Burundi na miaka 16 ya kuuawa Ndadaye


William Kapawaga's picture

Na William Kapawaga - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly version

MIAKA 16 imepita tangu Burundi itikisike kutokana na kuuawa kwa aliyekuwa rais wa kwanza wa kuchaguliwa kidemokrasia, Melchior Ndadaye. Tukio hilo lilitokea mwaka 1993.

Chimbuko lake ni Jeshi la Burundi kuasi na kusababisha mauaji ya kinyama kwa wananchi wasio na hatia yoyote.

Hali ya mambo bado haijatengemaa sawasawa katika nchi hii, pamoja na kuwepo na utawala wa kiraia ulio chini ya Rais Pierre Nkurunzinza. Kuna mauaji ya chini kwa chini na hali ya kutokuaminiana miongoni mwa wanasiasa.

Ndadaye aliyezaliwa 28 Machi, 1953 katika Mkoa wa Muramvya, ni msomi aliyepata elimu ya msingi kwenye mji wa Mbogora, mkoani Gitega mwaka 1960 hadi 1966.

Aliendelea na masomo ya juu na baadaye kuwa mwalimu na mtumishi wa benki.

Baada ya kushamiri kwa vita vya kikabila huku raia wengi wa kabila lake la Wahutu na Watutsi wachache, wakiuliwa kinyama na serikali ya kijeshi ya Burundi, kupitia kwa marais tofauti, Michael Micombero, Jean Babtist Bagaza na Pierre Buyoya, Ndadaye aliamua kuanzisha kundi la msituni ili kuleta mapinduzi, akilenga kusaidia kulinda haki za Wahutu.

Kuongezeka kwa makundi ya waasi wa Kihutu porini, yaliyokuwa yakipambana na serikali ya Buyoya, kulichagiza pande zinazohusika kukaa pamoja ili kutafuta muafaka na shinikizo la jumuiya ya kimataifa na nchi za Maziwa Makuu.

Shinikizo hizo zilifanikisha pande hizo hasimu kukaa pamoja kwa mazungumzo yaliyofanyika Arusha na Dar es Salaam, chini ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na hatimaye mwaka 1992 katiba mpya iliundwa ili kuandaliwa uchaguzi wa kidemokrasia mwaka uliofuata.

Uchaguzi huo wa 1993 ndio uliomwingiza madarakani Ndandaye baada ya kumbwaga Buyoya aliyekuwa ofisa mkubwa wa jeshi la Burundi.

Siku chache baada ya ushindi wa Ndadaye, kupitia chama chake cha FRODEBU, hatimaye 10 Julai, 1993, aliapishwa na kuwa rais wa kwanza wa kuchaguliwa huku akimteua Alphonce Kadege kutoka chama cha upinzani cha UPRONA, kuwa makamu wake wa rais.

Kuwashirikisha wapinzani katika serikali kulileta matumaini makubwa kwa wananchi wa Burundi, huku kwa muda wa miezi mitatu mabadiliko makubwa ya miundombinu na huduma za kijamii yakianza kuonekana kutokana na kufuta sera za kikabila.

Lakini kama ilivyo kwa msemo wa Waswahili kuwa “kizuri hakidumu,” ghafla ndoto ya Warundi ya kuingia katika utawala bora, ilizimika.

Ulikuwa ni usiku wa mshtuko kwao, kwa Afrika na dunia nzima pale redio ya taifa ilipotangaza asubuhi kuwa rais Ndadaye ameuawa na askari wa Kitutsi walioamua kuasi katika makazi yake jijini Bujumbura.

Mauaji yake yaliibua wimbi la mauaji ya kinyama dhidi ya Wahutu na wanajeshi wa serikali kutajwa kuhusika hadi kuthubutu kuipindua serikali ya kiraia katika mapinduzi yaliyofanikishwa na Meja Buyoya kwa mara nyingine.

Inakadiriwa raia 300,000 wengi wao wakiwa wa kabila la Wahutu, waliuawa huku maelfu ya wengine wakigeuka wakimbizi na kukimbilia nchi za jirani.

Takwimu za mwaka 2005 zinaonyesha kuwa nchi hiyo ina wananchi wapatao milioni saba.

Makabila makubwa yanayojulikana nchini Burundi ni Wahutu wanaochukua asilimia 90 ya wananchi wote, wakati asilimia 9 ni Watutsi na waliobaki ni kabila dogo la Watwa.

Kiasili, Warundi ni wakulima wa kahawa aina ya Arabika na Robusta, wakati kipato cha mwanachi ni chini ya dola moja.

Ndadaye aliuawa usiku wa manane nyumbani kwake, miezi mitatu tangu kuchaguliwa kwake, baada ya chama cha FRODEBU, kujipatia ushindi mkubwa kilipokibwaga chama cha Watutsi, UPRONA, kilichokuwa madarakani chini ya uongozi wa Charles Mukasi.

Burundi imejiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki miaka miwili iliyopita. Misukosuko ya mauaji makubwa ya kikabila ilianza mwaka 1972 pale Wahutu waliokuwa wengi jeshini, walipopindua serikali ya Watutsi waliokuwa wameshika hatamu ya uongozi chini ya rais Michael Michombero ambaye ni Mtutsi.

Kwa sasa mapigano ya kikabila yamepungua lakini zipo taarifa za chinichini kuwa hali ya mambo si shwari na tayari imezusha hofu kwa wananchi waliokuwa wamesahau machafuko.

Burundi inatawaliwa kwa kutumia katiba ya mwaka 2005 inayoelekeza kuwa kutakuwa na uchaguzi wa rais kila baada ya miaka mitano.

Bunge la Burundi lenye viti 100, lina asilimia 60 ya wawakilishi Wahutu na asilimia 40 ni Watutsi. Asilimia 30 ya wawakilishi bungeni ni wanawake.

Watutsi ndio waliokuwa wakazi asilia wa Burundi, lakini idadi yao ilizidiwa na Wahutu. Katika karne ya 15, Watusi waliingia eneo hilo na kuwazidi nguvu ya kiutawala Wahutu.

Wakati wa vita vikuu vya kwanza vya dunia, majeshi ya Ubelgiji yaliitwaa Burundi mwaka 1916 na mwaka 1919 nchi hiyo ikawa sehemu ya himaya ya Ubelgiji.

Julai mosi, 1962, Burundi ilipata uhuru. Lakini katika miaka hiyo ya 1960, ilitawaliwa na mapigano yaliyohusisha Wahutu na Watutsi.

Mwaka 1965 kulitokea jaribio la mapinduzi lililofanywa na Wahutu na kusababisha Watutsi walipe kisasi kwa kuwaua Wahutu wengi. Julai 1966, Mwambutsa wa IV alipinduliwa na mwanawe aliyefanywa kuwa Ntare wa V. Naye alipinduliwa katika mapinduzi ya kijeshi ya Novemba 1966.

Michel Micombero, ambaye alikuwa amechaguliwa waziri mkuu mwaka 1966, akawa rais, na katiba mpya ikaanzishwa mwaka 1970.

Micombero naye alipinduliwa na Kanali Jean-Baptiste Bagaza, pia Mtutsi, ambaye aliimarisha utawala wa Kitutsi madarakani.

0
No votes yet