CCM, CUF serikalini ‘tuko makini’


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 29 June 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

MIEZI saba baada ya kuundwa kwa serikali iliyoshirikisha vyama viwili vilivyokuwa hasimu kisiasa visiwani Zanzibar – Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), Zanzibar imethibitisha kuwa hakuna kisichowezekana.

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI wiki iliyopita, katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski, jijini Dar es Salaam, Omari Yusuf Mzee, waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo katika Srikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) anasema, “Mle ndani ya serikali hakuna tofauti ya vyama.”

Anasema, “Kila waziri ana jukumu la kutekeleza majukumu yake aliyopewa na rais. Si waziri kutoka CCM wala kutoka CUF, wote wanachapa kazi kutumikia wananchi.”

Mzee alikuwa akijibu swali lililohusu changamoto zilizopo ndani ya serikali inayoundwa na mawaziri wa vyama vya CUF na CCM ambao miezi 10 tu iliyopita walikuwa hawapikiki chungu kimoja.

Anasema, “Ninachokiona mimi ni kwamba kila waziri aliyepewa jukumu anataka kufanya kazi aliyopewa bila kujali mwananchi mmojammoja anapenda chama gani.”

Mzee ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ndani ya CCM anasema, “Kwetu sisi hakuna mawaziri wa chama fulani.”

Kauli hii haikutarajiwa kutolewa katika kipindi hiki kifupi cha maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa kati ya CUF na CCM, hasa ikitiliwa maanani kwamba uhasama wa vyama hivi ulikuwa mkubwa na uliotishia maisha ya wananchi.

Omari Mzee, mtaalamu wa fedha na mipango, aliyetumikia serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa miaka mitano – 2005 hadi 2010 – kabla ya kurejea Zanzibar, anasema katika kuhakikisha serikali inawatumikia wananchi wake, imepanga kutumia Sh. 613.07 bilioni kwa mwaka wa fedha 2010/2011.

Kati ya fedha hizo, Sh. 234. 17 bilioni ni kwa matumizi ya kawaida na Sh. 378.90 bilioni zimetengwa kwa ajili ya mipango ya maendeleo.

Anasema bajeti hiyo iliyowasilishwa kwenye baraza la wawakilishi wiki mbili zilizopita, imelenga katika maeneo matatu makubwa.

Kwanza, ni kuondoa umasikini kwa wananchi, hasa vijana kwa kuwapatia mitaji katika sekta ya uvuvi; miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji na upanuzi wa sekta ya elimu.

Anasema pamoja na kwamba bajeti hiyo inategemea wahisani wanaotarajiwa kutoa Sh. 340, lakini anaamini itaweza kutekelezwa bila matatizo.

 “Hakuna nchi yeyote duniani iliyopiga hatua bila kukopeshwa,” anaeleza Mzee.

Anasema mipango ya serikali ni kutumia raslimali ya ardhi, ambayo pamoja na udogo wake, inaweza kusaidia kubadilisha mtizamo wa vijana.

“Katika hili,” anasema, “serikali itatoa kipaumbele cha kuwajengea vijana uwezo wa kiuchumi kwa kuwawezesha kifedha ili washiriki harakati za  kujitegemea.

“Katika kipindi hiki cha miaka mitano ya kwanza, serikali imepanga kukigeuza kilimo kutoka kile cha jembe la mkono hadi kilimo cha kisasa cha umwagiliaji. Lengo ni kuhakikisha kilimo kinaleta tija haraka na kinawakwamua wananchi wetu kiuchumi,” ameeleza.

Anasema katika mpango huo, serikali inakusudia kuongeza kiwango cha mavuno ya mpunga kutoka tani 1.2 zinazovunwa sasa hadi tani sita kwa eka moja.

“Tunalenga kuwakopesha matrekta madogo, zana na pembejeo. Vijana watakaovutika kwenye kilimo hiki watapewa mbegu bora na watakopeshwa mbolea katika mpango kabambe ambao serikali itakuwa inafidia bei halisi ili kuwapunguzia mzigo,” anaeleza.

Anasema tayari benki ya Exim ya Korea Kusini imekubali kusaidia uwezeshaji katika kilimo cha mpunga kwa njia ya umwagiliaji.

Katika sekta ya uvuvi, Mzee anasema ni imani yake kwamba sekta hiyo ikijengwa vizuri itaweza kuleta tija hasa kwa kuwa Zanzibar ina hazina kubwa ya samaki katika Bahari ya Hindi.

Anatambua ugumu wa wavuvi wa Zanzibar kufika bahari kuu, takribani kilomita 30 kutoka ufukweni. Hata hivyo, Mzee anasema serikali italiangalia tatizo hilo kwa kutoa mikopo ya vifaa vya kisasa kwa vijana na kushawishi wafanyabiashara wakubwa na wale wa kati kuwekeza katika viwanda vya kusindika samaki.

Anasema, “Kiwanda kikijengwa kitahitaji samaki wengi na hivyo kupandisha bei ya samaki kutoka kwa wavuvi. Hii ni faida kwao lakini pia tutazalisha ajira kupitia kwenye viwanda. Haya ndiyo maendeleo tunayoyadhamiria.”

Kuhusu biashara, Mzee anasema serikali imelenga kulishughulikia kikamilifu suala hilo kwa kuwa wananchi wengi bado wanafanya biashara kwa mazoea.

Je, itawezaje? Anajibu, “Chukua eneo kama uwanjani Mwembekisonge; pale ukijenga majengo ya kisasa ya wafanyabiashara wadogo, unaweza kuwasaidia kupata mtaji kwa kuwa sasa wanaweza kukopeshwa na vyombo vya fedha, huku serikali ikijihakikishia mapato kwa kuwa sasa wataweza kulipa kodi bila usumbufu.”

Anasema kupitia mpango huo, vijana wengi wataweza kusafiri wenyewe kwenda nchi za Mashariki ya Mbali kama vile China, Taiwan na Singapore, kununua bidhaa, tofauti na sasa ambapo wanatumika kama wachuuzi na wenye maduka makubwa.

“Kule nje kuna wafanyabiashara wadogo – wale wanaoitwa Wamachinga nchini Tanzania – wana maduka makubwa katika majengo ya kisasa. Tunataka Zanzibar ielekee huko. Tunataka kujenga majengo ya kisasa, siyo kama yale ya pale Ilala,  ambayo yamejengwa kienyeji,” anaeleza Mzee.

Hata hivyo, Mzee anakiri kwamba maeneo yote hayo yanahitaji mitaji; sharti serikali ihakikisha fedha za kutekelezwa mipango hiyo zinapatikana.

“Sisi serikali tutakuwa mdhamini mkuu wa wananchi wanaotaka kukopa benki. Hili tumedhamiria hasa maana tunajua wengi watavutika badala ya kukaa na kusubiri ajira za serikalini ambazo hazipo,” anaeleza.

Kuhusu huduma za jamii, Mzee anasema serikali imepanga kutumia Sh. 123 bilioni kutatua tatizo la maji katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba. Sehemu ya fedha hizo itatoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB).

Benki hiyo, kwa mujibu wa waziri Mzee, inatoa kiasi cha dola 47 milioni, huku serikali ikipanga kutoa Sh. 3 bilioni.

Moja ya hatua kubwa zitakazochukuliwa katika kuhakikisha tatizo la ukosefu wa maji linapatiwa ufumbuzi, ni kuhuisha mfumo wa usambazaji wa maji kwa kuweka miundombinu ya kisasa na inayokidhi mahitaji.

Anasema, pamoja na maji kuhitajika kwa matumizi ya binadamu, lakini yanahitajika pia kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na viwanda.

Kwa upande wa sekta ya elimu, waziri Omari Yusuf Mzee anasema, kipaumbele kikuu ni kukamilika kwa mradi mkubwa wa ujenzi wa sekondari 21 za kisasa, kuzipatia nyenzo, zikiwamo kompyuta na maabara za kisasa kwa ajili ya masomo ya sayansi.

“Hapa tuna programu nzuri ya kupata walimu wenye uwezo na ujuzi kwa masomo ya sayansi. Baadhi yao ni Wazanzibari walioko nje ambao tumewahakikishia maslahi mazuri na mazingira bora ya kufanya kazi,” anasema.

Waziri huyo anagusia pia ufisadi serikalini. Hili anasema analifahamu na serikali inalitambua kuwa ni moja ya matatizo makubwa katika kufikia maendeleo.

Anasema, “Jukumu la kupambana na ufisadi litakuwa rahisi iwapo kila wizara itasimamia ipasavyo sheria ya matumizi ya fedha za serikali.”

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: