CCM hatarini kushitakiwa


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 19 January 2011

Printer-friendly version

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeingia katika mgogoro mpya na mwekezaji na huenda kikafikishwa mahakamani na hata kufilisiwa, imefahamika.

MwanaHALISI limegundua kuwa mgogoro wa sasa unatokana na hatua ya Baraza la Wadhamini la chama hicho, chini ya uenyekiti wa Peter Kisumo, kuingiza chama katika mkataba bila kushirikisha Kamati Kuu (CC) ya chama.

Mkataba ambao Kisumo na wenzake wameingia unahusu uendelezaji wa kiwanja Na. 1010 kilichopo eneo la Bonde la Msimbazi, manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam. 

Taarifa kutoka ikulu na ndani ya chama hicho zinasema, tayari mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete ameshutukia mradi huo na ameagiza kusitishwa mara moja.

Mkataba huo unaoweza kuingiza chama katika mgogoro wa kisheria, ni kati ya kampuni ya chama hicho inayoitwa Jitegemee Trading Co. Ltd., kwa upande mmoja; na makampuni matatu ya Camel Oil (T) Ltd., African Group of Industries na Simba Logistics, kwa upande mwingine.

Mbali na Kisumo, wengine wanaodaiwa kuingiza chama katika mgogoro, ni katibu mkuu wa chama hicho, Yusuph Makamba na aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Jitegemee, Andy Chande.

Kwa mujibu wa taarifa, Makamba ambaye ni katibu wa Baraza la Wadhamini la CCM, pamoja na kwamba sekretarieti ya chama chake iliukataa mradi huo, lakini yeye alitumia mamlaka yake kulazimisha kusainiwa.

“Kama chama kitaingia katika mgogoro kutokana na kusainiwa kwa mkataba huu, basi mtu wa kwanza wa kulaumiwa atakuwa Makamba. Huyu mzee aliingiza mradi huu bila kushirikisha CC. Alijua kuwa ukifika huko, hautapita,” anaeleza mjumbe mmoja wa CC ambaye hakupenda kutajwa gazetini.

Mtoa taarifa anaeleza, “Hata ndani ya Sekretarieti, naambiwa mradi wa Makamba ulikwama. Lakini yeye akaamua usainiwe kwa nguvu. Ndiyo maana nasema iwapo chama kitaingia katika mgogoro, basi mtu wa kwanza kulaumiwa, ni yeye.”

Habari zinasema mara baada ya Makamba kugundua kuwa Kikwete ameshtukia mradi huo, ameamua kupanga mkakati wa kuuvunja, jambo ambalo linaweza kuzalisha matatizo makubwa zaidi.

Gazeti hili limeweza kuona barua iliyoandikwa na Makamba, tarehe 13 Januari 2011 ambayo imekwenda kwa rais Kikwete ikieleza, hatua kwa hatua, jinsi mkataba ulivyofungwa na njia itakayotumika.

“…Ni kweli kwamba baraza la wadhamini katika kikao chake cha 19 Februari 2007 kiliridhia mipango ya bodi ya Jitegemee chini ya mwenyekiti wake Ndugu Chande ya kuendeleza bonde la Msimbazi.

“Katika kikao hicho baraza la wadahamini liliridhia maamuzi ya Bodi ya Jitegemee ya kuingia ubia na makampuni matatu ya Camel Oil (T) Ltd., African Group of Industries na Simba Logistics,” anaeleza Makamba.

Anasema, “Katika makubaliano hayo ni kwamba kila kampuni ingewekeza kiasi cha dola za kimarekani kisichopungua dola milioni thelathini na kila mwaka kampuni ingeweza kutoa kwa Jitegemee si chini ya dola milioni tatu. Bodi ya Jitegemee ilishawasilisha makubaliano hayo kwa Baraza la Wadhamini.” 

Makamba anasema, “Baada ya hapo mwenyekiti wa bodi ya wadhamini wa chama, Mhe. Peter Kisumo alimwandikia barua mwenyekiti wa bodi ya Jitegemee kuhusu uamuzi huo kwa utekelezaji… Mikataba ya makampuni hayo tayari imekamilika na imewekwa sahihi Julai 2010.”

Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja miaka miwili baada ya Kamati Kuu kumuondoa katika nafasi ya katibu mkuu wa Umoja wa Wanawake (UWT), Halima Hatibu kwa kile kilichoitwa, “Kuingiza chama katika mkataba bila kushirikisha chama chake.”

Gazeti hili liliripoti kuwa Baraza la Wadhamini la UV-CCM chini ya Lowassa lilisaini mkataba wenye thamani ya zaidi ya Sh. 30 bilioni, kati yake na makampuni mawili ya uwekezaji, bila wenye chama kujulishwa na kuridhia.

Baada ya taarifa hizo kuibuliwa, CC iliunda tume kuchunguza mkataba huo, huku Makamba na Lowassa wakisisitiza kuwa hakuna mkataba wowote uliosainiwa. Hata hivyo, CC ilijiridhisha kuwa kilichosainiwa na Lowassa ulikuwa mkataba kamili.

Kama ilivyo kwa mkataba wa Jitegemee, mkataba wa UV-CCM ulifungwa bila kushirikisha Kamati ya Utekelezaji ya UV-CCM, Baraza Kuu na chama chenyewe.

Lakini Makamba katika barua yake kwa Kikwete anasema, “Baada ya maelekezo yako kwamba mradi huu hautakuwa na tija kwa chama, nimeongea na mwanasheria Ndugu Mapande, Mzee Peter Kisumo na mwenyekiti wa Jitegemee, Peter Machunde na tumeafikiana kwamba tuchukue hatua za kubadilisha sura ya mradi huu.”

Hili, Makamba anasema, litatekelezwa kwa utaratibu ufuatao. Kwanza, kusitisha mikataba yote mitatu ifikapo tarehe 31 Januari 2011, siku ya mwisho waliyopewa wawekezaji kukamilisha masharti kadhaa kabla utekelezaji wa mradi kuanza.

Anasema, “Jambo hili litawezekana kwa vile hata wabia wenyewe wameonyesha kusuasua na wanaelekea kushindwa kutekeleza baadhi ya masharti hayo.”

Akiandika kuridhia mkataba huo, Kisumo anasema, “Baraza limeridhia maamuzi ya bodi ya kuingia katika ubia kati ya Jitegemee na makampuni ya Camel Oil (T) Ltd., African Group of Industries na Simba Logistics ambapo kila kampuni itawekeza kiasi kisichopungua dola za Kimarekani milioni thelathini.”

Barua ya Kisumo kuridhia mkataba iliandikwa 2 Machi 2010 na ilitumwa kwa Chande siku mbili baadaye. Anasema, “Makisio yanaonyesha kuwapo kwa mapato ya dola za Marekani 9.4 kwa mwaka.”

Iwapo matumaini ya Makamba yatagonga ukuta, pale anaposema huenda wawekezaji watashindwa kutekeleza masharti waliyopewa, basi wawekezaji waweza kufikisha CCM mahakamani kwa madai ya kuvunja mikataba iliyosainiwa Julai mwaka jana.

“Sikiliza. Ukiishasaini mkataba, unaanza kuzunguka kutafuta mitaji na hata wabia wengine. Makampuni haya yatakuwa yamekwishaingia katika makubaliano mengi na hata kupata mikopo kutoka mabenki,” anaeleza kiongozi mmoja wa CCM makao madogo, Dar es Salaam.

Anasema inawezekana baadhi tayari yameanzisha miradi midogo ya kusaidia kuendesha mradi huo mkubwa. Hivyo kuwakatisha kutakuwa na athari kubwa na hata kusababisha kushitaki chama, ameeleza.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: