CCM, CHADEMA wanacheza zero distance


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 11 April 2012

Printer-friendly version

KUNA vita ya kugombania nchi ambayo inaendelea. Labda niseme vizuri zaidi kuwa kuna mpambano unaendelea wa kugombania  nani atawale nchini; na katika hili hakuna urafiki, udugu, mapatano au umoja wa ulaghai.

Siyo tu tunashuhudia wanagombania nani atawale, bali pia tunashuhudia wanagombania kwanini watawale. Waua Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanajua wanachogombania lakini sijui kama Chama cha Demokrsia na Maendeleo (CHADEMA), wanafahamu kitu gani kinagombaniwa.

CCM inagombania kutawala kwani ni salama yake; kikianguka katika utawala, yaani kikiondolewa kuwa chama tawala, kutakuwa na matokeo mabaya kwa chama kama taasisi lakini vile vile kwa mtu mmoja mmoja ndani ya chama hicho.

Chama hiki kinatambua vizuri kuwa usalama wake, kama taasisi na usalama wa viongozi wake unategemea kuendelea kwake kuwapo madarakani.

Kwa muda wa miaka hamsini, CCM imefanya mambo mengi na kwa kweli kabisa yote tunayoyaona nchini yanayohusiana na utawala iwe katika nyanja za sanaa, uchumi, sayansi na teknolojia, siasa, utamaduni, kilimo na mengineyo vimefanywa chini ya utawala wa CCM.

Kama kuna mambo mazuri, na kwa hakika yapo mengi tu yamefanywa na utawala wa CCM, lakini pia kama kuna mabaya, na ni dhahiri yapo mengi, yamefanywa chini ya utawala huo huo.

Huwezi kuzungumzia kwa mfano mafanikio ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma bila kuzungumzia kufeli kwa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari kwa kiwango cha aibu.

Wala huwezi kuzungumzia kwa mfano mpango wa ujenzi wa taasisi ya moyo Muhimbili bila kuzungumzia kukosekana kwa vifaa vya kisasa katika hospitali zetu nyingi.

Aidha, huwezi kuzungumzia kujenga chuo cha kisasa cha polisi bila kuzungumzia unyanyasaji wa polisi kwa raia ambao tumeushuhudia mara kwa mara.

Hivyo, mtu anayeamua kuliangalia taifa hili kwa sasa, kwa kweli kabisa anachagua upande tu lakini atafanya makosa makubwa kuiangalia kwa upande mmoja tu.

Ni sawa na mtu anayetaka kuangalia Tanzania na kudai kuwa kuna utawala wa sheria akidai wanaotuhumiwa ufisadi wamefikishwa mahakamani wakati katika nchi hiyo hiyo waliofanya ufisadi mkubwa bado wanatembea huku wakicheua mafanikio yao.

Mtu hawezi kutuambia kuwa eti serikali inapambana na mafisadi wakubwa na kutupa mifano ya kesi zilizoko mahakamani wakati huo huo mafisadi wote na wezi wa Kagoda, Meremeta, Tangold na wanaofahamika hata kwa majina, bado wapo wanapeta kama wafalme katika nchi ya wasiojali.

Sasa vyote hivi vinaifanya CCM iwe na wakati mgumu kujihalalisha kwanini ikubaliwe zaidi kutawala tena. 

Lakini kinachotisha zaidi na ambacho naamini ni kweli – na watu wengine wanazidi kukiona – ni kuwa CCM haina mawazo mapya.

Tumeliona hili kwenye suala la shule za kata, tumeliona kwenye mpango ulioshindwa wa kilimo kwanza, na kwa hakika tumeliona katika programu nyingi tu za maendeleo (zimeshafikia tano katika miaka hamsini iliyopita!).

Sasa CCM haina watu wenye mawazo mapya kwani hata wale wanaodhaniwa kuwa na mawazo mapya ukiwasikiliza sana utaona wanatoa mawazo yale yale tu ila “tofauti.”

Tumeona kwa mfano walivyohangaika kujivua gamba na tumeona jinsi walivyojitahidi kushinda kiti cha Arumeru Mashariki kwa njia zile zile za zamani.

Ukifuatilia utaona kuwa CCM inaendelea kujikuta inakosa hoja za kuwashawishi wapiga kura, maana wakimaliza za udini, ukabila, ukanda na kumshambulia Dk. Willibrod Slaa, Freeman Mbowe, watahubiri nini zaidi?

Lakini kinachonitisha pia kwa upande wa CHADEMA ni kuwapo watu wanaoamini CCM ina nia nzuri kabisa ya kuboresha demokrasia! Hili linanishangaza.

Hawaamini kabisa kuwa kuna uadui wa msingi ambao unatokana na tofauti za kimsingi kabisa ambazo haziwezi kupatana  isipokuwa kwa kuunganisha vyama.

Wapo wanaowaangalia viongozi wa CCM, kwa vile eti ni watawala na huwategemea kuwa watafanya mambo mazuri ya kuimarisha upinzani na demokrasia.

Hawa wanafikiria CCM itachukua mafuta, itayaweka kwenye kikaango, itaweka moto chini halafu itajiweka kwenye kikaango na kutumia mwiko kujikaanga yenyewe! 

Kwanini? Wanatumia mojawapo ya ulaghai wa maneno kuwa yote ni kwa ajili ya “maslahi ya taifa.” Wanafikiria kabisa kuwa wanapozungumzia “maslahi ya taifa” wanamaanisha maslahi ya watu wote kwenye taifa! Ukweli ni kuwa “maslahi ya taifa” ni neno la siri tu hawa wanamaanisha “maslahi ya CCM”.

Nitawapeni mfano. Kuna watu ndani ya CHADEMA kwa makosa wanaamini CCM inaweza kuendesha na kuratibu mchakato wa Katiba Mpya na mwisho wa siku ikapatikana katiba itakayofaa “Tanzania nzima!” 

Nilikataa toka mwanzo kabisa Rais Jakaya Kikwete alipoamua kutangaza mchakato huu na kuifanya kuwa ajenda ya CCM huku CHADEMA walioasisi wakiachwa wakishukuru kwa furaha kuwa “Rais amefanya jambo jema!”

Wanafikiri kuwa Rais Kikwete atasimamia mchakato ambao unaweza ukakiondoa chama chake madarakani! Wenyewe wanasema “rais ana nia njema!” Wanasahau kuwa “nia njema” ya rais inahusisha kuhakikisha kuwa CCM inaendelea kubakia madarakani kwa muda mrefu ujao.

Binafsi simlaumu rais au wana-CCM kwa kuteka hoja hii kwani hata mimi ningekuwa wao ningefanya hivyo hivyo; nitengeneze mazingira ya kukiondoa chama changu madarakani?  Watoto wangu watakula wapi?

Sasa CHADEMA kama chama cha siasa ni lazima wawe na akili za kivita (war mentality), kuwa adui yao CCM ni chama kilichobobea katika mambo ya ‘vita’ na kitafanya jambo lolote lile ili kuhakikisha upinzani haufurukuti hata ikibidi kuachilia maeneo kimkakati. 

Kwa mfano, Rais Jakaya Kikwete alipokubali kukutana na ujumbe wa CHADEMA kujadili suala la katiba, wapo walioamini kuwa ni jambo zuri “kwa maslahi ya taifa.” 

Matokeo yake CHADEMA wamerudi mikono mitupu kwani leo tumeshuhudia, Tume ya Katiba Mpya imeundwa na rais wa Muungano na rais wa Zanzibar peke yao, hivyo hii si tume ya wananchi ya mabadiliko ya katiba bali, ni tume ya rais ya mabadiliko ya katiba na inasimamiwa na wana CCM!

Na litakapoundwa Baraza la Katiba theluthi mbili ya wajumbe wake watakuwa wana CCM! CCM imeachilia hoja ya Katiba Mpya, ikakubali, japo mwanzoni walikataa kabisa na wapinzani walipoingia laini sasa inawagonga kwa kila kona. 

Nawahakikishia katiba mpya itakayopatikana haitakuwa “mpya” bali itakuwa “tofauti”! Itakuwa katiba ambayo kwa hakika kabisa itaisimika CCM milele madarakani! 

Tunajua CCM inagombea kutawala na kwanini inataka kuendelea kutawala kwani kutotawala kutaiweka mahali ambapo haijawahi kuwepo. 

Lakini swali la msingi ni kuwa CHADEMA wanagombea nini? Na kwanini wanataka kutawala? Je, ni kwa sababu wana mawazo mapya au na wao wana mawazo “tofauti?” 

Kwa mfano, nimesikia mara kwa mara viongozi wa CHADEMA nao wanapanga kuchimba visima kama suluhisho lao la tatizo la maji huko vijijini; hili ndilo suluhisho la CCM vile vile! Swali langu ni kuwa je hakuna suluhisho jipya nje ya “visima vya maji ?”

CHADEMA isipojifikiria kuwa hii ni vita na CCM ina maslahi makubwa zaidi yanayogombaniwa watajikuta wanashinda hapa na kupigwa pale, wanachezewa hapa na kubezwa pale, na wakileta ukorofi kweli kweli watanyamazishwa kweli kweli.

Yapo matumaini angalau kidogo kuwa wakati baadhi ya viongozi wake bado wakiwa na fikra za CCM inaweza kutawala vizuri wananchi mitaani wameshaanza kukikataa kutoka mioyoni mwao! 

Wameamua kuchagua upande. Mtu anayesema “mimi siyo CCM wala mimi siyo mpinzani” ni dhaifu! Chagua upande wa vita hii na pigana kutetea upande wako kwani mwisho wa siku, kuna watu lazima washindwe. 

CHADEMA wataelewa hili, hivi sasa bado wameshikana mikono wakicheza ‘zero distance’ na CCM! 

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: