CCM ‘imejiua’, inasubiri kuzikwa


John Kibasso's picture

Na John Kibasso - Imechapwa 13 June 2012

Printer-friendly version

POLISI wa kitengo cha barabarani (trafiki) anapopata taarifa ya ajali, kitendo cha kwanza huwa ni kwenda kwenye eneo la tukio. Akifika atapima ilipotokea ajali ili kubaini chanzo na mkosaji.

Hatua ya trafiki kupima eneo la ajali inamsaidia kugundua aliyesababisha ajali, bila upendeleo wala uzushi.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) walitakiwa kuiga mfano wa trafiki, wafanye utafiti wa kina zaidi ili kubaini chanzo cha mdororo ndani ya chama, bila upendeleo wala uzushi. Utafiti huo ulipaswa kuanzia ngazi za chini na siyo ngazi ya taifa tu.

Bila kutafuta maneno, mgogoro ndani ya CCM ulikuzwa na kupata nguvu baada ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutoa baraka zao kuenguliwa kwa kamati kuu (CC) na sekretarieti nzima ya Katibu mkuu, Yussuf Makamba. Mpasuko ulishika kasi tangu siku ile.

Baada ya CC kujiridhisha na utafiti uliozaa falsafa ya “kujivua gamba” na kwa bahati mbaya au kwa maksudi, bila kutafakari madhara ya upande mwingine, waliamua kuining’niza sekretarieti ya Makamba bila huruma ili kuwachuna gamba. Dhambi ya kuning’iniza sekretarieti ya Makamba, bila utafiti wa kina, mpaka leo haijapoa na ndiyo inaitafuna CCM kwa kasi kubwa.

Sekretarieti mpya ikaja na kauli mbiu ya kuwatosa mafisadi ndani ya chama badala ya kushughulikia matatizo ya msingi. CCM ikaanza kukiri hadharani, kwamba wapo mafisadi miongoni mwa wanachama wake ambao ndio chanzo cha chama kupoteza haiba mbele ya jamii.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya siasa wanadai tatizo haikuwa sekretarieti ya Makamba wala mafisadi, bali tatizo kubwa ilikuwa na bado ni ni hali duni ya maisha ya viongozi wa ngazi za chini – tawi na kata. Huko ndiko uhamasishaji wa wanachama unakoanzia. Wapiganaji hawa wa chini wamepoteza ari ya kupambana na wapinzani wao.

Kilio kikubwa cha wapenzi na viongozi wa CCM ngazi za chini ni ukosefu wa vitendea kazi maofisini kwao, kupiga debe nyakati za kampeni, kutothaminiwa tena kampeni zikiisha, kukosa ruzuku, na ngazi za juu kukwapua mapato madogo wanayopata.

Kusema ukweli, kazi ya kwanza ya sekretarieti mpya ya CCM ingelikuwa kurekebisha matatizo haya ya viongozi wa ngazi za chini. Badala yake wakaanza kutembea nchi nzima wakikisulubu chama kwamba kimejaa mafisadi.

Viongozi wengi ngazi za kata, tawi na shina wamekuwa wakilia na viongozi wao wa juu ambao kipindi cha kampeni kinapofika, wamekuwa wakitoa ahadi nyingi za kuboresha maisha ya viongozi hao wa chini. Lakini ahadi hizo hazitekelezwi kila awamu ya uongozi wa juu inapoingia na kutoka madarakani.

Hali ya maisha imeendelea kupanda. Bei ya vyakula, vifaa vya ujenzi, bei ya vifaa vya kilimo iko juu, lakini watendaji hawa wa chini wamendelea kusota bila mkombozi wa kuboresha hali yao ya maisha.

Mathlani, makatibu wa kata waliahidiwa kupewa walau posho kila mwisho wa mwezi, lakini hadi leo hakuna kilichotokea.

Pamoja na kukosa posho za kila mwezi, hata hayo mapato madogo wanayopata kwenye kata, matawi nayo yanasombwa kupelekwa ngazi za juu. CCM ngazi ya  taifa inapata ruzuku; isitoshe wafanyabiashara wakubwa hapa nchini na mataifa marafiki wamekuwa wakisaidia chama. Sasa inakuwaje wanarudi kukwapua kile kidogo ngazi za chini?

Haya ndiyo matatizo ya msingi. Sekretarieti mpya ilitakiwa kurudi ngazi ya chini na kushughulikia matatizo haya. Kung’ang’ania mafisadi ambao wanatajwa na hawafiki hata kumi, huku ukiacha kushughulikia matatizo ya watu wapatao milioni mbili hapo busara iko wapi?

Kama ningebahatika kuwa mshauri wa sekretarieti mpya, jambo la kwanza ningeshauri waimarishe uongozi wa tawi hadi wilaya kwa kuongeza kifungu ndani ya katiba ambacho kitawatambua madiwani wastaafu kuendelea kuingia kwenye vikao vyote vya chama ngazi ya tawi hadi kata kutokana na nyadhifa zao walizokuwa nazo huko nyuma.

Aidha, ningependekeza wabunge wastaafu katika wilaya zote nchini, watambuliwe na kuingia kwenye vikao vyote vya chama ngazi ya kata hadi wilaya kutokana na nyadhifa zao walizokuwa nazo huko nyuma. Hatua hii itawafanya hawa wastaafu wajisikie kama bado wanaheshimiwa ndani ya chama.

Wabunge wengi wastaafu wana taaluma katika nyanja mbalimbali zinazogusa maendeleo ya jamii lakini kutokana na sera mbovu ya chama, hawatumiwi katika juhudi za kuleta maendeleo ngazi hizi za chini. Ni mstaafu gani atakubali kuendelea kujikomba kwa chama wakati hathaminiwi na wahusika waliopo madarakani?

Mbaya zaidi, kinapofika kipindi cha kampeni ndipo hapo baadhi ya wastaafu wanakumbukwa tena kwa kuombwa mchango wa kusaidia kampeni na si vinginevyo. Kampeni zikiisha wanabaki kuitwa makapi!

CCM walidhani wakiwatosa hao mafisadi wa kufikirika na kuondoa sekretarieti ya juu ndiyo lingekuwa suluhisho la matatizo. Matatizo yanayohitaji ufumbuzi yapo ngazi za chini na siyo juu hivyo, CCM ifikirie upya jinsi ya kurudisha matumaini ya viongozi wa chini na wapenzi wote.

Viongozi wa chini siyo mbumbumbu, tena wanajua kwamba siasa inalipa. Enzi za kujitolea na wachache kufaidi jasho la wengi sasa imepitwa na wakati. Hizi ni nyakati za uwazi.

Kwa staili hii ya viongozi wa juu wa CCM kuparurana hadharani eti wakidhani wanatimiza falsafa ya kujivua gamba, wajue wanapalilia njia na ngazi vyama vingine vya siasa kuwaa madaraka ifikapo 2015. Nani asiyetaka kupeperusha bendera ya nchi?

Viongozi wapo tu kwa mujibu wa katiba lakini siyo kwa mujibu wa itikadi za chama. Wengi wamekata tamaa, hawaoni mabadiliko ya kweli yakiwagusa katika maeneo yao ya kazi.

Siyo siri, sasa hakuna mikutano ya hadhara inayofanyika tena katika ngazi zote. Viongozi wanakwepa aibu kuitisha mikutano kwa sababu wanajua watakosa watu katika mikutano yao.

Kitengo cha itikadi kimekufa kifo cha mende kutika ngazi zote. Viongozi wamebaki kuviziana kimakundi, kundi lipi lianze kuitisha mikutano ya kuimarisha chama.

Viongozi wa juu kuendelea kupashana vijembe wakati ngazi za chini zikikosa viunganishi walau kwa kurudisha matumaini katika sehemu zao za kazi, inaigharimu CCM, kwani kila kukicha mipasho inaibuka na kuchukua muda mwingi badala ya kushughulikia mambo muhimu ya chama.

Hata viongozi wa chama cha KANU cha Kenya hawakutarajia kuwa kuna siku chama hicho kingekuwa chama cha upinzani. Dalili zote zilizoifikisha KANU kwenye nafasi ya kuwa chama cha upinzani zimeanza kujitokeza wazi wazi ndani ya CCM. Tusubiri.

Mwandishi wa makala hii John M. Kibasso ni kada na mbunge wa zamani wa Temeke na anapatikana kwa simu namba 0713-399004 au 0767-399004.
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: