CCM, Chama Cha Makamanda


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 19 January 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

UKIONDOA Makamu Mwenyekiti, Pius Msekwa, na Mweka Hazina, Amos Makalla, viongozi wote wa sasa wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walikuwa wanajeshi.

Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete (Luteni Kanali), Katibu Mkuu, Luteni Yusuf Makamba, Naibu Katibu Mkuu, Kapteni George Mkuchika, na Naibu Katibu Mkuu, Kapteni John Chiligati, wamepata kuwa maofisa katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Nimepitia vyama vingine vya ukombozi barani Afrika na kugundua kuwa kwa sasa ni CCM pekee kilichobaki na wanajeshi kama waendeshaji wakuu wa chama.

Uganda, Mwenyekiti wa chama tawala cha National Resistance Movement (NRM), Yoweri Museveni aliwahi kuwa mwanajeshi kufikia cheo cha Luteni Jenerali.

Lakini Katibu Mkuu, Amama Mbabazi, ni mwanasheria anayeheshimika na hana historia ya uanajeshi. NRM wana ‘Chiligati’ wawili: Ofwono Opondo na Mary Karooro-Okurut.

Okurut ni mwanafasihi, na Opondo alikuwa mwanahabari maarufu miaka ya nyuma; ndiyo maana hadi leo pamoja na mwenzake (Mary) wanaendeleza safu magazetini kuhusu mwelekeo wa chama na majibu ya hoja za vyama vya upinzani.

Afrika Kusini inaongozwa na Chama cha African National Congress (ANC) chini ya Rais Jacob Zuma ambaye hakupata kuwa mwanajeshi bali sehemu ya jeshi la chama hicho lililofahamika kama Umkhonto we Sizwe – jeshi la ukombozi.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa ANC, Gwede Mantashe ambaye si mwanajeshi bali mkomunisti mkubwa. Anatoka kundi la watetezi wa haki za wafanyakazi.

Kiongozi wa sasa wa chama tawala cha Msumbiji (FRELIMO), Rais Armando Guebuza, alitumikia kundi la wapiganaji wa chama hicho katika vita vya msituni dhidi ya ukoloni wa Wareno. Tuseme ana historia ya uanajeshi.

Lakini Katibu Mkuu, Filipe Paunde, na viongozi wengine wa FRELIMO, si wanajeshi. Wanatoka fani mbalimbali za maisha kama ujasiriamali, uanasheria na uchumi.

CCM ingeweza kuwa na mwanajeshi mmoja kama kiongozi (Kikwete) kwa sababu ya mvuto wake wakati akiingia madarakani ambao sina hakika hasa kama angalinao. Naona hakukuwa na ulazima wa kuwanao kina Makamba, Mkuchika na Chiligati.

Chama chochote cha siasa huongozwa na itikadi. CCM iliundwa kama chama cha kikada na kuwepo wanajeshi kama viongozi ni jambo la kawaida. Bali hatma ya chama chochote cha siasa leo, haiwezi kuachwa kwa wanajeshi.

CCM ya leo haifuati siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Hata kama katiba yake bado inaamini itikadi. Ukweli ni kwamba hakiifuati.

Hata hivyo, makada hao wanajeshi wanaoongoza CCM hawakulelewa na kufunzwa kwa ajili ya zama hizi mpya zinazoegemea sera za soko huria.

Na kwa sababu hawakufunzwa na kuandaliwa katika mahitaji ya sasa, ndiyo maana mambo mengi ya nchi yanakwenda shaghalabaghala kwa muda sasa.

Manahodha wamepewa meli kwa sababu wanajua kuongoza lakini hawajui hasa ramani ya kule wanakotakiwa kwenda!

Sisemi kwamba kama kina Makamba wakifukuzwa leo, CCM itabadilika kesho, hapana. Ninachoamini ni kuwa kama nafasi zao wangepewa makada wa taaluma nyingine zinazoendana na mahitaji ya leo, hali ingebadilika tu.

ANC walimchagua Mantashe ingawa walijua ni mkomunisti. Kilichowavutia kwake ni mfungamano wake na wafanyakazi, nguvu kubwa ya kisiasa nchini Afrika Kusini.

Kuwa na kiongozi anayejua shida za wafanyakazi ni kitu muhimu sana katika siasa za nchi hii yenye uchumi imara zaidi barani Afrika.

Labda nitoe mfano. Tunaye Nicholas Mgaya, kaimu katibu mkuu wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania (TUCTA). Angekuwa Katibu Mkuu wa CCM ya sasa, angekuwa msaada mkubwa.

CCM ingekuwa na mtaji muhimu kisiasa kupitia kwa wafanyakazi kwani shida na matumaini yao yangezingatiwa. Faida isingeishia hapo.

Mgaya huyohuyo angeshiriki katika utengenezaji wa sera za CCM zikaendana na matakwa ya wafanyakazi ambao wanachokitaka ni maslahi yao tu kutazamwa.

Kikwete asingekuwa na sababu ya kuita wale wanaoitwa “Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam” kwa ajili ya kuwashitaki wafanyakazi.

Lakini, unapokuwa na chama ambacho viongozi wake wote hawajawahi kuajiriwa (CCM) zaidi ya kwenye chama chao na serikalini kwa vipindi, unategemea nini kwa chama hicho?

Nani amewahi kusikia wanajeshi wamegoma kazi? Hivi Kikwete, Makamba, Chiligati na Mkuchika wanajua nini hasa maana ya mgomo wa wafanyakazi wakati wenyewe hawajawahi kuajiriwa?

Hata kama wanadai CCM ni chama cha wakulima na wafanyakazi, viongozi wa juu wa sasa wa CCM hawajawahi kuwa wakulima.

Kuna tofauti kubwa kati ya kumiliki mashamba na kuwa mkulima. Mwalimu Nyerere alikuwa mkulima. Aliwahi kukosa ajira na kukaa kijiweni.

Ndiyo maana ilikuwa rahisi kwake kufahamu matatizo ya wakulima na taabu anayoipata yule asiye kazi. Kuna taarifa kuwa mwalimu hakuwa akifukuza watu kazi kwa kuhofia kuvuruga maisha ya mtu.

Wanajeshi wanaoongoza CCM sasa hawana sifa hizo. Wamekaa madarakani kwa muda mrefu. Hawawezi kufikiria maisha nje ya chama tawala na serikalini. Ndiyo maana unasikia majibu ya Makamba kwenye tukio la mjini Arusha.

Ukimsikiliza Msekwa utagundua tofauti kubwa ya kimtazamo baina yao. Msekwa ni msomi, kada na mtu ambaye kuna kipindi alikaa nje ya chama na serikali na kufanya mambo yake.

Wanajeshi wanaoongoza CCM sasa hawakupata ‘nuksi’ hii ambayo imewapata Watanzania wengi na ni yule tu anayejua kinachowapata wananchi angestahili kuongoza chama cha siasa.

Niliamini hivyo siku nyingi. Nayasema leo kwa sababu muda umefika. Mauaji yaliyotokea mjini Arusha yamenigusa sana. Ninachohofia sasa ni itakuaje pale CCM itakapokuja kuamua kuendesha serikali kijeshi?

Viongozi watakataza maandamano kijeshi; wataamua kuajiri kijeshi; kuendesha mijadala kijeshi na kutatua kero za wananchi kijeshi. Itakuwa hatari kubwa kwa taifa.

Itakuwa hivyo maana walioko kileleleni mwa uongozi wa chama, wote ni wanajeshi?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: