Bunge limjadili Rais Kikwete


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 25 January 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli
Rais Jakaya Kikwete

ALHAMISI ya 20 Januari 2011, Rais Jakaya Kikwete alifanya kazi mbili nzito mchana na usiku; moja yenye maslahi kwa taifa na nyingine yenye tija kwa mafisadi.

Mchana aliongoza kikao cha Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kilitoka na maazimio ya kujifurahisha.

Rais Kikwete aliongoza Kamati Kuu iliyokubaliana eti meya wao wa Arusha ni halali. Halafu wakakomaa iwe isiwe, wananchi watake wasitake serikali lazima iilipe kampuni ya kufua umeme ya Dowans tuzo ya Sh. 94 bilioni kwa madai ilishinda kesi dhidi ya Tanesco.

Usiku Rais Kikwete akaandaa bakuli kubwa kwa ajili ya  harambee ya kuchangia uboreshaji wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Katika harambee hiyo ambayo ilihudhuriwa na mabalozi na watu wenye nazo fedha taslimu Sh. 64milioni zilikusanywa na ahadi Sh. 1.33 bilioni.

Hizo ndiyo kazi alizofanya Alhamisi. Akiwa mwenyekiti wa CCM mchana, Kikwete ‘alikomalia’ malipo ya fidia ya Sh. 94 bilioni kwa kampuni feki ya Dowans, lakini usiku kama mkuu wa nchi, anapitisha bakuli kuomba fedha kwa ajili ya maendeleo ya taasisi muhimu ya UDSM.  Watu wenye akili lazima watatucheka.

Kwamba mchana Kikwete anaona serikali ina fedha za kuchezea, lakini usiku anaomba watu waisaidie serikali kupata fedha za maendeleo ya elimu. Kuna nini hapa?

Rais Kikwete alipoteza uhalali wa kuwa mtetezi na mlinzi wa raslimali za taifa tangu alipojitoza kuwa kiungo cha kufanikisha Richmond/ Dowans kuingia mikataba kinyume cha taratibu za Bodi ya Zabuni.

Akiwa CCM anajiagiza; akiwa serikalini anatekeleza.

Mwaka 2006, akiwa ndani ya Kamati Kuu ya CCM aliagiza serikali itafute njia za kuondokana na giza. Akiwa rais, serikali ikafanya ujanja ujanja ‘ikaanzisha’ Richmond; kampuni iliyoshika mkia mara mbili katika mchakato wa kupewa zabani ya kufua umeme na mara ya tatu ikashika nafasi ya tatu.

Mwaka 2007 Kamati Teule ya Bunge iligundua kwamba Richmond ni feki na haiko kokote duniani isipokuwa mizizi yake iko Dar es Salaam. Ghafla ‘bin vuu’ serikali ya Kikwete ikatangaza kwamba kampuni mpya iitwayo Dowans imechukua mikoba ya Dowans.

Nyaraka za Mahakama ya Kimataifa ya Biashara (ICC) kikundi kidogo cha mawaziri, kwa kutumia kampuni moja ya uansheria, ndicho kilibuni Dowans ingawa haikujihusisha na udhaifu huo kisheria katika usuluhishi.

Kama Richmond iliyopatikana kupitia mchakato wa Bodi ya Zabuni ilionekana feki, basi kisheria ilitakiwa mrithi apitie taratibu hizohizo – Richmond haikuwa na haki kisheria kuteua mrithi.

Kitu cha kushangaza, na kwa vile huo ndio uhuni ambao umekuwa ukifanyika muda mrefu, ikulu ikatia mkono na sasa CCM inadai eti “sisi ndio tuliokosea kuvunja mkataba.”

Kama utaratibu huu usio wa kisheria ndio unatetewa na ikulu ni ushahidi kuwa Dowans imezaliwa ikulu. Kwa maneno mengine kati ya wamiliki wa Dowans, mkuu wa nchi ameshiriki kuileta, ndiyo maana ameshikilia bango lazima Dowans ilipwe.

Uhuni huu umefanikishwa hivi; kampuni ya uanasheria iliyotumika kuhalalisha mkataba huo, ndiyo baadaye ilitumika kushauri uvunjwe, ndiyo hiyo serikali ilishauri Tanesco iitumie kwenye utetezi wake katika kesi dhidi ya Dowans na ndiyo bado inaishauri serikali.

Yaani kampuni hiyo inacheza kama kipa wa adui, halafu mshambuliaji wa upande wa pili na kisha inatumika kama kiungo. Huu ni uhuni na kama serikali imefikia kufanya madudu kama haya itakuwa imekalia kuti kavu.

Hivi daktari anayetoa ushauri kwamba ili binti yako apone haraka ugonjwa wa malaria inabidi anywe kwa mpigo vidonge 12 vya malaraquin, akifa daktari huyo anafaa kufanyia post mortem maiti? Hiyo ndiyo ikulu.

Bunge

Kwa kuwa ushauri wa kwanza wa kuvunjwa mkataba huo, ulitolewa na Bunge, kufuatia kazi iliyofanywa na Kamati Teule ya Bunge, kama kuna matatizo kuhusu utekelezwaji wake, Bunge liombe taarifa za utekelezaji wa maazimio yake.

Suala hilo likirudishwa bungeni kama Umoja wa Vijana wa CCM ulivyotumiwa na mafisadi kushauri, hoja haiwezi kuwa serikali ilipe au isilipe. Bunge lijadili, kwa kuzingatia katiba, nafasi na uwezo wa rais kwa lengo la kumshtaki bungeni.

Suala la Dowans likirejeshwa bungeni ina maana rais hajakubaliana na maazimio ya Bunge lililopita, hivyo analipatia mtihani mwingine.

Lakini kwa vile hoja ya Richmond ilianzia bungeni na serikali inakataa kutekeleza, ni dhahiri imeamua kujitumbukiza katika kashfa nzito ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani.

Mwaka 2008 baada ya Kamati Teule ya Bunge kufanya uchunguzi wa kina iliwasilisha ripoti bungeni ikiwa na mapendekezo 14. Bunge liliongeza mengine likafunga mjadala kwa maazimio 23.

Baadhi ya maazimio hayo yalitaka aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa apime nafasi yake – alipima  akajiuzulu pamoja na waliokuwa mawaziri wa nishati na madini, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha.

Serikali ilipewa majukumu kadhaa na kuwachukuliwa hatua watu kadhaa akiwemo mkurugenzi wa Tasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hoseah, aliyekuwa mwanasheria mkuu, Johnson Mwanyika, aliyekuwa Katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi. Hayo yote yalikuwa majukumu ya rais.

Rais hakutaka kuelekezwa na Bunge, hakufanya kazi hiyo badala yake alisubiri Mwanyika na Mwakapugi wakastaafu na akampa Dk. Hoseah rungu kuwatwanga wabunge wote waliotafuna posho mbilimbili.

Dk. Hoseah akapewa kazi nyingine ya kumsafisha bila ushahidi Andrew Chenge kwamba kesi ya rushwa ya rada iliyokuwa inamkabili haipo kwa madai kesi kuu iliyokuwa Uingereza ilifutwa. Siku chache baadaye Dk. Hoseah akaaumbuka kesi ile ilimhusisha.

Serikali ya Kikwete ikafanya kazi ya kusafisha ‘ujasiri wa kifisadi’ uliofanywa na wasaidizi wake badala ya kuwapa adhabu kama alivyotakiwa. Na sasa Kikwete amepewa ushauri kuwatimua madarakani mawaziri walioibua ufisadi huu na kupinga malipo kwa Dowans.

Rais hatarini

Katika mazingira haya, hoja haiwezi kuwa kujadili tena Dowans, wabunge walishapita hatua hiyo; ushahidi wote uko wazi kwamba anayeng’ang’ania malipo haya si Dowans ila ni ikulu. CCM na ikulu zimekunjwa na ufisadi mithiri ya mbwa akiona chatu.

0
Your rating: None Average: 3.8 (5 votes)
Soma zaidi kuhusu: