CCM iache kunyang'anya


editor's picture

Na editor - Imechapwa 20 January 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

UKISOMA "Taarifa Maalum" ya Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu (TAMISEMI), Celina Kombani kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika 25 Oktoba mwaka jana, utaamini uchaguzi haukuwa na tatizo hata moja.

Ni taarifa yenye maneno matamu matupu. Hakueleza matatizo yaliyotokea wala hakutaja kuwepo kesi kadhaa mahakamani za kupinga matokeo ya uchaguzi huo, kufuatia vitendo vya uvurugaji taratibu zake.

Mwishoni mwa taarifa yake ya 16 Januari, ametaka tu wananchi na wale aliowaita “wadau wote” kutoa maoni na ushauri kuhusu maeneo ya kuboresha uchaguzi ujao.

Kwenye safu hii, Toleo Na. 160 la Oktoba 28-03 Novemba 2009, tulieleza mazonge yaliyotokea siku ya uchaguzi na tukalaumu serikali kwa kushindwa kuwajibika.

Katika baadhi ya maeneo ya nchi, matokeo yalisubiriwa kwa muda mrefu isivyo kawaida, tena bila ya kutolewa sababu yoyote.

Ufuatiliaji ulionyesha matatizo mengi yalikuwa katika maeneo ambayo chama tawala, CCM, kilijua kilishapoteza kutokana na ushindani uliopo.

Ndipo tulipohoji, “Hivi kweli itafika siku Watanzania tujivune mbele za watu kuwa tumefanikiwa kujisimamia?”

Tahariri yetu ile ilibebwa na maneno “Hatujafanikiwa kujisimamia.”

Hivi tunavyojadili, hadi sasa yapo maeneo ambayo wananchi hawajatangaziwa matokeo ya uchaguzi kulingana na taratibu zilizopo ingawa viongozi “waliowekwa” na dola, wanafanya kazi.

Isitoshe, tunajua zipo kesi kwenye mahakama mbalimbali nchini za kupinga matokeo; mkoani Dar es Salaam pekee zikiwapo zaidi ya kumi.

Siyo tu kwamba taarifa hizo na nyinginezo hazistahili kufichwa wananchi, ukweli hizo ni taarifa muhimu kwao kujulishwa.

Serikali haijatendea wananchi haki. Imewapora haki yao ya kupashwa habari. Haiwezekani maana ni haramu.

Tuna hakika serikali inajua matatizo mengi yaliyotokea wakati wa uchaguzi. Watendaji wake waliyaona na wanayajua.

Kulikuwa na matukio ya kijambazi yaliyothibitisha hasa kwamba dola, ikishirikiana na vyombo vyake, iliandaa mazingira ya makusudi kulazimisha CCM kushinda kwa kishindo.

Na kweli kishindo maana katika baadhi ya maeneo idadi ya kura zilizotangazwa imepita ile ya watu waliojiandikisha kupiga kura.

Hata siku moja hatuwezi kujenga demokrasia ya kweli iwapo chama tawala kinanyang’anya haki za wananchi.

Ni jambo linalosikitisha. Huko ni kufumba mambo.

Hatua ya Waziri Kombani kuficha wananchi ukweli wa yaliyotokea, ni unyimaji wa haki yao ya kikatiba.

Kuwapora wananchi haki yao ni uhalifu. Ni jinai.

Katiba inaeleza wazi kuwa ni haki ya wananchi kujulishwa kila serikali yao inalotenda.

Watu wenye fikra pana wanaamini serikali imelenga kufunika kombe ili mwanaharamu apite. Imetenda kosa kubwa kwani siku za uwazi na ukweli tulizopo, kombe linapaswa kufunuliwa ili “mwanaharamu asimame.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: