CCM imechoka, italeta maafa


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 09 March 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi
Waziri Wassira

CHAMA Cha Mapinduzi kimechoka. Kimeshindwa siasa. Kinaomba “vyombo vya dola” kuingilia kati kudhibiti wanaofanya siasa. Hii maana yake ni kwamba kinajisalimisha kwa majeshi. Huu ni mchoko mchafu.

Yote haya eti ni kwa kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo kimeanzisha “madarasa ya umma” – kuelimisha wananchi juu ya kinachoendelea ndani ya ofisi, kumbi na kwenye baraza za utawala; na kujadiliana nao juu ya mustakbali wa taifa lao.

Rais Kikwete anasema CHADEMA wanataka kuvuruga amani. Kwamba wanafanya maandamano yenye nia ya kuondoa utawala wake (!). Waziri wake wa “mahusiano” Stephen Wassira, hataki suluhu. Anaonya kuwa CHADEMA wasije wakalalamika pale “serikali itakapoishiwa uvumilivu.”

Wassira na Ofisa wa habari wa CCM, John Chiligati, wanakubaliana kuwa maandamano na mikutano ya vinahamasisha uasi na kuchochea chuki dhidi ya serikali. Wanahitimisha kwa kuomba “vyombo vya dola kuwa imara kuchukua hatua za kisheria” kukabiliana na CHADEMA.

Maana ya serikali “kuishiwa uvumilivu” ni serikali kushindwa kwenda kwa hoja; kushindwa kujibu maswali mengi ya wananchi; kujisikia kukerwa na kupatwa na kiwewe. Maana halisi ni kwamba serikali imeishiwa pumzi. Ndicho alichosema Wassira.

Je, hayo yaweza kutokea sasa? Katika siku 100 tu za kwanza za ngwe ya pili ya Rais Kikwete – serikali inakosa pumzi? Inataka kutumia “vyombo vya dola” kukabili wanaoandamana na kuhutubia mikutano? Chiligati na Wassira wanataka kutawala pamoja na askari – polisi, jeshi na usalama wa taifa?

Niliwahi kumnukuu rafiki yetu Profesa Wole Soyinka – msomi wa fasihi wa kuheshimika na mshindi wa Tuzo ya Kimataifa ya Nobel akisema, wanasiasa wanaopenda kutumia mabavu katika tawala zao, si afadhali wakabidhi kabisa tawala zao kwa wale waliofunzwa jinsi ya kutumia mabavu.

Aidha, CCM inataka kutunga taratibu, kanuni na sheria vya kuongoza vyama vingine vya siasa jinsi vitakavyoweza kuikosoa, kuipinga kistaarabu –  bila kuichokonoa zaidi, bila kuiumbua, bila kuiaibisha, bila kuidhoofisha, bila kuiacha uchi.

Mtindo huu utaua haki na uwezo wa kufikiri na kuwa na mawazo. Utaziba mifereji ya fikra ya watu wengi kwa kuwa wanaotawala hawataki kutawala wanaofikiri bali aina ya misukule – ebintungwa. Hatari! Mtindo utalea chuki za chinichini ambazo mlipuko wake na athari zake kwa utawala na taifa, vyaweza kuzidi ule wa mabomu ya Mbagala na Gongolamboto kwa pamoja.

Hata kule ambako akina Wassira na Chiligati wanataka kukimbilia, hakuko salama. Walioko katika vyombo vya ulinzi vya dola – ambavyo ni vya wananchi – ni watoto wetu, ndugu zetu na marafiki zetu. Lakini zaidi, hao ni watu na wananchi raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Chukua yeyote. Kaa naye pembeni. Mhoji. Utakuta ana uchungu wa nchi yake hata kuliko wale wanaojitangaza kila leo. Atakuorodheshea wizi ndani ya BoT, ndani ya Hazina, ndani ya ofisi za serikali na hata ndani ya eneo lake la kazi.

Anaweza kukushangaza kwa kukueleza jinsi ambavyo yeye na wenzake wamekuwa wakifuatilia taarifa za wizi, uporaji na ufisadi uliopitiliza katika mikataba mbalimbali ikiwemo ya migodi; ulaghai katika Richmond, Dowans na IPTL na hata katika ununuzi wa vyombo vya usafiri serikalini.

Kwamba wamevaa magwanda, haina maana kuwa waviomo katika vyombo vya dola hawajui kinachoendelea; kwamba hawaoni nani anafuja nini na wapi; kwamba hawana mbongo za kufikiri, uwezo wa kufanya maamuzi na nyoyo za kuchukia.

Tena afadhali Chiligati na Wassira wangefikiria jinsi ya kujiondoa gamba, kama alivyosema Kikwete. Kwamba chama chake lazima kichukue tabia ya nyoka ya kujiondoa gamba kuukuu na kupata jipya. Kwa njia hiyo waweza hata kufanya ulaghai mpya ndani ya ghiliba ya zamani.

Lakini hawawezi kufanya ghiliba kwa kutumia vyombo vya dola. Vyombo hivi siyo vipande vya mashine au makombora. Ni akili zilizoajiriwa kazi maalum. Ni watu wanaofikiri na wenye uchungu na nchi yao. Kujaribu kipiga mbiu kwa vyombo vya dola ili vinyamazishe wanaotoa sauti za wasio na sauti, ni uhalifu mwingine wa aina yake.

Huo hasa ndio uchochezi. Uchochezi unaofanywa na walioko kwenye utawala. Si uchochezi tu; ni vitisho hata kwa wananchi kuwa vita vitakuja na kwamba wananchi watakufa. Kwa hiyo kama hawataki kufa, wakatae kusikiliza CHADEMA.

Leo hii CCM na viongozi wake, wamefanya uchochezi na vitisho kuwa ndiyo siasa yao. Ushawishi umetoweka. Mijadala imeyeyuka. Shuruti imetawala. Bali “madarasa ya umma,” kama hayakuendelea hadharani, yataendelea kimyakimya. Kiko wapi ambacho CHADEMA wanasema na hakipo? Angalia mifano michache hii.

Wananchi wanaambiwa kuwa kampuni ya Meremeta iliiba mabilioni ya shilingi; serikali ikakaa kimya. Kwanza serikali ilisema Meremeta ni kampuni ya serikali kwa asilimia 100 inayoshirikiana na jeshi la wananchi. Ilipogundulika kuwa ni wezi tu, bado serikali haijafanya lolote. Uchochezi uko wapi.

Darasa linagusa ukimya wa serikali kuhusu wizi wa mabilioni ya shilingi uliofanywa na makampuni ya Kagoda Agriculture Limited na Deep Green. Serikali iko kimya. Haitafuti wezi; haiwaambii chochote wananchi.

Wanafunzi wanaelezwa kuwa serikali imekaa kimya kwa miaka sita sasa, bila kununua mitambo yake ya umeme, huku “washikaji” wakisubiri ukame na ukosefu wa nishati ya umeme ili watekeleze wanachoita “misheni ya Dowans” – wanunue au wawashe mitambo hii na washikaji waneemeke.

Madarasa ya umma yanahusisha elimu juu ya wanaotawala ambao hawana uwezo wala sifa za kuwa kwenye mamlaka. Kila mmoja anatajwa alivyo kwa wananchi kuelewa kwa nini “mambo hayaendi” na kwa nini mkuu wa kaya hachukui hatua.

Katika mazingira bora ya kisiasa na uhuru wa kutoa maoni, inatarajiwa kuwa aliyesemwa, kama ameumia, amekashifiwa, aende mahakamani. Kwa njia hii CCM yaweza pia kwenda mahakamani na hata serikali, au rais kutaka haki itendeke.

Wanasiasa wa CCM hawataki hayo. Wanatishia wananchi na vyama vyao. Wanataka kuviundia utaratibu wa kufanya kazi za siasa. Wanakodisha hata baadhi ya wanachama na viongozi wa vyana vidogo vya upinzani; na kuomba au kuamuru msajili wa vyama vya siasa kukuza na kuendeleza vitisho.

Mbona Tanzania ni jukwaa pana? Kwa nini CCM inataka kubana wananchi ili waimbe wimbo uleule, sauti ileile kwenye jukwaa lilelile, wakati kuna fursa za ubunifu na katika viwanja ainaaina?

Kuna njia ya kusaida CCM isife; kwani ikifa vyama makini vitakosa mshindani. Nayo ni kuiambia kuwa watu makini wa nchi hii, na hasa sasa, siyo wa kutishia kwa nyau. CCM ikijaribu, kwa njia yoyote ile, kuzuia uhuru wa watu na vyama, kufikiri na kutoa maoni, hata kile wanacholilia hawatakipata. Tutakataa.

0713 614872 ndimara@yahoo.com www.ndimara.blogspot.com
0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: