Busanda 'waporwa ushindi'


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 26 May 2009

Printer-friendly version
Uchambuzi
Kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Busanda

KAMPENI za uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Busanda, mkoani Mwanza zimemalizika kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutangazwa mshindi.

Wala hakuna ubishi kwamba wiki tatu za kampeni za uchaguzi huo zilikuwa ngumu kwa chama hicho ambacho kipo madarakani kwa karibu nusu karne.

Uchaguzi wa Busanda umefanyika kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Faustine Kabuzi Rwilomba aliyefariki dunia miezi miwili iliyopita.

Uchaguzi huu, pamoja CCM kuibuka kidedea, umedhihirisha kuwa chama hiki kikongwe kinakabiliwa na kibarua kigumu huko kiendako.

Wala viongozi wa CCM hawawezi kujitapa kwamba bado wako imara kwa kushinda uchaguzi huu wa Busanda. Hili linathibitishwa na jinsi chama kilivyoendesha kampeni zake.

Kuna madai kuwa baadhi ya viongozi wa chama hiki walilazimika kutisha wananchi wakiwamo wachimbaji wadogo wa madini kuwa iwapo hawataichagua CCM wataondoshwa katika maeneo ya migodi.

Anayetajwa kuendesha kampeni hiyo, ni William Ngeleja, waziri wa nishati na madini. Hatua ya Ngeleja inatokana na kile kinachoitwa, kuulizwa maswali ya msingi na ambayo yeye (Ngeleja) hakuyategemea, na hakuwa na majibu nayo.

Mathalani wachimbaji hao walimuuliza Ngeleja wakati akihubiri kile alichoita, “Sera ya serikali ya kulinda wachimbaji wadogo,” kwamba serikali ilikuwa wapi hadi ikasubiri mbunge wao Rwilomba aage dunia ndiyo ijitokeze na kusema itatoa maeneo kwa wachimbaji wadogo?

Hicho ndicho kinachodaiwa kuwa kilimfanya Ngeleja kutisha kwa kusema, “Msipoichagua CCM mtafutiwa leseni za uchimbaji na serikali itatumia Mamlaka ya Mapato TRA kukagua kama mnalipa kodi.”

Ngeleja hakuishia kutisha wachimbaji wadogo peke yake. Amenukuliwa akiwaambia wananchi wa Busanda kwamba iwapo watamchagua mgombea wa Chadema, basi hatatoa kibali cha mradi wa umeme wa jua ambao mgombea wa Chadema ameahidi.

Hivi havikuwa vitisho vidogo. Ni vitisho vikubwa na vinavyotosha kulazimisha wananchi kuchagua chama wasichokipenda.

Lakini swali moja muhimu la kujiuliza ni kwa nini CCM wamelazimika kutumia nyundo kuua sisimizi?

Jibu ni dhahiri. Kushindwa kwa serikali ya CCM kutatua matatizo ya wananchi, pamoja na kunyamazia vitendo vya ufisadi, ndiyo chanzo cha chama hiki kufika kilipo sasa.

Kwa kuzingatia idadi ya kura ambazo CCM imetangaziwa, umri wake kwenye madaraka na mtandao wake mkubwa, lazima ionekane kuwa yalikuwa maji shingoni.

Ilibidi CCM itumie nguvu zote kwa vile ilijua wananchi wanajua kuwa chama hiki kimewahidi; kimewahadaa miaka mingi na kwa njia mbalimbali kimewapora hata utajiri wao.

Hata kitendo cha mawaziri wa serikali kuacha ofisi za umma na kuhamia Busanda kuhadaa wananchi, kilionekana wazi kwa wana-Busanda na taifa zima.

Ahadi ambazo watawala wameshindwa kutekeleza kwa miaka 40 ndizo CCM na serikali yake vimewapa mawaziri na wapiga debe wake wengine waende kuwahadaa wananchi.

Iwapo watatokea watu na kusema uchaguzi ulikwenda vizuri na uliendeshwa kwa misingi huru na haki, hao watakuwa ama wameishia tu kuangalia zoezi la upigaji kura na matokeo, au watakuwa wameamua, kwa makusudi kufumbia macho yaliyotokea.

Lakini kwa kweli, zoezi zima la uchaguzi huu lilivurugwa na CCM. Wananchi hawakupewa nafasi ya kuchagua mgombea wanayemtaka. Vitisho vilikuwa vingi.

Kutokana na hali hiyo, ukichukua matokeo yaliyopatikana na ukachanganya na vitendo vya wazi na vile vya siri vilivyofanyika wakati wa kampeni na hata wakati wa kuhesabu na kujumlishaji kura, utabaini mara moja kuwa CCM kinateketea mithili ya mti unaotafunwa na mchwa.

Kwa miaka nenda rudi serikali imeshindwa kuwapatia wachimbaji wadogo wa dhahabu maeneo ya kuchimba madini. Kata 13 za Busanda zina utajiri mkubwa wa madini.

Hata wachimbaji wakubwa ambao serikali imekuwa ikiwakumbatia kwa miaka yote, nao wameshindwa kusaidia wananchi wa maeneo haya ya migodi.

Badala yake wananchi wanashuhudia ndege kubwa na ndogo zikitua katika maeneo yao kuchota rasimali za nchi yao na kutokomea nazo.

Hakuna mahali popote ambapo wananchi hawa au taifa linaweza kusema kwamba  limenufaika na rasilimali yake.

Ukiondoa mrahaba wa asilimia tatu inayotolewa katika madini na pipi wanayolambishwa viongozi kwa kuchimbiwa mashimo ya choo katika shule na ujenzi wa kuta za shule, hakika taifa hili halina kubwa la kujivunia.

Ndiyo maana mpaka sasa, Busanda pamoja na utajiri wake mkubwa iliyonayo haina umeme. Umasikini kwa wananchi umekuwa mkubwa kuliko ilivyokuwa kabla ya uhuru.

Haya yote yanatokea kutokana na mipango na sera mbovu za serikali ya chama kilichopo ikulu.

Kuna hata madai ya baadhi ya mawaziri waliokuwa wanapiga kampeni kugawa rushwa ya chumvi, sidiria na chupi kwa kina mama na vyandarua. Hata Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Luis Makame amelikemea hilo akisema ni kosa la jinai.

Lakini ukiacha hilo, kuna hili la CCM kupoteza umiliki wa maeneo ya mijini ambako ndiko wapigakura wengi waliko.

Hata Mkuu wa Kitengo cha Parapaganda cha CCM, Mbarouk Msabaha Salum, anakiri kuwa Katoro ambako ndiko walipo wapigakura wengi, Chadema imepata kura nyingi kuliko chama chake.

Katika maeneo maarufu na yenye watu wengi kama Rwamgasa, Bukoli, Nyakabale, Kamena, CCM imepata upinzani mkubwa.

Haya ni maeneo ambayo yamekuwa yakiishi katika giza kutokana na serikali kushindwa kupeleka umeme. Hata wananchi wake wanakabiliana na hali ngumu kiuchumi.

Kutokana na hali inavyokwenda na kutokana na mwamko wa wananchi wa kujua haki zao, ni vema CCM ikaanza kupuuza kauli za baadhi ya makada wake kama vile George Mkuchika.

Ni Mkuchika aliyesema Watanzania wengi wanaoishi vijijini hawapati nafasi ya kusoma magazeti, wala kusikiliza redio na kuangalia televesheni; na hivyo hawana mwamko wa kujua haki zao.

Kwa kuzingatia maisha duni ya wengi huko Busanda; kwa unyonyaji wa kikatili unaofanywa na makampuni ya madini kwenye ardhi ya Busanda, huwezi kutegemea wananchi wachague chama ambacho kimekuwa mfereji wa kupitishia dhiki zinazowakabili.

Hapa hakuna haja ya kuongelea vyama. Ukweli ni kwamba, wananchi wa Busanda wameporwa ushindi. Ghiliba, vishawishi na vitisho, vimetumika kupora ushindi wa wananchi.

Je, ghiliba ina uwezo wa kuishi kwa miaka mingapi?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: