CCM haina uzalendo, inatorosha twiga?


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 24 August 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

KIMEELEWEKA. Mtu yeyote aliyefuatilia michango ya wabunge walipojadili makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii atakuwa amegundua kuwa, walau kwa wiki iliyopita, hakukuwa na ushabiki wa kisiasa.

Wabunge wa chama tawala (CCM) na upinzani walizika tofauti zao.

Mwanzoni mwa Bunge la 10, hususan mkutano wa Bajeti, ilikuwa mbaya. Kila kambi, CCM na upinzani, ilijipanga kutofautiana, kujeruhi, kuaibisha, kuomba mwongozo na kutoa taarifa ili kujihami.

Wabunge walihamanika, walibabaika, walijaa hofu, hawakuruhusu hoja ya upinzani kuumiza kambi yao na upinzani ulipingwa hata ulipokuwa na hoja.

CCM walipokumbuka wajibu wao na kuamini upinzani katika mambo ya msingi; upinzani wakiibua hoja, CCM wanashindilia; upinzani wakikandamiza chini, wa CCM wanachinja.

Ndivyo kambi mbili hizo hasimu zilivyozoeana na kushirikiana kuchimba na kuchimbua mizizi ya magamba mengine yaliyojichimbia ikulu na mamlaka ya juu CCM.

Wabunge waliokataa unafiki na kuasi msimamo wa CCM wa kulinda uovu, wakawaanika peupe Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa.

Luhanjo ambaye ofisi yake ni ikulu, anahusishwa na kutengeneza mtandao wa viongozi wa kabila moja la Wabena katika Idara ya Wanyamapori huku Msekwa ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) anatajwa kujigeuza mwenyekiti mtendaji.

Viongozi hao wakubwa wanadaiwa na wabunge kuwa kiini cha uzembe na kiburi wanachojengewa wawekezaji kutaka kujenga hoteli maeneo yaliyokatazwa katika hifadhi.

Imedaiwa Msekwa amejihusisha kutoa vibali vya ujenzi wa hoteli za kitalii tena katika mkondo wanaopita faru.

Kutajwa kwa Msekwa na Luhanjo ni dosari kubwa kwa chama na ikulu na kielelezo kwamba kuongezeka kwa magamba ndani ya CCM.

Na hii ndiyo sababu ya viongozi wa serikali na chama kuwa wazito wa kueleza utoroshwaji wa wanyama hai 116 wenye thamani ya Sh. 163.7 milioni na ndege hai 16 wenye thamani ya Sh 6.8 milioni na kupelekwa Qatar.

Walikamatwa Ngorongoro, wakapakiwa kwenye malori, wakasafirishwa, njiani magari yalipimwa uzito, yakafika Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (umbali wa km 300), wakashushwa, wakaingizwa kwenye ndege na kutoroshwa.

Nani alikagua vibali vya kusafirisha? Walipitaje vituo vya polisi na vizuizi vya maliasili? Intelejensia ya Polisi ilikuwa wapi? Jeshi la Ulinzi lilikuwa wapi lisishughulikie ipasavyo ndege ya jeshi la Qatar ilipotua nchini hadi inaondoka na wanyama wetu? Ndio nguvu ya ufisadi, mpaka mfumo wa ulinzi na usalama huingiliwa!

Ili kupoza hasira za wabunge, serikali imetaja mbuzi wa kafara katika sakata hili; Mkurugenzi mkuu wa Idara ya wanyamapori, Obeid Mbangwa na wenzake wawili. Haitoshi.

Wizi huu ulifanyika Novemba mwaka jana. Kwa nini serikali ilikaa kimya hadi gazeti lilipofichua Julai iliyopita? Kwa nini serikali iliandika barua CITES Agosti mwaka huu tena siku chache kabla ya Waziri Ezekiel Maige kusoma bajeti?

Serikali iliogopa nini kutangaza ‘nyara za taifa zimeibwa?’ Kama wabunge wa CCM hawana imani na bodi ya Msekwa katika usimamizi wa hifadhi ya Ngorongoro, hawawezi pia kumpa kwenye chama.

Je, Msekwa bado atakuwa na sauti yenye mamlaka ya kusuta Mapacha Watatu waliosimangwa hadi mmoja, Rostam Aziz, kuamua kujiuzulu uongozi?

0658 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet