CCM imeasisi, inafurahia matatizo North Mara


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 25 May 2011

Printer-friendly version

SERIKALI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inapiga kelele ikisaka mchawi katika mgogoro usioisha wa wananchi na kampuni ya African Barrick Gold (ABG) ya Canada inayochimba madini ya dhahabu North Mara, lakini haijitazami.

Viongozi wa serikali za vijiji kata za Nyangoto, Kemambo, Kibasuka, Kerende (wote CCM) ndio mwaka 1996 walioingia makubaliano ya kifisadi na Kampuni ya Afrika Mashariki Gold Mine (AMGM) bila ridhaa ya wananchi.

CCM ndio waliuza kinyemela maeneo ya watu na sasa hawataki kusimamia walioporwa maeneo walipwe fidia na kuondoka.

AMGM hawakulipa fidia na hawakuandaa mpango wa kuhakikisha wananchi wa Nyamongo wanafaidi utajiri unaotoka penye asili yao. Ilipoona imezidiwa na mzigo wa malipo ya fidia kwa mamia ya watu, mwaka 2002 iliwaachia mgogoro Placer Dome ambayo nayo mwaka 2006 ikaacha zigo la fidia na uhasama kwa Barrick.

Wananchi wanapokimbilia serikalini hawapati msaada. Viongozi wakiingia mgodini hutoka ‘fosi’ wamefunga vioo vya mbao wasiwaone wananchi.

Halafu serikali ya CCM ikawapa Barrick ulinzi wa askari wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) wanaoua, kujeruhi na kukandamiza haki za wakazi wa North Mara.

Nimebahatika kufanya ziara mara mbili mgodi ulioko Nyamongo, Tarime mkoani Mara. Kwanza ni wakati wa ziara ya kamati mbili za Bunge zilizokwenda kusikiliza malalamiko ya watu kwamba wao na mifugo waliathiriwa na maji ya sumu ya PAF iliyokuwa inatiririshwa na Barrick kwenye Mto Tigithe kutoka mgodi wa Gokona mwaka 2009.

Msafara huo ulioongozwa na Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai (sasa Naibu Spika) ulikuwa wa kamati za  Ardhi, Maliasili na Mazingira; na Nishati na Madini. Walikuwepo mawaziri saba wakiwemo William Ngeleja Nishati na Madini, Dk. Batilda Burian (Mazingira) na Dk. Aisha Kagoda (Naibu waziri Afya) na wabunge kadhaa.

Mara ya pili ilikuwa mwaka jana nilipokwenda kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya wananchi juu ya utatuzi wa kudumu wa mgogoro wao na Barrick.

Kamati ya Ndugai ilifanya mikutano ya hadhara katika kata za Kemambo, Kibasuka na Nyangoto. Wananchi walitoa mapendekezo kupitia risala.

Walitaka Barrick idhibiti maji yanayotiririka kwenye Mto Tigithe; ifunge mgodi wa Gokona uliokuwa unatiririsha maji ya sumu ili ufanyike ukarabati wa mabwawa ya kuhifadhia maji machafu.

Pia walitaka watendaji wa serikali na mgodi waliohusika kuficha ukweli wa tukio la maji ya sumu kutiririkia mtoni waadhibiwe, na kampuni ilipe fidia ya mali zao kwa viwango vya kimataifa na kuhamisha wakazi wa eneo hilo.

Hawa walitaka Barrick idhibiti maji yenye sumu yasiingie mtoni na katika visima vya maji; igharamie matibabu kwa watu walioathirika na sumu.

Vilevile waliomba kampuni itoe njia mbadala ya kupata maji safi na salama kama vile kuchimba visima virefu na mabwawa kwa ajili ya matumizi ya binadamu, mifugo na shughuli za uzalishaji mali.

Ngeleja hatasahau adha aliyopata hapa yalipo makao makuu ya Nyamongo. Alipokuwa naibu waziri katika wizara hiyo aliwaambia wakazi kwamba atahakikisha wanapata haki yao.

Alipokwenda mara ya pili akiwa waziri kamili aliwapa matumaini hakutakuwa na kikwazo kwa vile sasa yeye ni alfa na omega tofauti na awali.

Alipoingia katika msafara wa ‘kuzima moto’ wakazi hawakutaka kusikiliza usanii wake. Polisi walilazimika kuingilia kati kuzingira kwa lengo la kumwokoa na hatari ya kudhuriwa kwa kutoa majibu mepesi.

Risala yao haikutofautiana na tatu zilizopita kwani nao walitaka maji yadhibitiwe yasiingie kwenye vyanzo vya mito; kampuni ihamishe mkondo wa Mto Tigithe usipite karibu na maeneo yanayotiririka maji ya sumu, na watu wote walioathiriwa na sumu, wakiwemo watakaothibitika baadaye, mali na mifugo yao watibiwe kwa gharama za mgodi.

Aidha, walitaka wananchi wanaoishi karibu na mgodi wapewe maji mbadala yaliyo safi na salama; watu wote waliohusika kupotosha ukweli kwa kusema maji hayo ni salama wakati hayafai, wawajibishwe; na serikali itoe tamko la haraka juu ya maji ya Mto Tigithe kwamba yatumike au yasitumike kwa watu na mifugo.

Ndugai na wenzake walioshuhudia maji mazito mekundu yakiingia mtoni walipigwa butwaa Barrick walipokiri ni kweli walitiririsha maji ya sumu; na ni kweli sumu ile inaathiri, na ni kweli maji hayakuwa salama kutumiwa na binadamu.

Siku ya mwisho, Kamati ya Ndugai iliachwa mdomo wazi ilipoambiwa katika mkutano na maofisa kutoka Ofisi ya Mkemia mkuu na Baraza la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) na Lake Victoria Initiative kwamba PAF ina madhara.

Mshangao
Katika kila kata ambako msafara wa Ndugai ulikwenda, wataalamu wa afya walichukua sampuli za damu ya watu waliodaiwa kuathiriwa na maji yale kwa ajili ya utafiti wa kimaabara.

Lakini kilichoshangaza, serikali ya CCM ikilenga kuficha kashfa, ilikataa kutoa ripoti ya uchunguzi ikidai haina fedha za kufanya utafiti wa kina.

Hadi nilipofanya ziara ya pili mwaka jana, utekelezaji pekee wa mapendekezo ya wananchi uliofanyika ni wa kujenga mabwawa mengine ya kuhifadhi maji ya sumu katika mgodi wa Gokona, lakini maji ya sumu ya cyanide kutoka mgodi wa Nyabirama yalikuwa yanaendelea kutiririka.

Walichokifanya Barrick ni kuomba askari wa FFU ambao sasa wamepiga kambi hapo, kulinda mgodi hasa yanakotiririka maji yenye sumu hiyo.

Hili ni eneo la ghadhabu. Walinizuia kwa muda wa nusu saa wakinihoji kwa kupiga picha hapo. FFU hao wanaoishi kwa kodi za wananchi wanatembeza mkong’oto kwa wapita njia.

Hao ndio wanaua watu kwa visingizio ni majambazi au wamevamia mgodi. Inakadiriwa zaidi ya watu 70 wameuawa tangu Barrick wachukue mgodi huo kutoka Placer Dome mwaka 2006.

Hadi mwaka jana, Serikali ya CCM ilikuwa haijaanza kuchimba visima vya maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu na haitaki kusimamia malipo ya fidia halali kwa mamia ya wakazi ambao maeneo yao yaliporwa na mgodi. Kwa kuwa mgogoro umedumu miaka 15 sasa, ni dhahiri CCM imetia saini kupuuza wananchi.

0789 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: