Busara ya piga, jeruhi, tia jela


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 16 November 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

KATIKA ziara yake ya kwanza mkoani Mbeya, Oktoba 2008, msafara wa Rais Jakaya Kikwete ulizuiwa Mwanjelwa.

Bila ya kujali wingi wa polisi wakiwa na magari ya ving’ora, umma wa vijana ulikusanyika Mwanjelwa na kumzuia rais kupita.

Rais alilazimika kusimama na kuhutubia kutokea juu ya gari lake. Aliomba vijana waunde kamati na kuratibu maoni ya shida zao na kuyawasilisha kwa mkuu wa mkoa (RC). Alitaka akabidhiwe anapohitimisha ziara yake wilayani Mbarali.

Vijana waliandaa taarifa na kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wakati ule, John Mwakipesile. Akaifungia kabatini.

Ikumbukwe, wakati Rais Kikwete anarejea mjini Mbeya baada ya kukamilisha ziara yake wilayani Chunya, kiza kikiwa kimeanza, msafara wake ulipigwa mawe kijiji cha Kanga.

Haraka Mwakipesile alidai matukio hayo yalichochewa kisiasa wakati Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu alidai kuwa walioshambulia msafara walikuwa walevi.

Nilitumwa kuchunguza chimbuko la matukio ya Mwanjelwa na Kanga. Ukweli ni kwamba, tukio la Mwanjelwa lilihamasishwa na wafanyabiashara ndogondogo japo upepo wa kisiasa ulivuma vibaya kwa Prof. Mark Mwandosya aliyetupwa kinyang’anyiro cha urais 2005 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tukio la Kanga lilitokana na mvutano wa kisiasa ndani ya uongozi wa serikali ya kijiji chini ya CCM.

Siku ya tukio, uongozi ulioondolewa, uliwatumia baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kanga, kuupiga mawe msafara ule. Baada tu ya shambulio, watoto na vinara wa shambulio walitoroka. Alfajiri, wakazi wa Kanga waliamshwa kwa virungu vya FFU.

Wiki iliyopita, Mwanjelwa ililipuka tena. Walioanzisha ni wamachinga walewale na kilio ni kilekile kunyimwa maeneo ya kufanyia biashara kama alivyoambiwa Rais Kikwete mwaka 2008.

Mkuu mpya wa mkoa, Abbas Kandoro akafungua faili la sababu aliloacha Mwakipesile akadai kuwa vurugu zile zimechochewa kisiasa.

Msisahau, Kandoro na mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Wilson Kabwe ndio walikuwa kiini cha vurugu Jiji la Mwanza na mkuu wa wilaya Evans Balama ndiye alikuwa Ilala.

Safari hii Kandoro atashikilia hoja hiyo kwa nguvu kwa vile, baada ya wamachinga kujihami kwa ‘nguvu ya umma’, alipeleka polisi, FFU, askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Wananchi kujibu hoja za wamachinga kwa virungu, risasi na pingu.

Wote walihangaika kwa siku mbili bila mafanikio hadi alipofika Joseph Mbilinyi ‘Mr Sugu’, Mbunge kijana na aliyefikia mafanikio hayo baada ya kuhangaika sana na hata serikali kupuuza malalamiko ya ‘wizi katika fani ya muziki’, alikusanya umati wa wamachinga na kuwatuliza kwa mistari ya ‘hip hop’ tu.

Ndiyo, Mbunge wa Mbeya Mjini, Bw. Joseph Mbilinyi ni wa CHADEMA. Mr Sugu ametumia silaha gani kutuliza vijana wale? Amepiga risasi ngapi? Alitumia jeshi la wapi kurejesha amani na utulivu Mwanjelwa?

Kandoro anaposema vurugu za Mbeya zilichochewa kisiasa, anataka kueleza kwamba wamachinga wote wa Mwanjelwa ni wafuasi wa CHADEMA? Hivi hakuna vijana wa CCM wasiotaka kubughudhiwa katika biashara zao?

Kama wamachinga wote ni wafuasi wa CHADEMA, kwa hiyo aliona busara ni kutuma JKT na JW kuua raia?

Viongozi wote wa aina ya Kandoro, RC mwenzake wa Arusha, Magessa Mulongo, na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wanaodhani busara ya “piga, jeruhi, tia jela” ndio uongozi mwema, wajue wanachochea watu waichukie serikali. Shida kubwa, viongozi wamesahau uongozi wa majadiliano.

0658 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet