CCM ikivuliwa gamba itavuja sana


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 30 March 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi
Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kinakabiliwa na wakati mgumu kutekeleza mpango wake wa “kujivua gamba.” Kama wanavyosema wengine, uvuaji gamba waweza kuchubua hata kipande cha ngozi nyembamba kilichosalia.

Hatua ya viongozi wakuu wa chama kushindwa kujitathmini mapema, kumesababisha gamba wanalotaka kujivua kutengeneza urafiki na ngozi, na hivyo uwezekano wa zoezi hilo kufanikiwa, wengi wanaona, ni kama haupo.

Badala yake kila hatua itakayochukuliwa na viongozi wa chama kurejesha imani ya wananchi kwa chama chao, yaweza kubomoa serikali na pengine chama chenyewe.

Kwa mfano, chama ambacho kila kukicha kinaonekana kukumbatia wenye fedha, ili kiaminike kujali wananchi wengine wa kawaida, sharti kitende tofauti na kinavyoonekana sasa.

Iwe nyumba hazitabomolewa kupisha ujenzi wa barabara mpya au zitabomolewa na kufidiwa kwa fedha za kutosha, uamuzi wowote utakaochukuliwa utaiweka serikali njiapanda.

Pale ambapo nyumba za wananchi zinatakiwa kubomolewa ili kupisha ujenzi wa barabara, ni sharti zoezi la ubomoaji lisitishwe ili kuondoa manung’uniko ya wananchi dhidi ya serikali yao.

Lakini pale serikali itaposhindwa uvumilivu na kuamua kutimiza wajibu wake, chama kitazidi kubomoka na mpango mzima wa kujivua gamba utakuwa umeishia njiani.

Mfano mzuri ni wa hatua ya Rais Jakaya Kikwete mwenyewe kuunga mkono uamuzi wa waziri wake mkuu Mizengo Pinda kumzuia waziri wa Ujenzi, John Magufuli kuendelea na mpango wake wa “bomoabomoa” nchi nzima ili kuruhusu ujenzi wa barabara mpya na kupanua baadhi ya zile za zamani.

Magufuli alikuwa anatakeleza ahadi za Kikwete za kujenga maelfu ya kilomita za barabara kabla ya kuondoka madarakani, Oktoba 2015.

Ni Kikwete na chama chake walioahidi wananchi wa Kilimanjaro kuwajengea barabara ya kiwango cha lami kutoka Same mpaka Kisiwani – Kihurio na kuiunganisha na barabara kuu ya Moshi - Dar es Salaam.

Ili barabara hii iweze kujengwa, sharti nyumba zilizopo katika hifadhi ya barabara, kwa mujibu wa sheria ya sasa ya barabara zibomolewe. Ili barabara hii iweze kujengwa, sharti wanaohusika walipwe fidia na waondoke katika maeneo hayo.

Wakati waziri Magufuli akitoa muda usiozidi miezi sita baada ya notisi ya kutakiwa kuhama kutolewa, bila kujali mhusika analipwa fidia au halipwi, Kikwete anataka wananchi wapewe miaka hadi mitatu ya kujiandaa kuondoka katika maeneo yao. Anataka pia serikali ilipe fidia kwa wale wanaostahili.

Uamuzi huo una maana kuwa ujenzi wa barabara karibu zote hautaanza au ukianza hazitakamilika kwa muda unaotakiwa, kwa kuwa serikali haina fedha za kujenga barabara na papohapo kulipa fidia. Lakini pili, muda utakaosalia kabla ya Kikwete kuondoka madarakani utakuwa mdogo sana.

Kwa mfano, Kikwete hataweza kujenga barabara ya Igunga hadi Tabora kwa kuwa anataka wananchi waliopo katika hifadhi ya barabara kuachwa kwa miaka mitatu.

Hataweza kufanikiwa kutekeleza ahadi yake ya kuzipandisha hadhi hospitali maalumu saba nchini kuwa za rufaa ili kuipunguzia mzigo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN).

Kabla ahadi ya Kikwete ya kuzipandisha hadhi hospitali hizo, zinahitaji kupanuliwa. Baadhi ya wakazi wake wanaoishi karibu na hospitali lazima waondolewe ili kupisha upanuzi. Lakini siku hazitakuwa zimesimama kumsubiri Kikwete kutimiza ahadi zake. Uchaguzi utakuja na hapo ndipo chama chake kitakapoulizwa na wananchi kwa nini kilisema, lakini kilishindwa kutenda.

Wananchi wa Bukoba Mjini na wale wa Misenyi, waliohidiwa kujengewa uwanja mpya wa kisasa wa ndege na kupanua ule uliyopo, nao watakuwa wameachwa solemba. Hakika ni mtihani mkubwa.

Wapo wanaotaka barabara nzuri na wako tayari kupokea fidia, lakini wapo ambao hata neno fidia hawataki kulisikia. Wanachotaka ni nyumba zao zibaki kama zilivyo hata kama zimejengwa katika hifadhi ya barabara. Lakini pia wanataka serikali itimize wajibu wake wa kujenga barabara, zahanati, kupeleka umeme vijijini, hospitali na shule za sekondari na vyuo.

Kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo, wizara ya ujenzi iliyopewa kazi ya kujenga barabara, haipaswi kupewa fedha za ujenzi wa barabara kwa kuwa hakuna barabara itakayojengwa kwa sasa. Rais ameagiza, hakuna ubomoaji wa nyumba utakaoruhusiwa nje ya kipindi cha miaka mitatu na bila kulipa fidia. Analenga kutaka kujivua gamba.

Ndani ya miaka mitatu, Bunge lisiidhinishe hata shilingi kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya ndege ambavyo ujenzi wake unahitaji watu kuondolewa. Wananchi wanahitaji miaka mitatu na rais ameeleza kwa niaba yao. Lengo: Anataka wananchi waseme serikali na chama chao ni sikivu.

Lakini mwisho wa yote itakuwa kilio na kusaga meno kwa Kikwete na chama chake, walioona kuwa hatua ya Magufuli kusimamia ujenzi wa barabara inaichonganisha serikali yake na wananchi.

Kutokana na mtizamo mpya wa Rais Kikwete, itakuwa vigumu kwa serikali kufanya kazi yake ya kidola, huku chama kikiwa katika mradi wa kujivua gamba. Ili mradi wa kujivua gamba uweze kufanikiwa, sharti vitu hivi viwili vitenganishwe.

Lakini ikiwa Rais Kikwete atashikilia msimamo wake wa “tahadhari” ya kuvua gamba, anaweza kukosa yote. Anaweza kujikuta gamba linaendelea kung’ang’ania ngozi huku serikali ikishindwa kutimiza wajibu wake. Upo msemo, “Huwezi kula keki na papohapo ukabaki nayo.”

Hilo likifanyika, chuki ya wananchi dhidi ya serikali yao itazidi kuongezeka; matumaini ya wananchi kwa chama chao yatazidi kupungua; na matumani ya wananchi kwa rais wao yatatoweka. Wengi wataweza kumuona rais wao kuwa ni bingwa wa kunena kuliko kutenda.

Walewale waliomtumia rais ujumbe wa simu ya mkononi kulalamikia serikali kuvunja nyumba zao ili kupisha ujenzi wa barabara, ni haohao watakaomlaumu, yeye na chama chake, kwa kushindwa kutimiza ahadi zake.

Hatari kubwa ya kuondoa gamba ambalo limeoteana na ngozi ni kwamba mwili wa chama utavuja sana. Nani asiyejua athari za kupoteza damu nyingi au yote?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: