Buriani Mazee Rajab Mazee


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 16 February 2011

Printer-friendly version
Tanzia
Mazee Rajab Mazee

ASUBUHI ya Jumapili iliyopita ilikuwa mbaya kwangu. Majira ya saa 1: 14, nilipokea ujumbe mfupi wa maneno kwa njia ya simu kutoka kwa Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro.

“Mazee Rajab Mazee, kiongozi wa CUF, amefariki dunia,” ulisomeka ujumbe huo mfupi wa maneno. Ndiyo kwanza nilikuwa nimeamka na ujumbe huo ulinisikitisha.

Nikakumbuka mara yangu ya mwisho kukutana na Mazee akiwa hai. Ilikuwa mwishoni mwa Desemba mwaka jana mara baada ya kufanya mabadiliko ya uongozi ndani ya CUF yaliyomng’oa katika wadhifa wake wa Naibu Mkurugenzi wa Vijana na Blue Guards wa chama hicho.

Katika mazungumzo naye kwa vile nilimfahamu kwa kipindi kirefu kidogo, nilitaka kujua msimamo wake iwapo ataendelea kubaki ndani ya CUF au atahama kama walivyofanya akina Shaibu Akwilombe na Wilfred Lwakatare katika siku za nyuma.

“Ezekiel,” alinishtua kwa kuniita jina halafu akaendelea. “Suala la mimi kuhama CUF halipo. Mimi nitahama vipi CUF? Niende wapi? Bila ya CUF mimi ningekuwa wapi? Haya madaraka ambayo sasa nimevuliwa alikuwa nayo mtu mwingine kabla yangu na mimi pia nimempisha mtu kama nilivyopishwa mimi”.

“Kwa upande wangu, mimi naona chama sasa kimenipa nafasi ya kuanza kukijenga katika jimbo langu la Tunduru. Kuanzia sasa nitaanza kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi wowote utakaojitokeza lakini zaidi ule wa mwaka 2015,” aliniambia Mazee.

Hakujua kwamba Mungu alikuwa amempangia umri mfupi wa miaka 40 tu katika maisha ya dunia hii. Hakujua kwamba Mungu hakupanga yeye agombee tena ubunge!

Mazee Rajab Mazee alikuwa miongoni mwa wanasiasa vijana niliowapenda sana, siyo kwa sababu alikuwa rafiki zangu bali aina ya siasa aliyokuwa akifanya; ni aina ile ya siasa ambayo vijana wengi wanaielewa.

Utampenda Mazee akipanda jukwaani na kuzungumza kwa lugha ya kimjini ambayo vijana wanaielewa zaidi. Katika kipindi cha kati ya mwaka 2000 hadi 2007 ambapo CUF kilikuwa chama kikuu cha upinzani nchini, huyu alikuwa kati ya viongozi wa vijana wa chama hicho waliokifanya kitikise.

Mazee alikuwa na heshima kwa viongozi wa juu wa CUF. Katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, Mazee alikuwa burudani tosha kila alipopewa fursa ya kumtambulisha jukwaani Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba.

“Naomba sasa niwatambulishe kwenu, Mwenyekiti wa CUF- Chama cha Wananchi, mgombea urais, mchumi aliyebobea, full bright professor, Ibrahim Haruna Lipumba, aje hapa awachambulie uchumi wa nchi yetu kinagaubaga,” alikuwa akisema na mara nyingi akiwasisimua wana CUF.

Mazee ni kati ya wanasiasa waliofanya nishindwe kwenda kazini siku ambayo matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 yalianza kutangazwa. Niliposikia kuwa aliyekuwa mgombea wa CCM, Juma Jamaldin Akukweti (Mola Amlaze Pema) alimshinda Mazee katika jimbo la Tunduru, roho iliniuma sana.

Nililia kwa sababu Mazee alifanya kazi kubwa sana ya kisiasa wakati huo. Nilikwenda Tunduru wakati huo na idadi ya watu na hamasa iliyokuwapo kwenye mikutano yake ya hadhara ilikuwa kubwa mno.

Alibubujikwa machozi tulipokutana tena Dar es Salaam mara baada ya uchaguzi huo. Alilia si kwa sababu alikuwa na uchu wa madaraka, la hasha, isipokuwa ukweli kwamba mfumo wa siasa nchini ulimnyima nafasi yeye lakini ukampa mtu ambaye ilionekana hakuwa chaguo la wananchi.

Mazee alikuwa mcheshi sana. Nilipokuwa naye tulikuwa tukizungumza naye mambo mengi ya kisiasa na yale ya vijana. Na niseme wazi kuwa wakati nilipokuwa Tunduru, alihakikisha naishi vizuri bila ya matatizo. Kwa lugha ya vijana inayotumika sasa hivi; Mazee angesema “alinipa bata.”

Ningefurahi kama siku moja Watanzania wangepata bahati ya kumwona bungeni Mazee. Alikuwa na uwezo mkubwa wa kujieleza na hakuwa mwoga. Angeweza kuzungumza chochote kile katika jumba lile bila ya kumwogopa yeyote.

Ujasiri wa Mazee ulikuwa  wa kipekee. Kwenye maandamano au shughuli yoyote iliyokuwa ikifanywa na CUF, yeye alikuwa miongoni mwa viongozi waliokaa mstari wa mbele. Na alikuwa mtetezi wa kweli wa wanyonge.

Mazee alifariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita kutokana na ugonjwa wa malaria kali. Alizikwa juzi katika makaburi ya familia yake yaliyoko Tunduru Mjini.

Akizungumza katika mazishi yake hayo, Prof. Lipumba aliwataka vijana nchini kufuata nyayo za Mazee katika utetezi wa haki za wanyonge na kutaka Tanzania yenye mabadiliko na maendeleo kwa wote.

Mazee ambaye aliwahi kuwania ubunge wa Tunduru mara tatu katika kipindi cha miaka sita iliyopita, alizikwa na umati mkubwa wa watu; jambo lililoonyesha namna alivyoishi vizuri na watu.

Ombi langu kwa CUF ni moja tu; Mazee ameacha wajane wawili na watoto – chama kinatakiwa kuona kuwa familia yake haiadhiriki kwa kumkosa kada huyu. Ni lazima kitafute namna ya kumuenzi kada wake huyu.

Duniani sote tunapita. Siku moja tutaonana tena mbele ya haki. Mola amlaze pema Mazee Rajab Mazee.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: