Buriani Juma ‘Jenerali’ Mkambi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 24 November 2010

Printer-friendly version

KATIKATI ya miaka ya 1970 klabu ya soka ya Yanga ilikumbwa na mgogoro mkubwa na ikaondokewa na wachezaji wake nyota.

Hicho ndicho kipindi, Yanga ilikuwa imekaribisha uteja wa kudumu kutoka kwa watani wao wa jadi katika soka, Simba kuanzia mwaka 1977 ilipokung’utwa mabao 6-0.

Uteja huo ulitokana na wachezaji nyota kuondoka baada ya kuibuka mgogoro mkubwa. Walioondoka ndio baadaye walikuja kuunda Pan African.

Kuondoka kwa nyota hao kuliicha Yanga ikiwa taabani. Hata hivyo ilijikongoja, ikapandisha baadhi kutoka timu ya vijana na ikasajili wapya kutoka klabu nyingine.

Miongoni mwa waliosajiliwa mwaka 1978 alikuwa kijana mmoja wa kiungo kutoka Nyota Africa ya Mtwara, naye hakuwa mwingine isipokuwa Juma Mkambi.

Haraka alikonga nyoyo za mashabiki kwa uhodari wake wa kupokea mipira na kutoa pasi za uhakika na hata kufunga mabao. Alikuwa na uwezo wa kupanda juu kusaidia mashambulizi na kurudi nyuma haraka kuzuia.

Mafanikio

Haraka Mkambi alijiimarisha katika kikosi cha Yanga na haikushangaza umahiri wake ulipowavutia Kocha mkuu wa Taifa Stars, Paul West Gwivaha na msaidizi wake Joel Bendera pamoja na mshauri wa ufundi, Vladmir Wolk kutoka Poland wakamteua katika kikosi kilichoshiriki fainali za Kombe la Mataifa Nigeria.

Taifa Stars ilifuzu kucheza fainali hizo baada ya kuitoa Mauritius kwa jumla ya mabao 6-3 halafu Zambia kwa jumla ya mabao 2-1.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Dar es Salaam, Taifa Stars iliishinda Zambia kwa bao 1-0 na katika mechi ya marudiano nchini Zambia ililazimisha sare ya bao 1-1.

Baada ya kufuzu, nchini Nigeria, Stars ilipangwa kundi moja na wenyeji hao pamoja na timu zenye uzoefu za Ivory Coast na Misri Kundi A.

Katika mechi ya fungua dimba, hadi mapumziko wenyeji Nigeria walikuwa mbele kwa mabao 2-0, lakini kipindi cha pili, Mkambi aliwanyanyua mashabiki wachache wa soka wa Tanzania waliofika kushuhudia fainali hizo alipofunga bao la kufutia machozi katika dakika ya 54 katika mechi iliyomalizika kwa kipigo cha mabao 3-1.

Mechi ya pili dhidi ya Misri, Stars ilifungwa mabao 2-1 huku Waziri akifunga bao la kufutia machozi na ni Waziri aliyefunga tena bao dhidi ya Ivory Coast mchezo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Kwa matokeo hayo, safari ya Stars iliishia hapo na wachezaji walirejea kwenye klabu zao kutoa mchango katika Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu ya Bara).

Magazeti yaliyochambua mechi mbalimbali zikiwemo za Stars yalisema katika safu zao “…generally Mkambi played very well…” yaani kwa ujumla Mkambi alicheza vizuri sana. Lakini waswahili walitafsiri neno generally kuwa jenerali na hiyo ndiyo siri ya kupachikwa jina la Jenerali.

Klabuni

Mkambi aliendelea kuwa mchezaji tegemeo katika timu ya taifa, lakini mchango wa kihistoria alitoa katika klabu yake ya Yanga.

Ni Jenerali Mkambi aliyehitimisha uteja wa Yanga kwa Simba baada ya kupachika bao lililoiwezesha klabu hiyo ya Jangwani kuchinja mnyama kwa bao 1-0 mwaka 1981 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo iko kwenye rekodi ya klabu mbili hizo kwamba Mkambi alifunga bao kwa mkwaju aliotandika kutoka umbali wa mita 40 hivi na mpira ukajaa wavuni.

Ushindi huo ulirejesha amani, shangwe, faraja na hali ya kujiamini kwa mashabiki wa Jangwani na kustawisha jina la Jenerali. Hakika, kwa mafanikio hayo alikuwa mmoja wa wachezaji walioheshimika sana.

Watu waliocheza naye katika miaka ya 1980 kama vile Charles Boniface Mkwasa wanasema Mkambi alikuwa na hulka ya kiuongozi na alitoa ushauri kwa wachezaji wenzake.

“Alikuwa na uwezo mkubwa wa kukaba, kugawa mpira na kudhibiti,” anasema Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Leodegar Tenga, ambaye alikuwa nahodha wa Taifa Stars iliyofuzu kucheza fainali Nigeria.

Mwanamichezo-mwanasiasa Idd Azzan anasema, “Mkambi alitofautiana na wachezaji wengine waliopitia Yanga. Huyu alikuwa na mapenzi na Yanga kwani tangu ajiunge hakuondoka hadi alipostaafu.”

Jenerali Mkambi ameichezea Yanga kwa miaka 10 tangu mwaka 1978 na hadi anastaafu hakujiunga na klabu nyingine.

Wasifu

Jenerali Mkambi alikuwa mchezaji wa miraba minne lakini tofauti na watu wengine wenye miili mikubwa, mkongwe huyo, alikuwa mstaarabu.

Hii imebaki historia, Mkambi hayupo tena amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kuugua kwa muda mfupi. Amezikwa katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam juzi.

Alifikishwa katika hospitali hiyo akisumbuliwa na malaria. Amewahi kulazwa katika hospitali ya Regency ambako alifanyiwa uchunguzi.

Mkambi aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 55 ameacha mjane na watoto watatu; wawili wa kiume na mmoja wa kike.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: