Bunge likatae kubeba serikali


editor's picture

Na editor - Imechapwa 04 March 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KATIKA hali ya kawaida, haitegemewi serikali kutumia bunge kutekeleza mambo yake; wala haitarajiwi bunge kufanya kazi zake kwa kuitumia serikali.

Serikali inatawala. Bunge linatunga sheria, kusimamia na kushauri serikali na kuwakilisha wananchi.

Katika mgawano huu hatutarajii serikali kutegea bunge au kutaka kubebwa na bunge katika utekelezaji wa kazi zake.

Vivyo hivyo hatutarajii bunge kudandia au kuomba fadhila za serikali katika utendaji wake.

Sasa hapa kuna suala la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) la kutaka kununua mitambo ya kuzalisha mitambo ya umeme inayomilikiwa na kampuni ya Dowans.

Dowans walipewa mkataba na kampuni ya Richmond ambayo ilishindwa kutekeleza mradi wa kufua megawati 100 za umeme ilipopewa kazi hiyo kwa upendeleo katika mkataba uliogharimu Sh. 172 milioni.

Richmond iliishafutwa. Nayo Dowans haina mkataba na serikali hata kama hivi sasa haizalishi tena umeme. Mitambo imesimamishwa.

Lakini menejimenti ya TANESCO chini ya Mkurugenzi Mtendaji, Dk. Idris Rashid inataka serikali inunue mitambo ya Dowans. Imeleta visingizio vingi kuhusu hatari ya taifa kuingia gizani.

Naye Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja ambaye aliwahi kusema mitambo hiyo haiwezi kununuliwa, sasa amegeuka na kutetea ununuzi mithili ya dalali.

Kampeni imekuwa kubwa kiasi cha kutumika ujanja wa kuliingiza bunge kutafuta uhalali. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe anaonekana dhahiri kutumika katika hili.

Iwapo serikali inaamini kununua mitambo ya Dowans ni halali, si ifanye hivyo badala ya kutafuta ridhaa ya bunge, kitu ambacho haijawahi kukifanya hata siku moja?

Kwa ushawishi mkubwa, serikali na TANESCO wanataka kuonyesha wananchi kuwa wanahusisha bunge katika maamuzi wakati katika eneo hilo hakuna nafasi ya bunge.

Imefikia mahali Zitto akaingiza suala la “maslahi ya taifa” na kusema angetaka spika wa bunge aketishe kamati yake na Kamati ya Nishati na Madini ili kuona jinsi ya “kusaidia” Ngeleja na Dk. Rashid.

Huku ni kwenda mbali sana. Ni kuvuka mipaka, kwa mtu binafsi na kwa Kamati ya bunge kama wajumbe wake watakuwa wanakubaliana na Zitto.

Kuna dalili za Ngeleja na Dk. Rashid, na labda siyo serikali nzima wala TANESCO yote, kutaka kutumia Kamati ya bunge kuhalalisha ununuzi wa mitambo kinyume cha sheria na kanuni; na huenda kwa bei kubwa zaidi kuliko ile ya mitambo mipya.

Tusingependa kuona mtu yeyote au hata serikali, ikitumia bunge kuhalalisha mambo ya ovyo. Katika hili, bunge lisihusishwe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: