Bunge likinyamaza, wananchi wanasema


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 15 July 2008

Printer-friendly version

WABUNGE wameamriwa, kwa mujibu wa kanuni zao, kutoendelea kujadili suala la 'ushirikina bungeni' ambalo linahusisha kupatikana kwa unga katika ukumbi wa bunge.

Naibu Spika Anne Makinda amesema mjadala juu ya kilichoitwa ushirikina ndani ya bunge, sasa umefungwa na kwamba suala lenyewe lilikuzwa na vyombo vya habari. Sawa. Mjadala umefungwa bungeni; nje ya bunge bado unaendelea.

Kwanza, uchawi upo. Kutoa kauli za kukana uchawi hakuondoi uchawi unaotajwa katika vitabu-kiongozi vya madhehebu makuu ya dini duniani na katika fasihi nzima ya binadamu na mahusiano yake.

Pili, uchawi umepewa maana kadha wa kadhaa. Kwa mfano kutomtakia jema mwenzako au yeyote yule (huitwa roho mbaya), wivu mbaya wa kijicho (babinkiza), hasira ya kupindukia ielekezayo katika visasi na tendo lolote linalolenga kudhuru maisha.

Orodha ni ndefu. Lakini katika mazingira ya sasa, utoaji sumu (usumuishaji) kwa mtu ili afe au adhirike, unawekwa pia katika mazingira ya ulozi ambao ni sehemu ya ushirikina.

Hapa basi, tendo la ushirikina linatoka katika imani au itikadi ya kidhana na kuwa na maana pana zaidi inayohusisha matendo halisi; yenye lengo la kudhuru, lakini yanayokinzana na matakwa na matarajio ya jamii kwa ujumla. Hii ndiyo maana mjadala hauwezi kuisha haraka.

Huku nje ya bunge bado tunauliza: Nani alianza kuona unga uliomwagwa bungeni? Alikuwa peke yake au na wengine? Unga ulipoonekana, nani alibaki pale kuhakikisha unga huo hauondolewi hadi hatua muwafaka zichukuliwe?

Unga uliokutwa bungeni ulichotwa na nani? Katika chombo kipi? Aliyeuchota aliupeleka wapi? Katika chombo gani? Unga ulihifadhiwa wapi? Chini ya ulinzi wa nani?

Ni muhimu kujua kama yule aliyeona unga, akashuhudia unachotwa na kupelekwa polisi au kwingineko, anaendelea kuwepo kama mlinzi wa nyongeza katika maeneo yote ambako unga unapelekwa au unahifadhiwa kwa hatua ya baadaye.

Hata kama alikuwepo wa kufuatilia namna hiyo, alikuwa amekula kiapo cha kutunza unga? Ni kiapo cha nani hicho – bunge? Ni kweli kuwa viapo hukiukwa lakini ni muhimu kiwepo.

Sasa turudi katika kujihoji. Unga uko mikononi mwa Mkemia Mkuu wa Serikali – mtaalam wa vipimo anayepaswa kuthibitisha aina ya unga na madhara yake kwa binadamu, kama yapo.

Nani anajua fika kwamba unga uliochotwa bungeni ndio uleule uliohifadhiwa (na muhifadhi yeyote yule)? Nani anajua kama 'unga wa bungeni' ndio ulifikishwa kwa mkemia mkuu wa serikali na kwamba mkemia alishughulikia 'unga asilia?'

Hadi hapa, ni vema kwamba hakukuwa na kesi. Kama kesi ingekuwepo, bila shaka maswali yote haya, na huenda mengine mengi yangejitokeza au yangeibuliwa.

Sasa mkemia anasema unga aliopelekewa na ambao amepima, hauna madhara kwa binadamu. Ni unga aliopelekewa ambao si lazima uwe unga asilia wa bungeni. Ukizingatia maswali ya awali, utaona uwezekano wa unga kubadilishwa.

Tatizo litakuwa kubadilisha unga kwa manufaa ya nani. Walioandaa kasheshe hii wasingependa kupeleka unga usio na chochote ndani cha kuwaunga mkono ili wakamilishe lengo lao.

Imenikumbusha 'uchawi' katika magazeti ya Uhuru na Mzalendo. Tulikuwa pamoja na akina Josiah Mufungo (mhariri wa sasa wa Uhuru na Mzalendo), Mazeyinzile Nkurlu, Ndimara Tegambwage na wengine). Wakati fulani waandishi walimchukia sana mhariri wa habari ambaye alikuwa amegeuka 'bwana haambiliki.' Hayupo sasa.

Waandishi walijua kuwa mhariri huyo ana imani kubwa na kali katika ushirikina. Chumba cha habari cha gazeti hakikuwa na dari, kwa hiyo njiwa walionekana wakiruka huku na kule ambako papi ziliunganishiwa.

Waandishi wawili wa habari, watundu, walimuua njiwa mmoja na kumweka ndani ya mtoto wa meza wa meza ya mhariri wa habari! Mhariri wa habari aliingia ofisini. Kufungua mtoto wa meza, akakuta njiwa aliyekufa. Aliruka, akapiga kelele huku akisema kwa sauti ya juu, 'Najua! Najua, kuna wanaotaka kunimaliza.' Alihakikisha meza hiyo inaondolewa ndipo arejee kwenye nafasi yake.

Wakati waandishi waliofanya mzaha maalum kwa ajili ya kumtisha mhariri waliyejua ni 'muumini' wa ushirikina wakicheka na kupasuka mbavu mhariri alipunguza ubabe wake.

Katika sakata lote la bungeni hakuna aliyetajwa kuwa wa kwanza kuona unga bungeni. Watuhumiwa wa kimazingira, Andrew Chenge (Mb – CCM) na mfanyakazi wa Ofisi ya Katibu wa Bunge, Japhet Sagasii, hawajasema kama waliona unga ndani ya bunge.

Haijaelezwa pia ilikuwa ni baada ya muda gani hao wawili wametoka bungeni ilipogundulika kuwepo unga, na nani aliona unga huo kwanza. Je, hakuna waliokuwa wameingia bungeni baada ya wao kutoka?

Chenge amewahi kutoa cheche, akilaani kuhusishwa na ushirikina bungeni. Naye Sagasii aliwahi kunukuliwa na gazeti hili akisema ni mtumishi wa siku nyingi wa bunge, asiyeamini katika ushirikina na asiye na sababu ya 'kufanya kitu kama hicho.'

Nani basi katika bunge anayejishuku kuandamwa kama alivyokuwa akiandamwa mhariri mwenye itikadi ya ushirikina? Nani ndani ya bunge ambaye hawezi kujirekebisha hadi awekewe unga kwenye kiti?

Sababu na ushahidi, hata wa kimazingira, wa kuhusisha Chenge na Sagasii katika tukio hilo, haujaweza kutolewa. Bali kuna taarifa zisizorasmi juu ya kile ambacho kinaweza kuwa sababu ya kuwaandama watu hawa wawili.

Hata hivyo kinahusu mtu mmoja; naye ni Japhet Sagasii. Sagasii amekuwa mfanyakazi wa Ofisi ya Katibu wa Bunge. Amekulia bungeni na kukomaa.

Baadhi ya wabunge humtania Sagasii kwa kumwita 'Katibu wa Bunge' kwa vile alivyoonyesha kujali na kuitika haraka. Wafanyakazi wenzake wanaheshimu hilo pia. Hata akichukua nafasi hiyo hakuna atakayenuna kwa kuwa anastahili – kwa misingi ya umri, utaalam, uzoefu na maadili. Hashindani na yeyote.

Ni kutokana na hali hiyo, kisingizio kwamba Sagasii ameshiriki ushirikina kinaweza kuwa kimepandikizwa kuziba nafasi yake au amekumbwa na mashaka ya wanaovutana kisiasa ambako anaweza kushukiwa kuwa upande tofauti.

Vyovyote itakavyokuwa, Spika Samwel Sitta hatarajiwi kushindwa kuona kinachoendelea na kuzima njama za kumchafua kibarua wa bunge kwa miaka mingi.

Hatua ya kumharibia Sagasii, ni ushirikina mtupu iwapo tutazingatia ainisho mwanzoni mwa makala hii, na iwapo tutakumbuka kuwa hakuna uchunguzi wowote wa maana uliofanyika kuhusu vyanzo vya kasheshe ya ushirikina bungeni.

0
No votes yet