CAG: NSSF hatarini kufilisika


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 18 April 2012

Printer-friendly version

MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) uko hatarini kufilisika na kupoteza fedha za wanachama wake.

Hii inatokana na serikali kushindwa kurejesha katika mfuko huu, mabilioni ya shilingi iliyokopa au kudhamini katika miradi mbalimbali.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya 2010/2011, fedha za wanachama, hata katika mifuko mingine ya jamii, ziko hatarini kupotea.

Mbali na NSSF, mifuko mingine inayotajwa kuwa katika hatari hiyo ni Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF); Mfuko wa Wafanyakazi wa Serikali Kuu (PSPF), Mfuko wa Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (LAPF) na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF).

Kulingana na taarifa ya CAG, sehemu kubwa ya fedha za wanachama ambazo hazijarejeshwa, zilikopeshwa kwa serikali kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Katika chuo hiki, NSSF peke yake iliingiza Sh. 234.1 bilioni. Mifuko iliyosalia ilitoa jumla ya Sh. 181.3 bilioni.

Katika ujenzi wa UDOM, PPF ilitoa Sh. 39.99 bilioni, PSPF (Sh. 105.9 bilioni), LAPF (Sh. 22 bilioni) na NHIF (Sh. 13.4 bilioni). Fedha hizo na riba yake hazijarejeshwa.

Ripoti ya CAG, Ludovick Utouh, inasema kutorejeshwa kwa mikopo hiyo, iliyochukuliwa au kudhaminiwa na serikali, ni kinyume cha sheria ya udhamini ya mwaka 1974.

“Kutolipika kwa mikopo hii iliyodhaminiwa na serikali kunaiweka mifuko hii ya hifadhi katika hatari ya kupoteza fedha za wanachama na kuhatarisha uwezo wa mifuko kufanya uwekezaji zaidi,” anasema na kuongeza:

“Kushindwa kulipa madeni taasisi hizi ambazo baadhi yake zilipata udhamini wa serikali, kunatia shaka iwapo upembuzi wa kina wa wakopaji ulifanywa na mifuko ya kijamii kabla ya kutoa mikopo hiyo.”

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau hakupatikana kwa maelezo kuwa alikuwa kwenye mkutano mkoani Mbeya.

Lakini Meneja Kiongozi Uhusiano wa NSSF, Eunice Chiume amesema mikopo kwa serikali imetolewa kwa uangalifu na inalipwa bila matatizo na kwa misingi ya kibiashara.

“Mikataba ya kisheria imesainiwa kukidhi mazingira mbalimbali ikiwa ni pamoja na iwapo itacheleweshwa…. Hakuna hatari yoyote ya fedha kutolipwa wala kupoteza fedha za wateja,” amesema Chiume.

Lakini CAG katika taarifa yake ya kurasa 183, anasema, “Ukubwa wa kibiashara kati ya serikali na mifuko unatia shaka kutokana na kusuasua kwa serikali katika ulipaji madeni yake. Hii inahatarisha uendelevu wa mifuko hii.”

Katika ukaguzi wake, CAG amebaini kuwa NSSF ilitoa Sh. 234.1 bilioni kwa mradi wa UDOM, lakini mkataba uliosainiwa ni wa Sh. 35.2 bilioni tu. Hii ni hatari kwa fedha za wafanyakazi na wastaafu.

Akifafanua suala la fedha kwenye mkataba kutofautiana na fedha zilizotolewa, Chiume alisema mkataba ulitakiwa kuwa mmoja ambao ulisainiwa wakati wa awamu ya kwanza.

Chiume alisema kwa awamu ya pili, kilichotakiwa ni kusaini addendum (makubaliano ya nyongeza), ambayo “yako mbioni kukamilika.”

Utouh anaripoti, “Majengo kwa ajili ya awamu ya kwanza yalikamilika na kuwekwa katika matumizi mwezi Septemba 2008. Mpaka wakati wa ukaguzi 2010/2011, mfuko ulikuwa haujafanikiwa kukusanya malipo ya pango kutoka serikalini.

Kwa msingi huo, hadi sasa limbikizo la riba limefika thamani ya Sh. 14 bilioni,” anasema Utouh.

Mkopo huo ulitolewa kwa utaratibu wa kubuni, kujenga, kumiliki na kuhamisha ambapo mfuko ungepokea kodi iliyokokotolewa kwa riba ya asilimia 15 kwa kipindi cha miaka kumi.

Vilevile CAG amebaini kuwa majengo yaliyojengwa kwa mkopo huo, hayako kwenye vitabu vya UDOM wala katika vitabu vya NSSF, kutokana na uelewa tofauti uliopo kati ya pande mbili zinazohusika.

Kuna mikanganyiko katika uelewa kwa serikali na mifuko ya hifadhi, ameeleza CAG. Wakati mifuko inasema fedha zilizotumika kujenga majengo hayo zilikuwa mikopo kwa serikali, yenyewe serikali inadai fedha hizo ni uwekezaji wa kawaida wa mifuko hiyo.

Mbali na UDOM, serikali pia haijalipa jumla ya Sh. 19.77 bilioni zilizotumika katika ujenzi wa ukumbi wa bunge, ambazo hazilipwi kulingana na makubaliano. Hadi wakati wa ukaguzi, NSSF ilikuwa inadai Sh. 8.96 bilioni, PPF (Sh. 7.9 na LAPF Sh. 2.91.

Pia upo mkopo mwingine wa NSSF wa Sh. 5.33 bilioni na riba ya asilimia 15 kwa miaka kumi, uliotolewa kwa ajili ya ujenzi wa “taasisi ya serikali ya kiusalama” mwaka 2007.

Mfuko mwingine uliowekeza katika mradi huo ni PSPF uliotoa Sh. 6.4 bilioni.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, NSSF kwa udhamini wa serikali ilikopesha taasisi kwa shughuli mbalimbali.

Kwa mfano, ujenzi wa nyumba za polisi kwa Sh. 20 bilioni na Sh. 12. 9 bilioni kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam mwaka 2007 kwa ajili ya ujenzi wa Machinga Complex, Ilala.

“Hadi sasa hakuna malipo ya riba wala sehemu ya mkopo hiyo yaliyofanywa. Hii ni kinyume cha mkataba,” inasema sehemu ya ripoti ya CAG.

Kwa upande wa Machinga Complex, hadi tarehe 30 Juni 2011, mkopo na riba yake ulikuwa umefikia Sh. 15.3 bilioni.

Ripoti ya CAG imeainisha pia mikopo mingine ambayo hailipwi kulingana na mikataba ya mifuko hiyo, bila ya kutaja viwango vyake.

Mikopo hiyo ni iliyotolewa kwa Continental Venture (T) Limited, Meditech Industrial Co. Ltd, General Tyre (GT), Kiwanda cha Sukari Kagera, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) na mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio amesema hajaona ripoti ya CAG na yuko safarini Tanga.

Hata hivyo amedokeza kuwa hivi karibuni walikaa na CAG kujadili suala hilo na kubaini makosa ya kifundi katika uhasibu baina ya mifuko na serikali katika ujenzi wa UDOM; hivyo CAG kuahidi kuyashughulikia kwa upande wa serikali.

Alipoulizwa ni makosa yapi hayo, Erio alimtaka mwandishi awasiliane na kaimu wake, Stephen Alfred ambaye ilielezwa kuwa yuko kwenye mkutano. Hadi tunakwenda mitamboni, Alfred hakupatikana.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)