Bunge lisiingiliwe


editor's picture

Na editor - Imechapwa 30 March 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

ILIBAINIKA wiki iliyopita kwamba Sheria ya Gharama za Uchaguzi iliyosainiwa na Rais Jakaya Kikwete tarehe 17 Machi mwaka huu, ilikuwa na vipengele ambavyo havikupitishwa na Bunge.

Hii ina maana kuna vipengele vilivyochomekwa baada ya bunge kupitisha muswada. Kitendo hiki hakikubaliki katika nchi iliyoamua kufuata misingi ya utawala bora.

Vipengele vilivyochomekwa viko katika kifungu cha 7(3), ambacho hakikuwepo kabisa kwenye muswada uliojadiliwa na kupitishwa bungeni.

Kwa mujibu wa muswada uliowasilishwa bungeni, haikusemwa nani anatakiwa kukagua timu za kampeni.

Lakini kwenye kipengele ambacho kimo kwenye sheria iliyosainiwa na rais kinaonyesha kwamba timu za kampeni za mgombea urais zinatakiwa kuhakikiwa na msajili wa vyama vya siasa.

Tunaamini kwamba kilichofanyika, hata kama itadaiwa kuwa ni kwa nia njema, siyo sahihi.

Kama kitendo hicho kitapita bila ya hatua kuchukuliwa, kitakuwa kimefungua mlango kwa vitendo vingine kama hivi kufanyika katika siku zijazo.

Kinachotuumiza wengi ni kufahamu kwamba wapo watumishi wa serikali ambao, kwa sababu mbalimbali, wanadiriki kupindisha sheria za nchi kwa utashi wao binafsi.

Sheria ya Gharama za Uchaguzi ni miongoni mwa mambo ambayo pengine Rais Kikwete alikuwa amepanga yawe kumbukumbu ya utawala wake miaka mingi baada ya yeye kuachia madaraka.

Na ndiyo maana, kwa kuzingatia hilo, alihakikisha tukio la utiaji saini muswada huo linakuwa kubwa na kushuhudiwa, si tu na wananchi pekee, bali pia wawakilishi wa nchi mbalimbali waliopo nchini pamoja na wadau wa maendeleo wa taifa letu.

Tunaamini kwamba hakuna sababu yoyote inayoweza kutolewa na wahusika wa tukio hili kuhalalisha walichokifanya.

Kama rais Kikwete anataka kujenga serikali ambayo haitaki kuvumilia dharau dhidi ya mamlaka ya rais, serikali na bunge, ni muhimu akawa makini na kuchukua hatua muafaka katika hili.

Vinginevyo, na hili ndiyo hofu yetu kuu, kuna siku tunaweza kuonyeshwa live kwenye luninga tukio la rais kusaini kitu fulani, tukaja kubaini baadaye kwamba kumbe ikulu, au pengine nchi yetu yote, ilikuwa ikiingia mkataba wa kuuzwa; mbele ya macho yetu.

Pengine hata mikataba katika sekta ya madini na ubinafsishaji ambayo imeiingiza nchi yetu katika matatizo makubwa kwa sababu ya kuchomeka yale ambayo hayakupitishwa katika vikao halali.

Hata yatolewe maelezo marefu kiasi gani na hata rais akikaa kimya katika hili; sisi tungependa bunge liheshimiwe na kazi yake, baada ya kukamilika, isiingiliwe na yeyote mwenye uma, kijiko au mwiko.

0
No votes yet