Bwege: CCM wajiandae kuwa wapinzani


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 05 October 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

ALIPOKUWA akilalamikia viongozi wa serikali kwa kujenga na kulea mfumo wa kuuza mazao unaonyonya wakulima, Seleman Said Bungara alionekana “bwege” kweli.

Leo, miezi mitatu baada ya kushutumu utawala bungeni mjini Dodoma kwa mfumo huo unaonyonya wakulima wa ufuta wa Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, anajivunia mabadiliko.

Bungara, mbunge wa Kilwa Kusini kupitia Chama cha Wananchi (CUF), amesema katika mahojiano maalum hivi karibuni na MwanaHALISI yaliyofanyika Dar es Salaam , serikali imelegeza kamba.

Imeachia wakulima wauze ufuta kwa wanunuzi wawatakao na ambao wanatoa bei yenye maslahi kwa pande zote mbili.

Bungara alilalamika wakati wa mjadala wa makadirio ya matumizi ya bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika bungeni, akisema utendaji dhaifu wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) umeimarisha upinzani.

Alisema wakati taifa linaelekea kusherehekea miaka 50 ya uhuru, CCM imeshindwa kuondoa ujinga, maradhi na umaskini hivyo kusababisha wananchi kuishi kwa shida.

Bungara alianza kama utani kuibeza CCM kwa kushika dola kwa nusu karne, lakini ikiendelea kuanda bajeti inayotegemea misaada ya nje kwa zaidi ya asilimia 30.

“Miaka 50 ya Uhuru bado hatujaweza kujitegemea, Mwalimu Nyerere (Julius Kambarage Nyerere) alisema asiyeweza kujitegemea hayupo huru…Ni bora tu wajiandae kuwa wapinzani 2015,” alisema Bungara.

Bungara alikuwa anajenga hoja kutetea wakulima wa ufuta wa jimboni kwake na Kilwa nzima; akishutumu viongozi wa serikali kwa kuwazuia kuuza ufuta kwa bei nzuri.

Alisema matokeo ya kikwazo hicho, ni raha kwa sababu, “yamesaidia kujenga upinzani imara wilayani Kilwa.”

Bungara alitaja viongozi wa serikali waliokataa kuwajibika kusaidia wakulima hao.

“Nilimwandikia barua Waziri Mkuu, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kuwajulisha kuwa wakulima wa Kilwa wanaonewa, sijajibiwa mpaka leo.

“(Wakubwa hao) wanamuogopa Mkuu wa Mkoa,” alisema na kuapa: “Sitachoka, nitapigania haki za wakulima na kuhamasisha maandamano ya kudumu mpaka waruhusiwe kuuza ufuta wao kwa uhuru na bei nzuri.”

 “Kuna kikundi kidogo cha watu kinaongozwa na Mkuu wa Mkoa kuwanyonya wakulima wa ufuta. Haiwezekani wakulima wazuiwe kuuza ufuta wao kwenye bei nzuri.

Bungara alimtaja Sadik Meki Sadik aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Lindi ambaye sasa ni mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam , kuwa kinara wa mfumo huo.

Leo, Bungara anasema kilio chake kimesikika. Serikali imeachia wakulima wauze ufuta watakavyo.

Vyama vya ushirika vimepandisha bei hadi Sh. 1,500 kwa kilo; na tunao wafanyabiashara binafsi waliokuwa tayari kununua ufuta kwa bei kubwa kuliko bei iliyotangazwa na serikali lakini wakikataliwa na serikali.

Bungara hakuweza kutaja kiasi gani wakulima wameshapata kwa sasa, lakini, anasema: “Sasa ni raha tupu. Kidogo presha imepungua. Wakulima nao wamepumzika kunung’unika.”

Hata hivyo, wakati Bungara anafurahia mafanikio hayo, zile kauli zake zilichukiza baadhi ya viongozi CCM.

Anamtaja Nape Nnauye, katibu wa itikadi na uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kama mmoja wapo.

Nape amekaririwa akimuita Bungara ni muongo aliyetoa malalamiko ili kutetea maslahi yake; anafanya biashara ya ufuta. Pia Bungara anamkariri Nape alimuita mbunge huyo “mlanguzi na mwizi.”

Tuhuma hizo zinamsukuma Bungara kuandaa kumshitaki Nape mahakamani kwa madai ya kumdhalilisha. Anasema kesi hiyo ipo kwa wakili Twaha Taslima.

“Nape amenidhalilisha mbele ya wananchi na chama changu. Ameniita mlanguzi na mwizi. Unajua maana ya mlanguzi? Maana yake ni mhujumu uchumi. Hivi ninapotetea wakulima nahujumu uchumi,” anahoji.

 “Sijawahi kushiriki katika biashara ya ufuta isipokuwa ninachofanya ni kusimamia maslahi ya wakulima,” anasema.

Bungara anasema kitendo chake cha kutembelea vijiji 10 na kata tano wilayani na kuhamasisha wakulima kupinga dhulma inayosimamiwa na viongozi wa mkoa, kimekasirisha CCM na kumjia juu.

Katika ziara yake hiyo alifanikiwa kupata wakulima 2,599 waliosaini tamko la kugomea mfumo wa kunyonya wakulima.

Bungara anayezungumza huku akichezesha mikono na kusita akipanga hoja, alikomaa tena wakati wa mjadala wa makadirio ya Wizara ya Maji.

Anasema serikali haiwaelezi wananchi ukweli kuhusu tatizo la maji. Huko ni kujichimbia kaburi kisiasa.

Bungara anapinga takwimu za wizara kwamba asilimia 57.8 ya wananchi wa vijijini wanapata maji safi na salama.

“Ni dalili ya unafiki. CCM ni ‘longolongo’. Wananchi katika jimbo langu wananunua debe moja la maji kwa shilingi 500. Hivyo hata kama mwananchi akitumia kiasi hicho kwa siku, kwa mwezi anatumia shilingi 150,000 kwa ajili ya maji tu.

“Maskini wa Tanzania atapata wapi (fedha hizo) ili apate maji safi na salama,” anahoji Bungara akihofia wananchi wanaopata huduma hiyo huenda wasifike hata asilimia 10.

“Nashindwa kuelewa. Hivi sisi wa Kusini tumekosa nini. Tunaomba serikali ya CCM itukumbuke na ituheshimu watu wa Kusini,” anasema.

Analalamikia matatizo yanayoikabili sekta ya elimu wilayani ikiwemo uhaba mkubwa wa walimu wa shule za sekondari. Anasikitika kuwa wananchi wamekata tamaa ya matatizo hayo kupata ufumbuzi.

Anatoa mfano wa sekondari ya Likawage yenye mwalimu mmoja tu wakati ina wanafunzi wa kidato cha kwanza mpaka cha tatu.

“Mwalimu huyu akifuata mshahara Kilwa Masoko, shule inafungwa. Unatarajia watoto watafaulu mtihani katika hali kama hii,” analalamika.

Anashangaa kuzuiwa na halmashauri kuhangaikia walimu mbadala. “Sijachoka kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayotukabili. Nitapambana… najua wanavyuo wanazuiwa kwa sababu wameletwa nami mbunge wa CUF. Hii ndiyo serikali ya CCM,” anasema.

Bungara anakubali kuitwa Bwege, jina la utani, japo anajua maana halisi ya neno hili – mtu lofa au hohehahe.

Anasema limekuwa likitumika tangu alipokuwa shule ya msingi ya Kivinje, wilayani Kilwa na analichukulia hivyo kwa kuamini, “Kwa mwoga hwenda kicheko na kwa shujaa hwenda kilio.”

Bungara anasema ulofa huohuo ndio uliomwezesha kumbwaga Ramadhani Madabida, kada maarufu wa CCM katika ubunge mwaka 2010.

Bwege aligombania kiti cha Kilwa Kusini alipoona wakati anatimiza miaka 50 ya kuzaliwa, ‘rafiki’ yake, Tanzania , anakwenda kusherehekea miaka hiyo akiwa mnyonge.

Nchi inakabiliwa na umasikini mkubwa; sehemu nyingi hakuna miundombinu imara ya barabara, umeme na hospitali hazina dawa za kutosha na vifaa tiba.

Bungara alizaliwa 18 Novemba 1961, wiki tatu kabla ya uhuru wa Tanganyika , akiwa mtoto wa pili kwa familia ya Said Ally Bungara (marehemu) na Salama Seleman Ngonole. Watoto wao ni 11.

Lakini baba yake, aliyekuwa mwalimu, alikuwa na mke mwingine alikopata watoto wengine 18.

Bungara alijiunga na siasa mwaka 1992 akiwa Tanzania Democratic Alliance (TADEA). Mwaka 1993 akaingia CUF na baadaye kuchaguliwa mwenyekiti wa wilaya ya Kilwa.

Hakuingia katika siasa kwa bahati mbaya. Baba yake alikuwa mbunge kwa miaka 15 kuanzia 1965.

“Baba alikuwa mbunge wa enzi za mwalimu. Walitumia usafiri wa baiskeli kutoka Kilwa hadi Ikwiriri,” anasema. Mama yake alikuwa mama wa nyumbani.

Kwa sasa, ubunge wake unapingwa na Madabida aliyefungua kesi Na. 4/2010 katika Mahakama Kuu Lindi.

0
No votes yet