CCM na CUF kamilisheni kazi mloianza


editor's picture

Na editor - Imechapwa 13 May 2008

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MAZUNGUMZO ya kutafuta muwafaka kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) yanaendelea kukwama. Kukwama kwa mazungumzo hayo kumetokana na misimamo iliyowekwa na vyama hivi.

Wakati CUF wanasema mazungumzo yamemalizika, na kwamba ajenda ya kura ya maoni ililetwa kwa hila na CCM, wenzao wanasema mpaka sasa ni ajenda nne tu zilizojadiliwa.

Ajenda hii, kwa mujibu wa CCM, inahusu utaratibu wa utekelezaji na progamu ya utekelezaji wa makubaliano.

Pande zote mbili tumezisikia. Tumewasikia CCM kama tulivyowasikia CUF. Lakini ukweli uliobaki ni kwamba mazungumzo haya yamekwama kutokana na ulaghai wa CCM wa kuumba jambo jipya walilolipachika jina la "kura ya maoni".

CCM wanakiri kuwa hili halikuwamo katika vikao vyote 14 vilivyokwisha fanyika.

Kwa mujibu wa waraka wa CCM uliofikishwa Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu (NEC), jambo hili lililetwa na Kamati ya CCM katika mazungumzo, baada ya kutakiwa na Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume waliingize.

Hakika, hili ndilo chimbuko na kichocheo kikuu cha muwafaka kukwama.

Matokeo yake, ni kupanda kwa joto la kisiasa Zanzibar maana tunaanza kusikia yaliyopita yakifanana na yale yaliyotokea baada ya kumalizika chaguzi za mwaka 995 na 2000.

Ni vema CCM ikaondoa ajenda hii ya kura ya maoni kwa maslahi ya taifa, ili vyama virudi kumalizia palipobaki.

Ni imani yetu hilo linawezekana. Hii ni kwa sababu katu CCM haiwezi kujivua na lawama za kuchochea upya mgogoro ambao mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, aliuahidi ulimwengu kuupatia ufumbuzi wa kudumu.

Ikumbukwe kwamba CCM ndio chama tawala na kinacholaumiwa katika kukataa kuachia mkondo wa demokrasia kufuatwa.

Kama Watanzania wanataka ukweli ubaki kuwa ukweli, basi CCM hawana jeuri ya kutamba kuwa wamefanikiwa kusimamia uchaguzi huru na wa haki Zanzibar.

Kinachoshuhudiwa kila unapofanyika uchaguzi, tangu wa 1995, ni vurugu na ukiukaji wa misingi ya uchaguzi unaonyima wananchi fursa ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Binadamu wenye akili wakifika mahali kuamua na kusimamia hasa kukwamisha kile wanachokiamini kitaleta ufumbuzi wa mgogoro, basi hapo tumeondokana na ubinadamu. Tunaweza kwenda hivi?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: