CCM imechoka, serikali legelege


editor's picture

Na editor - Imechapwa 03 August 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

JUNI 8 mwaka huu, serikali iliwasilisha bungeni bajeti yake iliyokuwa inaainisha makadirio ya makusanyo ya mapato na matumizi kwa mwaka 2011/ 2012.

Serikali iliwasilisha bajeti ya Sh. 13.5 trilioni ikibainisha vipaumbele kadhaa vya kutekeleza, kama vile nishati na ujenzi wa barabara. Na ili kukabiliana na tatizo kubwa la wafanyabiashara wa mafuta wasio waaminifu, serikali ikatangaza kuongeza bei ya mafuta ya taa na kupunguza ushuru katika bidhaa za petroli.

Hivyo ndivyo Baraza la Mawaziri chini ya Rais Jakaya Kikwete liliona inafaa kukabili changamoto mbalimbali za kiuchumi.

Lakini kinyume na matarajio ya serikali, katika kipindi cha wiki mmoja ya mjadala wa bajeti hiyo, wabunge hasa wa upinzani, walipinga pendekezo la kuongeza ushuru katika mafuta ya taa kwa vile lingesababisha ongezeko la bei kwa bidhaa hiyo inayotegemewa na wananchi wengi wasio na uwezo wa kumudu gharama za umeme na gesi.

Aidha, wananchi nao walitahadharisha na vyombo vya habari vilionya kuwa hatua hiyo ingewaumiza maskini na kulazimisha wengi kutumia mkaa na kuni jambo ambalo litasababisha ukataji mkubwa wa miti kwa ajili ya nishati.

Rai hiyo iliangukia kwenye masikio mfu ya serikali ya CCM, na ikishangiliwa kwa makofi na wabunge wa CCM ikapandisha bei ya mafuta ya taa.

Cha kushangaza ni kwamba, mwezi mmoja tangu bei mpya ya mafuta ianze kuuma, Kamati Kuu (CC) ya CCM iliyoziba masikio kipindi chote cha mjadala huo, imeibuka na kuitaka serikali ipunguze bei ya mafuta ya taa.

Katika taarifa yake, Kamati Kuu imedai haijaridhishwa na kiwango cha bei ya mafuta ya taa nchini kwa kuwa ndio nishati inayotumiwa na wananchi wengi wenye kipato cha chini.

Aidha, CCM imesema haikuridhishwa na maelezo ya kupandishwa kwa bei ya mafuta hayo kwa kisingizo cha kuzuia uchakachuaji wa mafuta mengine.

Tunaitaka serikali ya CCM iache kutania, kukejeli watu na kujidhalilisha. Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete na ndiye pia Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri. Ameshindwa vipi kuliona tatizo hilo mapema? Alikuwa wapi wananchi walipopinga ongezeko la bei hiyo? Hivi, Rais alikuwa anasubiri kikao cha CCM ndipo ajiagize kwenda kupunguza bei serikalini? Huu ni uchovu hatari kwa mustakbali wa nchi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: