CCM genge la wanasiasa walaghai


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 21 September 2011

Printer-friendly version
Tafakuri
Rostam Aziz

WAHAFIDHINA wanaweza kutaharuki, kupiga kelele na hata kula nyama yako ukiwaambia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni genge. Hata hivyo, ukweli utabaki umesimama imara daima kwamba chama hiki sasa ni genge la walaghai .

Kamusi ya Kiswahili Sanifu inaelezea neno genge kuwa ni kundi la watu wafanyao kazi pamoja. Lakini CCM hawafanyi kazi pamoja tu bali kwa ulaghai. Nitafafanua.

Itakumbukwa kwamba mwaka 2007 hoja ya vita dhidi ya ufisadi ilipoibuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wabunge wa CCM, akiwamo Anne Kilango-Malecela wa Same Mashariki,  walisimama na kuendesha kampeni ya kupora hoja hiyo.

Walijitangaza kuwa ni makamanda wa kupambana dhidi ya ufisadi. Akizungumza bungeni kwa hisia kali, Kilango alisema hawezi kuwaachia wapinzani, akimtaja Zitto Kabwe (CHADEMA) kujitwalia umaarufu kwa kuendesha vita dhidi ya ufisadi.

Kilango alikuwa akijipambanua na kundi  la Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher ole Sendeka; Mbunge wa Kyela (CCM), sasa Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe;  William Shellukido (Bumbuli –CCM – wakati huo), Beatrice Shellukindo (Kilindi-CCM), James Lembeli (CCM-Kahama), Lucas Seleii (CCM- Nzega) na kiongozi wao, Samuel Sitta (CCM- Urambo Magharibi na Spika wa Bunge la Tisa). Hawa wote walijiweka hadharani kama wapambanaji dhidi ya ufisadi.

Walisimama kidete kupambana ukiwa ni mkakati wa kupiku CHADEMA ambao walionekana dhahiri kuungwa mkono na umma juu ya harakati zao za kupambana dhidi ya ufidadi. Umma, kwa bahati mbaya, ukaamini kundi hili la wanasiasa wa CCM, wakaaminika kuwa wanapambana kwa dhati ya mioyo yao. Lakini walikuja kushangazwa kundi hilo hilo lilivyogeuka na kukimbia kabisa hoja walizokuwa wanasimamia.

Ukweli huu ndio ulioneshwa kwa undani katika vita ya Richmond na jinsi Bunge lilivyoimaliza. Hata wale walioapa bungeni kwamba pangechimbika, hadi leo hapajachimbika. Hoja iliuawa na wao wamekaa kimya kana kwamba hawajawahi kusema lolote. Wapambanaji au genge la wasanii?

Aprili mwaka huu CCM ileile na wanasiasa wale wale wakaibuka na hoja mpya ya kujivua gamba. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, akapewa rungu la kuwakong’ota akina Rostam Aziz; Andrew Chenge na Edward Lowassa, kwamba ni magamba ya kung’olewa CCM.

Akapita huku na huko, kuwashughulikia wanachama wenzake. Mmoja wao akaona ya nini bwana, akaachia ngazi, nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na ubunge wa Igunga. Huyu si mwingine ila ni Rostam Azizi.

Akina Nape wakashangilia, wakafurahi kwamba vita yao inanoga. Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama naye akaonekana kukenua meno, kwamba vita ya gamba inafanikiwa. Mara likaja suala la kusaka kura Igunga.

Watu wale wale waliokuwa wanawatuhumu wenzao ni magamba, wakaenda kumwangukia gamba (Rostam) kwamba akawasaidie watetee jimbo la Igunga. Rostam akakubali, amefika Igunga amehutubia, wamemshangilia.

CCM baba! Mchana kinacheka, usiku kinaomboleza; mchana kinapuliza, usiku kinang’ata tena kwa meno yenye kutu na sumu mbaya. Usanii ule ule, miaka na miaka.

Katika picha hiyo mtu anapotazama CCM anashindwa kujua ina rangi gani. Je, ni kinyonga, au ni siasa za uchwara ambazo hata Rostam mwenyewe alipata kutamka wazi kwamba amechoshwa nazo?

Ni vigumu kujua kwa nini chama hiki kinaendesha siasa za namna hii! Lakini kitu kimoja ni wazi, chama hiki hakijapata kuamini katika maneno yake yenyewe, ndiyo maana kuna migongano ndani yake ambayo haina tija ila watu kujijengea uhalali wa kuwapo.

Jaribu kufikiria chama kikongwe kama CCM, uchaguzi unapomalizika tu viongozi wake na makada wote ni kuhusu uchaguzi unaofuata, nani atakuwa nani, na kwa mkakati gani; nani anamzuia nani ili aangamizwe mapema. CCM ya kusaka kura, CCM ya kumwaga ahadi ambazo asiliani hazitekelezwi na wala hakuna mpango wa kuzitekeleza isipokuwa kuhadaa umma kwa ajili ya kura.

Jaribu kusikiliza mgombea wa CCM katika uchaguzi mdogo wa Igunga, Dk. Peter Kafumu, kamishina wa zamani wa madini, leo ndiyo anakumbuka kuwa eti wachimbaji wadogowadogo watatengewa maeneo ya kuchimba madini!

Huyu amekuwa kamishina wa madini kwa kipindi cha kutosha, hakuwahi kuwaza kuwatengea wananchi eneo, lakini leo kwa kuwa anataka kura anatumia ahadi hiyo kama gia ya kupata kura.

Hakika baada ya uchaguzi hatatekeleza ahadi hiyo kwa sababu yeye ni sehemu ya sera na sheria mbovu za madini ambazo zimeacha taifa katika ukiwa mbaya!

Ukikutana na viongozi wa CCM na umati wa wanachama wake, ukiangalia wanavyong’aa katika sare zao nyeusi na kijani, ukisikia viapo vyao vya ahadi, hakika utaamini kwamba watasimamia kile wanachotamka katika vinywa vyao.

Masikini, muda si muda wananchi wanaachwa pale pale mwaka baada ya mwaka. Wanaimba nyimbo hizo hizo mwaka baada ya mwaka si kwa bahati mbaya ila kwa kuwa wao ni genge la wasanii, genge la walaghai, genge lisilojali la mtu ila matumbo yao na wale wa nyumbani kwao.

Inawezekana sera na mikakati ya binadamu na kwa maana hiyo inayotekelezwa na taasisi zilizoundwa na mwanadamu zisitimie kwa asilimia mia moja, lakini pale kitu kilichoahidiwa jana, tu leo kimeshasahaulika, si jambo dogo. Ni dhahiri huo ni mkakati wa makusudi wa watoa ahadi kwamba hawana nia ya kweli na dhati ya mioyo yao katika ahadi zao, kwa maana hiyo hili ni genge baya.

Habari kwamba CCM wanaweza kumweka kando Nape kwenda Igunga kupiga kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo hilo, kada wa chama aliyepewa jukumu la kushugulikia magamba; na watu wale wale walioapa majukwaani kwamba hawana utani na gamba, ni vigumu kuamini kwa vyovyote kama kweli CCM ina kitu chochote inachoweza kusimamia kwa dhati.

Binafsi naamni kwamba hata kushindwa kwa serikali kupambana na rushwa ni matokeo ya CCM kuishi na kushamiri katika rushwa; ni matokeo ya kuhalalisha rushwa kama mfumo wa maisha wa kujitafutia chochote, ndiyo maana kila aliyepata fedha chafu zamani au sasa, anakimbilia CCM ili kuzisafisha. Na CCM imekuwa sabuni, dodoki na maji ya kusafisha uchafu wote huo.

Watu wenye utajiri wa kutiliwa shaka wanauhalalisha kwa kutoa fedha zao kwa CCM; ni katika dhana hiyo hiyo pale CCM ilipowaza kutungwa kwa sheria ya kutenganisha siasa na biashara si tu kwamba muswada huo haukupata kuandikwa bali hata wizara za serikali zinazohusika nao hazitaki hata kukumbushwa.

Hawataki kwa kuwa huo ndio msingi wa maisha ya chama, kwamba hakiwezi kuacha kuishi ndani ya rushwa na kusaidia mafisadi. Huu ndio ukweli wa mambo kwamba CCM ni genge linalotukuza ulaghai.

0
No votes yet