Bunge sasa laweza kumchunguza Rais Kikwete?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 31 August 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

UNAHITAJIKA ujasiri kusema kuwa Bunge sasa litachunguza Ofisi ya Rais. Lakini unahitajika ujasiri zaidi kwa bunge lenyewe kufanya hivyo. Je, sivyo ilivyo?

Spika wa bunge hatasema waziwazi kuwa anachunguza ofisi ya rais. Kwa mazingira ya sasa waziri mkuu hawezi kuthubutu kusema anachunguza ofisi ya rais.

Lakini kama bunge linaunda kamati ya kuchunguza hatua ya ikulu ya kuruhusu “mtuhumiwa kurejea kazini,” hakika ikulu inachunguzwa – waseme au wasiseme; wakubali au wasikubali.

Uchunguzi huu unatokana na yaliyomsibu David Katundu Jairo, katibu mkuu wa wizara ya nishati na madini. Ilidaiwa bungeni kuwa wizara yake, akiwa mtendaji mkuu, ilipeleka barua kuagiza taasisi zilizoko chini yake kuchanga fedha za “kusaidia bajeti ya wizara yake kupita kwa urahisi?”

Madai hayo yalizaa fukuto. Waziri Mkuu Mizengo Pinda akasema angekuwa na madaraka angemfukuza Jairo kazi; lakini akaongeza kuwa rais hayupo nchini; yuko safarini Afrika Kusini.

Kauli hiyo ilionekana ya kujikinga tu; kwani aliyekuwa Afrika Kusini alikuwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Kila rais anapoondoka nchini, huacha rais mwingine anayemwapisha mwenyewe na kumwachia majukumu yake. Pinda hajasema kama alimwambia rais huyo akakataa au alimwogopa au hamwamini.

Lakini hata baada ya Jakaya Kikwete kurejea nchini, hakusema lolote. Ni Katibu wake Mkuu, Philemon Luhanjo aliyetangaza kuwa amampa Jairo “likizo” ili katika kipindi hicho ufanyike uchunguzi wa madai dhidi yake.

Alimwagiza Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo. Hakuchi kunakucha, Luhanjo akaja na taarifa, tena siyo kwa bunge bali kwa waandishi wa habari, kuwa Jairo ni msafi na kwamba arejee kazini.

Kwa nafasi aliyonayo, Luhanjo ndiye mkuu wa makatibu wakuu wote wa wizara – ndiyo maana anaitwa Katibu Mkuu Kiongozi. Huyu ndiye aliagiza likizo ya lazima; akaagiza uchunguzi na ndiye anatoa taarifa kumsafisha Jairo.

Katibu Mkuu Kiongozi ndiye Katibu Mkuu Ikulu. Yuko karibu sana na rais na kwa usahihi kabisa, hawezi kutenda jambo kubwa bila kutoa taarifa kwa rais au hata kumwomba ushauri.

Kutoka alikotoka, Luhanjo akawaambia waandishi wa habari kuwa Jairo msafi na anarejea kazini. Sherehe ikafanyika wizara ya nishati na madini. Akarudi ofisini.

Huku bunge likaota fundo kooni: Haiwezekani! Fukuto likarejea kwa kasi. Likatoka pendekezo la kuunda kamati ya kuchunguza mwenendo au mazingira yaliyomrudisha Jairo kazini.

Wakati kamati imeundwa, Rais Kikwete anajitokeza. Anasoma alama ukutani. Anatafakari kauli za waziri wake mkuu. Anaamuru Jairo “arejee likizoni.”

Ni bahati mbaya kwa rais kwamba tayari kamati ya uchunguzi imeundwa. Kuchunguza “mazingira yaliyomwachia” Jairo ni kuchunguza katibu mkuu kiongozi na kuchunguza CAG.

Kuchunguza katibu mkuu kiongozi, ni kuchunguza ofisi ya rais. Kuchunguza ofisi ya rais ni kuchunguza rais. Kwa mazingira ya sasa, kuchunguza rais ni kumchunguza Jakaya Mrisho Kikwete.

Inawezekana kabisa bunge lisifikie hatua ya kusema hivyo, lakini hatua yake inaelekea huko. Kwamba sasa rais tayari ameingilia kati, tunaweza kushuhudia kamati ya bunge ikiyeyuka kwa madai kuwa kilichotarajiwa kufanywa na kamati “tayari kimewekwa sawa.”

Ni mazingira haya ambayo yanaendelea kushawishi wengi kuwa serikali ya Rais Kikwete siyo makini, inalegalega au ni kigeugeu.

Taarifa ya Idara ya Mawasiliano ya Rais, iliyotolewa 26 Agosti 2011; kufafanua kilichompeleka Jairo likizo ya malipo, kumrejesha kazini na kumrudisha tena likizo, nayo imeshindwa kumtetea rais.

Taarifa inasema rais alifanya “uamuzi mmoja tu baada ya kupokea taarifa kutoka kwa katibu mkuu kiongozi (Philemon Luhanjo)” na kwamba aliufanya kabla ya bunge kuchukua hatua.

Ikulu inasema pamoja na rais kutoa maelekezo kwa katibu mkuu kiongozi, alimfahamisha pia waziri mkuu (Mizengo Pinda) kuhusu “uamuzi wake huo asubuhi hiyo ya 25 Agosti 2011.”

Kauli hii haileti maana kwa rais wala waziri mkuu. Wote wawili, pamoja na bunge, wanajua taarifa ya ikulu inalenga kuweka tu ushahidi kwamba msemaji wa ikulu alifanya kazi ya kutetea rais na ikulu. Basi.

Kwani katibu mkuu kiongozi aliitisha mkutano wa waandishi wa habari siku ya Jumanne, 23 Agosti 2011 majira ya mchana kutangaza. Hapa alitangaza “ripoti ya kumsafisha” Jairo.

Siku Luhanjo anakutana na waandishi wa habari, bunge tayari lilikuwa limeahirishwa kutokana na kifo cha Mussa Khamis Silima, mbunge wa bunge la Muungano kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Mjadala wa Jairo uliibuka bungeni Jumatano tarehe 24 Agosti 2011. Ni siku hiyo ambayo Naibu Spika, Job Ndugai alikubaliana na hoja ya kuundwa kwa kamati teule kuchunguza suala la Jairo.

Kwa hiyo taarifa ya ikulu ina walakini. Katika kutaka kujenga hoja kwamba rais hajashinikizwa na bunge kumwondoa tena Jairo, inataja tarehe ya 25 Agosti 2011 kuwa ilikuja kabla ya 24 Agosti.

Taarifa ya ikulu inataka kusema kuwa Luhanjo alikaidi maelekezo ya rais wake. Labda achukuliwe hatua. Aidha, inataka kupendekeza kuwa Pinda hakufanya kazi yake ya kuiwakilisha serikali, kwani tayari alikuwa na kauli ya rais.

Kwa wanaomfahamu vizuri Pinda, asingekaidi agizo la bosi wake. Kwa hiyo, kwa utulivu, Pinda aliliambia bunge, Alhamisi asubuhi, 25 Agosti 2011, wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo, kwamba tayari Rais Kikwete amemrejesha likizo Jairo.

Hii ni baada ya bunge kupitisha uamuzi wa kuunda kamati. Pinda alikuwa akijibu swali la kiongozi wa upinzani bungeni, Freeman Mbowe, aliyehoji kwa nini serikali isimpeleke likizo Jairo wakati huu ambao Bunge “tayari limeridhia kuundwa kamati teule kumchunguza.”

Hapa linajitokeza jambo moja kubwa, kwamba huko ikulu hakuna mawasiliano mazuri.

Kungekuwa na mawasiliano, kusingekuwa na mgongano huu. Inaonekana Luhanjo, ama hakuwasiliana na rais au kama alifanya hivyo, hakumfafanulia vizuri kile alichokuwa akienda kufanya – kumwachia Jairo.

Kwa upande mwingine, kama rais angekuwa na taarifa angetoa maelekezo juu ya Jairo tarehe 22 au 23 Agosti au hata kabla ya hapo na siyo baadaye kama anayekurupushwa.

Kama kungekuwepo mawasiliano, Luhanjo angemwambia waziri mkuu juu ya uamuzi, ama wake binafsi au wa rais, kuhusu hatua zinazotakiwa kuchukuliwa kuhusu Jairo. Waziri mkuu hakuwa na taarifa.

Kama waziri mkuu angekuwa na taarifa, asingekaa kimya bungeni, huku wabunge waking’aka na hatimaye kupitisha, kwa kauli moja, uamuzi wa kuunda kamati ya uchunguzi.

Vilevile kungekuwa na mawasiliano ikulu, idara ya mawasiliano ya rais ingejua kuwa Luhanjo anakwenda kusema nini, siku mbili kabla rais hajatoa kauli yake ya kumrejesha Jairo likozoni.

Kungekuwa na mawasiliano, Luhanjo angejua au angekumbuka kuwa sakata la Jairo lilianzia bungeni ambako kuna mwendesha shughuli za serikali – waziri mkuu. Angewasiliana naye kabla ya kuongea na waandishi wa habari.

Kinachojadiliwa sasa, kuwa ni ukosefu wa mawasiliano, kisingekuwepo na rais asingeonekana kama anashinikizwa. Vivyo hivyo, idara ya mawasiliano ya rais isingejikuta pabaya na kuanza kuficha ukweli.

Sasa hatua ya Rais Kikwete kumrejesha likizo Jairo kinyume cha uamuzi uliofanywa awali na ofisi yake kupitia Luhanjo, inaongeza uzito wa hoja ya utovu wa mawasiliano na hata ugeugeu katika ofisi kuu ya nchi.

Hapa unajengeka upenyo wa kuuliza: Je, ni nani yuko sahihi; Luhanjo aliyeamuru Jairo kurejea kazini, au Rais Kikwete aliyeagiza katibu mkuu huyo kuendelea na “likizo?”

Ni mwenendo huu unaothibitisha madai ya baadhi ya wachunguzi wa serikali ya Rais Kikwete, kwamba “imekumbwa na ombwe la uongozi;” kwani hakuna maelezo yoyote yanayoweza kuhalalisha mnyukano usio wa lazima katika sakata hili.

Kwa vyovyote vile, Jairo anastahili kuchunguzwa kama anavyostahili kusikilizwa. Kwa upande wake, Pinda aliishasema bungeni, “...kama ningekuwa na mamlaka juu ya ndugu Jairo, nigekuja mbele yenu na kuwaambia tayari Jairo hana kazi tena.”

Alisisitiza, “...suala lililokuwa linalalamikiwa, lilikuwa limeghubikwa na utata mwingi kiasi kwamba inakuwa ni vigumu kulitetea.” Kauli hii ina maana Pinda alishagundua mazingira yale yalitosha kumpumzisha Jairo.

Kilichobakia sasa miongoni mwa wananchi, ni kujuliza, “Nani zaidi – Luhanjo, bunge au rais?” Hii ni hatari katika mawasiliano ya ofisi kuu.

Hata hivyo, hatua ya Rais Kikwete kupingana na hatua ya katibu mkuu wake imeongeza ugumu katika tuhuma dhidi ya Jairo.

Je, ni kweli anataka kujua fedha zinazodaiwa kuchanghishwa zilikuwa zinapelekwa wapi? Anataka kujua kama kila wizara inafanya hivyo? Hivi inawezekana akawa hajui?

Mambo mengi yataanza kujitokeza. Rudovick Uttoh, yule mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali, ni mtu anayeheshimika na anayependa kulinda hadhi ya kazi yake.

Hivi ripoti yake ikoje? Nani anayo? Kwa nini Luhanjo hakuitoa kwa waandishi wa habari? Kwa nini waandishi hawakuitaka au hawajaitaka?

Kwa upande mwingine, Jairo anatajwa kuwa rafiki wa karibu wa Rais Kikwete tangu walipofanya kazi pamoja wizara ya nishati na madini katika miaka ya 1980.

Kwa msingi huo, hatua ya Rais Kikwete ya kupingana na katibu mkuu wake, yaweza kuwa ya kumlinda Jairo kuliko kumwacha akaangamia katika tuhuma na piga nikupige iliyokwishaanza.

Kumwondoa Jairo pia kunaweza kupoza bunge na kufanya liache uchunguzi ulionuiwa – ambao hauwezi kuwa uchunguzi mpaka umhusishe Jairo, Luhanjo, Rais Kikwete na wengine.

Bali hadi hapa, tayari wananchi wamejenga mashaka kuliko matumaini katika kujulishwa nini hasa kinaendelea.

Bunge likifanya uchunguzi litajizolea hadhi na uhalali wa aina yake mbele ya wananchi; bila kujali matokeo ya uchunguzi huo yatamfurahisha nani. Likizimwa kijanja au kwa woga, nalo litajengewa mashaka.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: