Busara imtume Nchunga kujiuzulu


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 09 May 2012

Printer-friendly version

MWENYEKITI wa klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam, Lloyd Nchunga atabaki kuwa kiongozi kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lakini amepoteza mashiko.

Nchunga amepoteza mvuto, hana ushawishi wowote klabuni, haungwi mkono na wazee na wanachama, na matokeo uwanjani yamemnyima ujasiri.

Wakili huyo wa kujitegemea anaweza kuendelea kujiita mwenyekiti wa Yanga, lakini mazingira yanaonyesha ni kiongozi asiye na mamlaka.

Amebaki mpweke, wajumbe alioingia nao madarakani wanajiondoa na waliompigia debe awe mwenyekiti mwaka 2010 wanamgeuka.

Klabuni hawaelewani kwa sababu yake, hawana ujasiri mbele ya watani zao, wanatembea wameficha nyuso na hawana raha kwa vile alikataa ushirikiano na “wenye” klabu kupitia kwa wazee.

Nchunga ndiye mwenye funguo za kurejesha utulivu na amani klabuni akitaka, lakini asipotaka kwa hali ilivyo, akabaki ameng’ang’ania kanuni za TFF ataitumbukiza klabu hiyo kwenye mgogoro mkubwa wa kiuongozi.

Namshauri Nchunga atumie ufunguo huo kuruhusu amani kwa yeye kutangaza kujiuzulu kwa hiari yake ili wenye klabu wajue wanamkabidhi nani. Akijiuzulu basi awajulishe TFF.

Hii ndiyo njia bora, na atapongezwa na wanachama na hata wazee watamsifu. Hofu yangu ni kwamba kwa hali ilivyo, akikataa ataporwa timu, hatakuwa na maamuzi, watamdhoofisha; atabaki kuwa mwenyekiti kwa mujibu wa kanuni za TFF lakini si kwa ridhaa ya wanachama.

Wazee wanataka timu yao wampe mwingine. Waliitaka kabla ya mechi dhidi ya mnyama Simba lakini Nchunga alikataa kwa vile yeye ndiye anatambuliwa na TFF.

Ni kweli. Lakini ile ni fursa aliyopoteza Nchunga. Laiti angekubali “kukabidhi” kwa muda bado Yanga ikalala doro angesifiwa kwa uungwana, lakini alikaidi – wenye timu wanataka timu yao na yeye akae pembeni.

Uongozi ni kipaji na busara. Si kila mtu aliyecheza soka anaweza kuwa kiongozi mzuri au kocha mzuri, vivyo hivyo, si kila aliyesomea uongozi anaweza kuwa kiongozi mzuri.

Aliposhinikizwa na baadhi ya wanachama ajiuzulu kabla ya mechi yenye matokeo ya aibu dhidi ya Simba, Nchunga alikaririwa akidai hataki kuacha klabu katika mikono ya wafanyabiashara ya unga. Najua Nchunga ni wakili, lakini sina hakika kama alipima uzito wa maneno hayo.

Maswali yanakuja, nani kati ya wanaotaka ajiuzulu ni wauza unga? Kama anawajua amewahi kusaidia polisi kuwanasa watu hao? Je, uongo si kosa la jinai?

Nchunga inabidi ajitathmini kama ana kauli ya mwisho katika masuala ya uongozi. Je, uongozi wake ulihusika kumwajiri Sam Timbe au alijitokeza ‘kibopa’ pembeni? Je, ni wao waliomtimua Timbe aliyeipa taji msimu wa 2010/ 2011 na kumrejesha Kostadin Papic?

Katika kipindi muhimu cha maandalizi ya Ligi Kuu ya Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ilikuwa hoi kifedha – kocha na wachezaji walikuwa wanalia njaa.

Yanga ilitolewa asubuhi kweupe. Katika hatua muhimu ya kutetea ubingwa, mzunguko wa pili Yanga ni kama haikuwa na viongozi wajuzi wa soka – sheria na kanuni.

Mzunguko wa pili kikawa kipindi cha kupoteza pointi na hasira juu. Ikalala 3-1 mbele ya Azam FC; ikaachia pointi tatu na mabao 3-0 kwa Coastal Union kwa kosa la kumtumia Nadir Haroub ‘Canavarro’; ikadunguliwa 1-0 na Toto; ikasulubiwa 1-0 na Kagera, ikaambulia ushindi wa mabao 4-1 kwa Oljoro JKT kabla ya kufunga msimu wa Ligi Kuu ya Bara kwa kuraruriwa na mnyama 5-0 Jumapili iliyopita.

Matokeo haya hayawezi kumpendeza shabiki yeyote wa klabu ya Yanga hasa inapotokea kuwa ni kutokana na uzembe wa viongozi wao.

Nchunga itabidi atazame matokeo hayo na awape jibu ambalo wanachama wanataka kusikia. Kama hajiuzulu ana mikakati gani ya kubadili aibu ya mwaka huu kuwa faraja mwakani?

Ni kweli Yanga haiwezi kushinda kila mechi, lakini viongozi hawajui mchezaji mwenye kadi nyekundu anatakiwa kutocheza mechi ngapi?

Vilevile ni kweli Yanga haiwezi kushinda kile mechi lakini viongozi gani hawajui mshikamano wa kiuongozi kabla ya mchezo mgumu kama ule dhidi ya watani wao wa jadi, Simba?

Mwisho narudia ushauri nilioutoa katika makala ya “Yanga waambulia kuizomea Simba” kwa kuwataka wazee waonyeshe busara wadhibiti kwanza viongozi wanaojiuzulu ovyo, warejeshe mshikamano, nidhamu, wasome kanuni, wajue mipaka yao ili kuepusha vurugu.

0789 383 979
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: