CCM haiwezi bila rushwa


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 28 July 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala
KATIBU Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba anasema hakuna tatizo la kushtua wakati huu wanachama wakishiriki kura za maoni za kutafuta wagombea. Anasema mambo ni shwari.

Kauli yake niliyoisikia mapema Jumapili ya Julai 25, 2010, wakati vyombo vya habari vikipitia vichwa vya habari vya magazeti, ilinishangaza.

Muda mfupi baadaye nikiwa katika ‘kijiwe’ cha kahawa kando ya kituo cha daladala cha Kinondoni, kwenda katikati ya jiji, nilipigiwa simu na mtu nisiyemjua.

Mpiga simu alijitambulisha kuwa anatoka Igunga mkoani Tabora (jina linahifadhiwa). Alianza kwa kuniomba nichapishe malalamiko atakayonipa. Alipiga simu katika namba yangu ambayo imechapishwa kwenye ukurasa huu hapo chini kushoto.

Alisema alikuwa anataka kunieleza mambo yanayotokea jimboni kwao wakati huu wakiwa wanatafuta wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani kupitia CCM.

Wakati anapiga simu, alisema jimboni kwao kuna watu wanawagawia wanachama wa CCM fedha ili wawapigie kura za kuteua mtu wanayemtaka awe mgombea ubunge wa chama hicho.

Akasema “rushwa” ilikuwa inagawiwa wakati waombaji uteuzi wakihutubia mikutano ya kampeni itakayokoma Agosti mosi – Jumapili ijayo – kwenye kura za maoni.

Kilichomsikitisha zaidi ni namna rushwa hiyo inavyotolewa bila hofu wakati maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) wanaona.

Bwana mhariri, “Nifikishie malalamiko yangu kwa wanaohusika kupitia gazeti hili tunalolipenda sana. Unajua haya mambo yanachefua na mimi sitaki kushiriki ndiyo maana mimi fedha nimezikataa”, alisema.

Hakunitajia aliyempa rushwa kwa kusema anahofia kumtia kwenye mtihani “mtu mdogo wakati mwenye fedha hana hofu.”

Tulipomaliza maongezi, watu walikuwa na shauku ya kujua nilikuwa nazungumza na nani kwani walisikia nilivyokuwa najibizana naye. Niliwaambia.

Nilipopitia magazeti nikiwa ofisini, nikakuta taarifa zilizomnukuu Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, John Tendwa akisema amepokea malalamiko 170 ya tuhuma za rushwa kwa wana-CCM wanaotafuta kugombea.

Tendwa, mwanasheria kitaaluma, anaonyesha msimamo imara kwamba haogopi yeyote na atachukua hatua zinazofaa dhidi ya wanaolalamikiwa.

Nilichota haya: “CCM ikivunja utaratibu mimi naigonga tu na hata viongozi wake nao wakivunja taratibu nawagonga. Hakuna ninayemuogopa maana nafuata sheria tu”.

Nilimtumia mwana Igunga namba ya simu ya Tendwa ili apitishie malalamiko yake maana kweli akitumia hasa sheria, wengi katika CCM watanaswa.

Baadaye alinijulisha alimpata Tendwa na hakika alimweleza. Aliulizwa iwapo TAKUKURU wapo Igunga naye alijibu wapo. Alisema Msajili aliahidi waendelee kuwasiliana.

Malalamiko haya yalinigusa kwani taarifa za rushwa kugubika zoezi la uchukuaji wa fomu na kampeni za wawania uteuzi CCM zimetawala vyombo vya habari. Baadhi zimezitolewa na wakuu wa TAKUKURU wa kanda.

Bali rushwa imetajwa hata kabla wana-CCM hawajaanza kuchukua fomu. Taarifa zimetoka majimbo mengi nchini. Tumekuwa tukiandika, “Rushwa, Rushwa, Rushwa mtindo mmoja CCM.” Chama kinakua kwa rushwa. Aibu kwa CCM, janga kwa taifa.

Kumbe CCM hawajamtii mwenyekiti wao, Jakaya Kikwete, ambaye mwaka 2007, wakati anafungua mkutano mkuu wa CCM Dodoma, alisema, “kuna tabia siku hizi wana-CCM kununua uongozi.”

Wakati huo wakiwa ukumbini, alisema, “kule nje watu wanagawa fedha eti wanashawishi wajumbe tuliomo humu tuchague wagombea wao.”

Rais Kikwete alirudia tena alipofunga mkutano mkuu wa CCM Dodoma hivi karibuni kuwasihi wananchi wasiwachague watoa rushwa.

Nilitarajia msaidizi wake mkuu katika chama atakuwa mbele kukemea ili kukomesha rushwa. Inaonekana hafanyi hivyo. Anapuuza vilio vya rushwa. Kibaya zaidi, Makamba ni kama vile anaipamba rushwa. Tuamini bila rushwa CCM haiwezi?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: