, kujeruhiwa na sasa yuko kwenye matibabu nje ya nchi, bunge linafungwa mdomo kujadili.

Mauaji ya ovyo ya raia yanazidi kuonge; Bunge halijadili. Utawala bora unatukanwa, huku wawekezaji na matajiri wakitwaa ardhi ya wananchi, bunge linafungwa mdomo. Huu ni uzembe.

Ndiyo maana tunashuhudia utamaduni mpya ukiibuka bungeni; ili hoja ya mbunge ijadiliwe inategemea ni mbunge gani, na hasahasa, wa chama gani.

Kama ni asiyependeza kiti, hapewi nafasi. Kama alipewa kwa kutegwa kwa kuwa spika hakujua atakachokisema, akiibuka mbunge wa watawala na kumhoji, anaridhiwa. Yule anaambiwa “huna hoja.”

Waongoza bunge wametafuta lugha wanazoona nzuri kumbe wanakandamiza haki za wabunge kusema bungeni. Wanataka wabunge wakasemee wapi?

Kisingizio cha kuingilia mahakama hakina nguvu. Kutaja tukio ambalo limefika kwenye mahakama hakuna maana kuwa unaingilia uhuru wa bunge.

Tunasihi waongoza bunge warudi kwenye mstari. Wakiamini hawajakosea wala hawajaudhi au kuwaangusha Watanzania, basi hiyo ni hatari.

Tanzania ipo ndani ya mfumo wa vyama vingi ambao una utamaduni wake. Chini ya mfumo huu, bunge lazima kuwa wazi na huru.

Tungependa waongoza bunge watumie mamlaka waliyonayo kuiwajibisha serikali iliyoamua kukataa kuwajibika. Kama yenyewe haitaki, inalindwa vipi?

0
Your rating: None Average: 3.9 (13 votes)