CCM, CUF jino kwa jino


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 06 June 2012

Printer-friendly version
Rais Shein na Makamu wake Sharif Hamad

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) vimeanza kufarakana; na serikali yao ya pamoja inaweza kusambaratika wakati wowote, MwanaHALISI limeelezwa.

Kila chama kinakishutumu kingine kwa kuanzisha, kuendesha na kuchochea mazingira ya vurugu Zanzibar.

Kauli za viongozi waandamizi wa vyama hivyo, katika mahojiano na gazeti hili juzi, Jumatatu, zinathibitisha kushutumiana, kutoaminiana na hatimaye uwezekano wa kufarakana.

Kwa upande mmoja, CCM inaituhumu CUF kwa kuunga mkono Jumuia ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu, ambayo imejiapiza kuongoza juhudi za kupinga ukusanyaji maoni ya katiba mpya hadi ifanyike kura ya maoni ya kuuliza Wazanzibari iwapo bado wanataka Muungano.

Kwa upande mwingine, CUF inaituhumu CCM kwa kuendesha mikutano, ambayo viongozi wake “wamemimina vitisho na matusi” kwa viongozi wa chama hicho cha upinzani ndani ya serikali ya pamoja.

Mkurugenzi wa habari wa CUF, Salim Abdalla Bimani amesema viongozi wa CCM wilaya ya mjini, mkoa wa Mjini Magharibi, wakiongozwa na mwenyekiti wao, Borafya Mtumwa Silima, wamekuwa wakiendesha mikutano ya vitisho dhidi ya wapinzani wa Muungano.

Amesema viongozi hao wamefika mbali zaidi; wakimhusisha Makamu wa Kwanza wa Rais, ambaye pia ni katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad kuwa anaunga mkono Uamsho.

Viongozi wa CCM wanaelezwa kufanya mikutano mitano katika mkoa wa Mjini Magharibi.

Katika mikutano hiyo, Bimani anasema walitukana viongozi wa Uamsho huku wakiwatisha waliowaita ‘wapinga muungano’ kwa kuwaambia “watakatwa vichwa na janjaweed.”

Janjaweed ni jina walilojiita vijana nchini Sudan waliokuwa wakifadhiliwa na chama tawala cha nchi hiyo, ili wapambane na wanamgambo waliokuwa wakishinikiza kuundwa kwa taifa la Sudan Kusini.

Kwa Zanzibar, jina hilo walipewa vijana waliokuwa wanadaiwa kufadhiliwa na CCM ili kuendesha vitisho – kuvamia kwenye makazi, vijiwe na hata nyumbani – na kuwajeruhi “wapinzani” kwa mapanga na vipande vya nondo.

Vurugu hizi zilionekana zaidi wakati wa uchaguzi mkuu hasa mwaka 1995. Zilisitishwa kabla ya uchaguzi mkuu 2010 baada ya muwafaka kati ya CCM na CUF.

“Wewe unawajua janjaweed ni nani. Unaposikia matamshi kama haya jukwaani, unapata tafsiri gani, kama siyo kwamba wanaoyatoa wamekusudia kuleta vurugu nchini petu?” anahoji Bimani.

“Hawa siyo kwamba wamechoka au hawana akili. Hata kidogo. Tatizo lao kubwa hawapendi maridhiano. Wanataka Zanzibar irudi kusherehekea siasa za fitna na mauaji,” ameeleza.

Lakini Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai amesema CCM haihusiki na vitendo vinavyochochea vurugu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa simu juzi Jumatatu, Vuai kwanza alijibu kwa ufupi, “Hili jambo unajua lipo mahakamani. Nisingependa kutoa kauli yangu. Tusubiri vyombo husika ambavyo vinafanya uchunguzi. Ukweli utajulikana.”

Bali alipoelezwa kuwa tuhuma kwa viongozi wa CCM kufanya mikutano ya hadhara na kutishia wanaoitwa “wapinga Muungano” hazina uhusiano na shauri lililoko mahakamani, alisema “…ukweli unajulikana ila wenzetu wanajaribu kuuficha.”

Vuai amesema wao wanajua kuwa CUF wanaunga mkono shughuli za Uamsho na ndio wanaohusika na vurugu “zilizosababisha fadhaa kwa nchi na uharibifu wa mali za wananchi.”

Wiki iliyopita (26 na 27 Mei), vijana waliosadikiwa kuwa wafuasi wa Uamsho, walifanya maandamano, kuchoma matairi na kuziba barabara; kuchoma moto makanisa mawili na kuvunja majumba ya kuuza bia – baa.

Vuai amesema wana imani kuwa “Uamsho ni wing ya CUF. Si unajua sisi CCM tuna wing ya vijana? Basi wenzetu wao Uamsho ni wing yao. Wanaunga mkono shughuli zao… wanaunga mkono yanayofanywa na Uamsho. Hili linajulikana,” amesema.

Amesema watu wasihangaike kusaka wahusika; vyombo vya dola vinafuatilia kila kitu ili ukweli uwekwe wazi licha ya watu “kujitahidi kuuficha.”

“Chukua CD za mihadhara ya Uamsho; chukua CD za hiyo mikutano mitano ya CCM; halafu ziweke hadharani watu waone na kusikiliza. Waache waamue ni nani aliyechochea vurugu,” ameeleza Vuai kwa sauti ya upole.

Vuai alikana kutetea au kulinda viongozi wa chini yake wanaotuhumiwa “kutukana” viongozi wa serikali na “kutishia wapinga Muungano.”

Lakini Bimani anasema viongozi wa CCM wamenukuliwa wakisema, “…janjaweed wangalipo, tena wana kontena za nondo ambazo watatumia kukata vichwa vya wapinga Muungano.”

Akiongea kwa hamasa, Bimani anasema, “Usidhani hawa wanafanya utani; janjaweed wanajulikana kukata vichwa na kuchanja watu. Hawa ndio watu wabaya ambao tungependa serikali ikabiliane nao.”

Bimani ametaja majina ya viongozi waliopanda jukwaani katika mikutano ya CCM na kudai kuwa wametumwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar kutoa salamu kuwa wapinga Muungano watashughulikiwa (orodha ya viongozi hao tunaihifadhi kwa sasa).

Amesema yote hayo yametokea bila CCM kukemea na kuongeza kuwa hata alipomfuata ofisini, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed na kumjulisha juu ya suala hilo, hakuchukua hatua.

“Nilikwenda ofisini kwake. Nikampa taarifa za uhuni unaofanywa na wasaidizi wao katika chama. Nikaonya kuwa uhuni huu utaleta vurugu. Lakini hakuchukua hatua,” ameeleza Bimani.

Bimani amesema CUF inajua kuna viongozi waliochukizwa na maridhiano; wanatumia kila mbinu kutaka kuchafua amani na utulivu uliopo.

Kiongozi huyo wa CUF amesema chama chake kinaachia vyombo vya dola kuchunguza na kuchukua hatua ila anasisitiza, “…wafanye kazi yao kitaalamu; asionewe mtu, asipendelewe mtu wala asibambikizwe kesi mtu.”

Maalim Seif hajasema lolote kuhusu hali hii. Kiongozi mmoja wa CUF ngazi ya taifa amesema, “…ukiona huyu kaingia kwenye mabishano haya, ujue ndoa yao inavunjika.”

“Alichokwambia mwenezi wa CUF ndiyo maoni na msimamo wa chama chetu. Hapa tayari kuna ‘jino kwa jino’ ya kimyakimya. Tuombe isilipuke,” ameeleza kiongozi huyo akiomba kutotajwa gazetini.

Tayari viongozi wakuu wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (JUMIKI) wamekutana na uongozi wa juu wa jeshi la polisi Zanzibar.

Mkutano huo ulifanyika makao makuu ya polisi Zanzibar, Ziwani juzi Jumapili.

Gazeti hili limeelezwa kuwa Sheikh Farid Ahmed Hadi, Amir wa Uamsho, ndiye aliongoza viongozi wenzake kukutana na polisi kwa ushauriano.

Katika kikao hicho, Uamsho walitoa orodha ya viongozi wa CCM ngazi ya wilaya wakiwatuhumu kutoa kauli zilizochochea vurugu.

Amir Farid ameiambia MwanaHALISI kuwa amekabidhi orodha hiyo kwa kamishna wa polisi. Orodha hiyo pia ina maelezo ya mikutano ambako CCM walitolea vitisho kwa viongozi wa Uamsho kwa madai kuwa wanapinga Muungano.

Uamsho wameshaendesha mihadhara ipatayo 50 kuelezea umuhimu wa kuitisha kura ya maoni kwanza ili Wazanzibari watoe kauli iwapo wanataka Muungano.

Katika kukabiliana na wana-Uamsho, yapata wiki mbili sasa, polisi walimkamata mmoja wa viongozi wao, jambo ambalo linadaiwa kuamsha hasira za wafuasi wao.

Kwa siku mbili mfululizo, polisi walikabiliana na vijana waliokuwa wakirusha mawe wakishinikiza kiongozi wao aachiwe.

Watu 30 wamekamatwa na kufikishwa mahakamani kwa mashitaka yanayohusiana na vurugu hizo. Wote walikana kuhusika na wapo nje kwa dhamana.

Vuta nikuvute iliyopo hivi sasa kati ya Zanzibar na serikali ya Muungano, ni kuanza kutumika kwa sheria ya kukusanya maoni ya katiba kabla sheria hiyo haijaridhiwa na Baraza la Wawakilishi (BLW).

Kikatiba na kiutaratibu, sheria yoyote inayotungwa na bunge kuhusu mambo ya Muungano na ikikusudiwa kutumika Zanzibar, sharti iwasilishwe katika BLW kabla ya kuanza kutumika.

Kuibuka kwa hoja hiyo sasa, ambayo inatokana ama na kupitiwa au kudharau, kumetajwa kuwa sababu kuu ya Tume ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba kuchelewa kuanza kazi yake.

Tume ilitarajiwa kuanza kazi tarehe 1 Mei. Jaji Warioba amekuwa akiwaambia waandishi wa habari kuwa tume yake ikiwa tayari, atawaita wao kwanza na kuwaleleza utaratibu.

Taarifa ambazo hazijathibitishwa ambazo zimefikia MwanaHALISI zinasema huenda baraza la wawakilishi, ambalo linaanza kikao chake cha bajeti wiki ijayo, likashughulikia uridhiaji wa sheria hiyo.

Tangu Rais Jakaya Kikwete atangaze utaratibu wa kupatikana katiba mpya ya Muungano, kumekuwa na harakati nyingi zikiwemo asasi za kiraia kuhamasisha watu kutoa maoni wakati utakapofika.

Lakini kwa Zanzibar, asasi zinaongeza vionjo kwa kushinikiza serikali iitishe kwanza kura ya maoni ili watu waamue iwapo bado wanapenda na kuridhika na Muungano.

Wiki iliyopita, akiongea na waandishi wa habari ikulu Zanzibar, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein aliwasihi Wazanzibari kuwa watulivu na kusubiri Tume ya Katiba kuchukua maoni yao.

Naye Rais Kikwete, katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Mei amesema, Muungano hauwezi kuvunjwa kwa maandamano.

Amesema Watanzania wako huru kutoa maoni yao juu ya Muungano.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: