Busanda: Ishara kutoka Magharibi


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 19 May 2009

Printer-friendly version
Uchambuzi

JUMAPILI hii, wapiga kura wa Busanda wilayani Geita, wanatarajiwa kukataa kuchagua mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hii si kwa sababu wanamchukia yeye binafsi, bali wanakataa chama chake.

Wananchi hao ninaamini watatuma ujumbe kwa watawala kuwa Watanzania hawawezi kamwe kuendelea kuchukuliwa kwa urahisi tu kwa sababu tu mtu fulani anaweza.

Katika uchaguzi mdogo unaokuja huko Busanda kuna watu ndani ya CCM, wakiongozwa na Katibu Mkuu wake Yusuph Makamba, wanaoamini kwa makosa kuwa chama hicho kina hati miliki ya jimbo la Busanda na hivyo ni lazima wachaguliwe kwani jimbo hilo lilikuwa “lao.”

Dalili za mwelekeo wa uchaguzi huo mdogo zinaonesha kuwa CCM itaadhibiwa kwa kutotimiza ahadi zake, kulea mazingira ya ufisadi na mafisadi nchini na zaidi sana kuwasahau watu wa Magharibi kwa miongo mingi tangu uhuru. Hii itakuwa ishara kutoka Magharibi.

CCM haina hati miliki ya jimbo la Busanda lakini pia haina jipya. Inayoahidi leo ingekuwa imeyatekeleza katika miaka 40 iliyopita. Iweje leo ndiyo watoe ahadi za umeme, na “kuleta maendeleo” kana kwamba Busanda ilikuwa ni kisiwa kilichosahauliwa katika nchi ya kufikirika?

Ishara hii kutoka Magharibi itaonekana kwa sababu wananchi wa Busanda ambao wamezukwa na utajiri wa kila aina bado wanaishi na kutegemea “maendeleo” kutoka serikali kuu.

Leo hii wanatambua kuwa chanzo cha matatizo yao siyo laana ya Mungu, wachawi, au mizimu bali ni uongozi mbovu na sera mbovu ambazo zimewarudisha nyuma. Wanatambua kuwa kuichagua CCM tena ni kuizawadia kwa kitu ambacho haistahili.

Wakati wananchi na watumishi wengi wanahangaika na hali za maisha kuna kundi kubwa la watu ambao wamechota utajiri mkubwa wa nchi yetu na kuufanya kuwa wa kwao na uzao wao. Na tukiwauliza basi wanakasirika na kufura. Miongoni mwa vitu vilivyochotwa ni madini ya Busanda.

Wananchi wanataka mabadiliko. Mabadiliko ya kwanza kabisa ni mabadiliko ya kifikra. Wanatambua kuwa Baba wa Taifa aliposema kuwa CCM siyo mama wala baba na kama ingeacha misingi yake angeweza kuiacha, wananchi wanajua alikuwa anamaanisha nini.

Leo hii viongozi wa CCM wanasimama na kutoa ahadi ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Busanda. Ahadi ambazo pia zimekuwa zikirudiwa katika chaguzi nyingine ndogondogo. Hata hivyo kitu kimoja hawawaambii wananchi juu ya rekodi ya serikali ya CCM katika suala la kueneza upatikanaji wa umeme nchini.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma iliyotolewa siku ileile milipuko mikubwa ya mabomu kule Mbagala (na hivyo kukoswa kusoma na watu wengi), inasemwa hivi kuhusu hali ya umeme nchini:

“Upatikanaji wa umeme hapa nchini (electricity coverage) kwa kaya ni asilimia 12 tu na kwa maeneo ya vijijini upatikanaji ni asilimia 2 tu. ”

Kwa jiji la Dar es Salaam, nusu tu ya nyumba zilizopo zimeunganishwa umeme. Wilaya tatu nchini zenye upatikanaji mkubwa wa umeme ni Ilala asilimia 46.3, Kinondoni asilimia 45.5 na Iringa asilimia 43.7 na wilaya tatu zenye upatikanaji mdogo kabisa wa Umeme ni Mtwara ambapo upatikanaji ni asilimia 0.1, Sumbawanga asilimia 0.1 na Biharamulo, asilimia 0.2.

TANESCO wanaendesha programu ya kufungia umeme wateja 100,000 kwa mwaka na kuweka utaratibu wa gharama za kuunganisha umeme kulipwa kwa kipindi kirefu ili kupunguza gharama za uunganishaji.

Kwa maneno mengine, ahadi ya kuweza kuwaletea Busanda umeme wa kutosha wakati Biharamulo tu ni asilimia 0.2 ni ahadi ya njozi.

Kama jiji la Dar kwenyewe wameshindwa hata kuwapatia umeme kwa asilimia 90 itakuwa ni ndoto ya alinacha kuamini kuwa serikali hiyo ya CCM itaweza kuwaletea umeme wa kutosha mwaka huu au miaka mitano ijayo wananchi wa Busanda.

Kwamba, mara zote nchi iko juu ya chama na iko juu ya mtu yeyote. Nchi ni ya kwanza kwani ndipo mahali pekee ambapo wana wan chi wanaweza kukimbilia ili wapate ulinzi wa utajiri wake na hifadhi ya maisha yao.

Jimbo la Busanda haliko juu ya nchi nzima; na hivyo wapiga kura wa Busanda kama wale wa Biharamulo wiki chache zijazo, hawana budi kutambu kuwa wanawakilisha kipima joto cha taifa. Wanapiga kura kutoa sauti ya taifa zima (kwani majimbo mengine hayana nafasi hiyo sasa hadi mwakani).

Hivyo, Busanda leo hii kama ilivyokuwa kwa Tarime imetambua kuwa mabadiliko ni lazima. Ni mabadiliko ya kuleta fikra mpya za kiuongozi, fikra mpya za mwelekeo mpya.

Hivyo, kwa CCM kumsimamisha mtu ambaye hakubaliki kunawafanya wana-CCM wampigie mtu kwa sababu ya chama na siyo kwa sababu watu wanamkubali. Hata hivyo, hata wana CCM wengine ambao wanatambua nguvu ya kura zao hawatamchagua mtu huyo kwani ni dhamira zao zitakazokuwa matatani.

Hivyo, uchaguzi huu wa Busanda hauhusu hisia, na vionjo, na kwa hakika hauhusu chama au vyama, unahusu maisha ya baadaye ya wananchi wa Busanda na taifa kwa jumla.

Wananchi wa Busanda wanatakiwa kujiuliza swali hili muhimu: Ni nani ambaye kweli ataweza kuwapigia kelele Bungeni na ambaye atakuwa tayari pia kuweka maslahi ya taifa mbele kuliko ya chama chake? Ni nani atakuwa tayari kupigana na wapambanaji wengine katika vita hivi dhidi ya ufisadi? Hakika si mgombea wa CCM.

Hivyo, ni uchaguzi rahisi kwa wananchi wengi kwani katika hali duni ya maisha yao, na katika kusahauliwa kwao kuna kitu kimoja ambacho hawajakipoteza bado: uhuru wao.

Ndiyo uhuru huu ambao watautumia kumchagua kiongozi wanayemtaka hata kama CCM na vyombo vyake vya dola watasimama na kuwatisha kwa sauti kali na kuleta kundi la wapiga debe wake.

Ukweli ni kuwa Busanda imeamka na hailali tena. Endapo CCM watapoteza Busanda mwaka huu ndiyo itakuwa dira ya uchaguzi mkuu Oktoba mwaka kesho.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: