CCM imeacha chuki Igunga


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 05 October 2011

Printer-friendly version

UKIRUSHA juu sarafu mbele ya watoto na ukataka waruke kuidaka huku yule atakayefanikiwa kuipata ataimiliki, basi tarajia mtifuano wa nguvu.

Hata watoto wenyewe hutumia mtindo huohuo pale mmoja wao anapotaka kuwagawia alichonacho. Basi utasikia: “Senti kalawe, amina; mwenye kupata, apate; mwenye kukosa akose.”

Anayeimbisha wimbo huo, hurusha juu anachotaka kugawa. Labda kipande cha nyama, muwa, tunda au kitu chochote cha kuchezea.

Hapo, wenye nguvu au wepesi au wenye akili huingia. Akirusha kitu chochote anachotaka kugawa, yeye huwa si miongoni mwa wawaniaji. Hubaki akitazama wenzake wanavyosukumana kama wanyama, wakiraruana kama mbwa, wakidonoana kama kuku, wakikanyagana na hata kupigana.

Ugomvi wa watoto hao huweza kuwaingiza hata wazazi; wakatifuana hasa. Wazazi wakiingilia na wakachapana makonde hujengeana uadui wa kudumu (soma kitabu cha Une Vie de Boy au The Houseboy).

Hicho ndicho kilichofanyika Igunga, jimbo la uchaguzi lililokuwa wazi baada ya mbunge wake, Rostam Aziz, kujiuzulu Julai mwaka huu akituhumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichomteua kugombea kwa siasa chafu.

Taratibu zilipokamilika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza kiti hicho wazi na ikapanga uchaguzi mdogo kufanyika tarehe 2 Oktoba (Jumapili iliyopita). Hiyo ndiyo siku ya Tume kurusha juu kiti cha ubunge Igunga na kuachia vyama vya siasa vishindanie.

Hapo ndipo mtifuano ukaanza. Watoto (wagombea ubunge) wakatamba, wakatunishiana misuli, wazazi wao (viongozi wa vyama vya siasa) wakakodi helikopta ya kuruka juu kuomba kura. Wakatangaza sera.

Baada ya mambo kuwa mazito, wazazi wao  wakajitosa kusaidia na kuwabomoa kwa makonde na kutishia kwa bastola wapinzani wao.

Vyama vikapeleka makada mashuhuri na mabaunsa. Wakagawa mkong’oto, kanga, kofia, mashati, ahadi na mbinu zote chafu hata za kubomoa magari yao ili ionekane kuwa ni wapinzani wao.

Ikawa kutumia nguvu, hila, fujo, na mtaji mkubwa wa fedha; tindikali inadaiwa ilimwagwa na nyumba zikatiwa moto.

Walichosahau wote – wagombea na wazazi – ni kwamba wamepanda na kuacha uhasama na chuki ya kudumu kwa wana Igunga. Waliopandikiza chuki wakiwemo viongozi wa chama tawala, CCM wameruka na ndege kurudi kwao.

Igunga wameacha wakisherehekea ushindi katikati ya chuki iliyoenezwa. Wenye dini wakatumika kukilaani na kusihi wafuasi wao wakinyime kura Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa madai ya kumvua hijabu Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario. Haraka polisi wakatumika kushika viongozi wa CHADEMA na kuwafungulia kesi.

Polisi hawakufungua kesi dhidi ya aliyemrushia mwenzake tindikali usoni, na haikufuatilia wale waliotinga na silaha kwenye mikutano kinyume cha sheria.

Vilevile Polisi hawakufuatilia na kuwatia ndani wabunge waliorusha risasi usiku wa manane. Polisi wanaona makosa ya upinzani tu.

Baadhi ya makala ziliandikwa na vipindi vingi viliandaliwa kushawishi wananchi wachukue msimamo wa kihafidhina yaani wapigie kura mgombea wa CCM na nyingine kushawishi mabadiliko.

Wananchi wa Igunga wamepigia kura ukale, ujima, siasa uchwara. Tuheshimu uamuzi wao.

Matokeo hayo ni somo kwa viongozi wa vyama vilivyoshindwa. Wakajiulize kwanini vyama vyao vinakataliwa maeneo ya mashambani? Wanayo matawi ya wanachama huko? Au wamejichimbia mijini tu.

Washabiki wao walijiandikisha ili siku ikifika watumie haki yao ya kikatiba kupiga kura au ni kukalia kusubiri tu kuandamana barabarani? Wakajipange upya. Lakini CCM ijiulize bila nguvu kubwa iliyotumika ingeshinda? Imeacha amani au chuki?

0
No votes yet