CCM imejivua magamba mawili tu


Nyaronyo Mwita Kicheere's picture

Na Nyaronyo Mwita ... - Imechapwa 20 April 2011

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

KWA kuwaondoa Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, Naibu Katibu Mkuu Bara, George Mkuchika na mwenzake Saleh Ramadhani Ferouz wa Zanzibar, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejivua gamba lipi?

Kweli kumpandisha Mkuchika na kuwaondoa Amos Makala na Bernard Membe CCM imebadilika?

Hivi hao wajumbe wapya wa sekretariati ya CCM Nape Nnauye, Emanuel Nchimbi, January Makamba na Wilson Mukama wataleta mabadiliko wakati wapo chini ya Mwenyekiti yuleyule aliyeshindwa kufuta ufisadi?

Vijana walioingizwa kwenye sekretarieti kwa mara ya kwanza wataleta mabadiliko gani wakati wapo chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara yuleyule na hata wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM bado ni walewale?

Viongozi wa CCM mikoani nchini kote ni walewale, viongozi wa CCM wilayani nchini kote ni walewale, viongozi wa kata zote nchini ni walewale na bado CCM wanadiriki kudai eti wamejivua gamba? Gamba lipi?

Hakuna, kwa sababu ilichofanya ni kubadilisha viongozi wachache na kuweka wengine waliokuwepo wakati ufisadi umezidi lakini hawakushiriki kupambana kuufuta.

Angalau Nape alithubutu. Alilalamikia ujenzi wa jengo la kitegauchumi la UVCCM, ingawa alikemewa hata akatoswa na wenzake. Akanyamaza.

Kama kuna gamba limevuliwa basi itakuwa halikuvuka mwilini maana kama ni shati limevuliwa upande mmoja tu. Kwingine bado linaning’inia.

La, kama gamba lenyewe ni gauni basi limevuliwa tu mabegani, sasa limegota kiunoni halijaacha mwili. Vizuri gamba likavuliwa mwili mzima. Bado CCM ina magamba mengi. Iyavue ndipo ikubalike.

Naona magamba mawili tu yamevuliwa. Kwanza, lile la Richmond na Dowans linalowahusu mbunge wa Igunga, Rostam Aziz na wa Monduli, Edward Lowassa. Gamba la pili lililovuliwa ni kwa mtuhumiwa wa rada, mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.

Ili CCM ipendwe, inapaswa kujivua gamba la tatu la dhulma. Bila ubishi ilishajichafua mbele ya umma.

Ilipora viwanja vya mpira mikoani. Hivi vilijengwa na wananchi wakati wa mfumo wa chama kimoja. Itikadi yao wakati ule ilikuwa ni kujenga taifa. Ulipoingia mfumo mpya, CCM ikajimilikisha. Ni haramu.

Chimwaga tulilochangia nchi nzima ili liwe makao makuu yake lilivyorudishwa serikalini basi na viwanja hivi virejeshwe serikalini.

Bora vimilikiwe na vyama vya mpira vya wilaya au mkoa. Si hivyo, CCM itazidi kuandamwa na magamba yaliyobaki.

Dhulma waliyofanyiwa wastaafu wa Afrika Mashariki inaumiza. Maofisa wamekula fedha za wastaafu lakini hawataki kulipa. Isipokuwa wapo tayari kulipa Dowan/Richmond? Haingii akilini.

Uonevu ni gamba la nne. Chochote kinachofanywa na viongozi wa serikali waliogombea vyeo kupitia CCM ni viongozi na makada wake na hivyo yote wanayoyafanya yakiwa ya maonevu, yamefanywa na CCM kuonea wananchi.

Mfano mzuri ni uvunjaji wa nyumba bila fidia maeneo ya hifadhi ya barabara kuu nchini. Sheria ya Ardhi ya 1999 inasema ardhi ni mali, na mtu hatanyang’anywa bila fidia. Kutenda kinyume ni kuvunja sheria.

Sheria ya utwaaji wa ardhi (Land Acquisition Act, 1947) inatoa viwango vya malipo vitakavyotumika kama ardhi ya mtu inatwaliwa, lakini Waziri John Magufuli na Wakala wa Barabara (TANROADS) wanavunjia watu nyumba eti kwa sababu zimeingilia eneo la hifadhi ya barabara!

Mpanda ilikuwa wilaya lakini leo ni mkoa wakati Kaliua ilikuwa tarafa, leo ni wilaya hivyo barabara ya Kaliua/Mpanda sasa ni barabara kuu yenye hifadhi ya barabara mita zaidi ya 30. Kuwavunjia bila fidia waliopo eneo hilo sasa ni ukatili.

Gamba la tano, nyumba. Hili linawahusu wote waliopora nyumba na sasa hawazitumii, wamezipangisha na wanalipwa kwa dola.

Nyumba za umma zinagawiwa ovyo kama vile kiama kimewadia, au kwamba mwisho wa watu kutawaliwa umefika! Makada wa CCM serikalini wakaamua kujigawia nyumba hizi na kuwapa wake, watoto na marafiki zao.

Tunafahamu hata Mwenyekiti wa CCM wakati ule, Benjamin Mkapa, na aliyemrithi, Rais Jakaya Kikwete, walipewa. Ni ufisadi maana ilichukua serikali mwaka mmoja tu kutumia fedha nyingi kujenga nyumba kama kijiji pale Mikocheni ili wakae mawaziri aliowaua Kikwete.

Gamba la kurithishana vyeo/madaraka. Kila mkubwa CCM anaacha kimelea chake uongozini CCM ili kije kitutawale siku moja. Wao tu kwenye ngazi za juu CCM ndio wanaojua kuzaa? Vueni gamba hili.

Gamba la saba: kupora viwanja vya wazi. Kila kiwanja cha wazi Dar, Mwanza, Arusha na kwingineko kimejengwa ofisi ya CCM! Hata matawi ya wakereketwa yapo barabarani au maeneo ya wazi.

Waziri Magufuli alipoanzisha kampeni ya kuvunja nyumba maeneo haya aligundua ninalolieleza hapa. Akaishia. Waziri Anna Tibaijuka naye amepoa licha ya kuahidi kulivalia njuga tatizo hili. Atawezaje kuibomoa CCM.

Gamba la nane la kugawa ovyo mali ya umma kwa mtu yeyote mweupe anayeonyesha dalili za kutaka mali za Tanzania. Zaidi ya nyumba, sijawahi kusikia mtu mweusi au Mswahili kagawiwa mali ya umma bure.

Angalia waliopewa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa bei poa. Wakapewa majengo mazuri ya benki. Wenyewe walivyoingia mkataba tu wa kununua NBC, wakayauza na kupata mara mbili ya zile walizonunulia. Wajinga ndio waliwao.

Wakagawa viwanda, ranchi, mashamba na mashirika. Waliopewa ni weupe. Haya yalifanyika wakati wameletwa nchini watu hawa kuongoza shirika lililoanzishwa rasmi kubinafsisha mashirika ya umma maarufu kama PSRC.

Wakati wa kubinafsisha shirika la reli, CCM wakakumbushwa walivyogawa vyote hivyoa. Wakasema wapo makini. Kweli, maana leo gari moshi la Kigoma na Mwanza linaondoka Dar mara moja tu kwa mwezi.

Gamba la tisa: Eti CCM wanawafanyia makosa Watanzania lakini hawataki kupingwa. Yeyote anayewapinga wanadai anahataharisha amani yetu, mshikamano wetu na upendo wa taifa!

Injili mpya kwa Wagalatia na Wakorintho wa Tanzania inayohubiriwa na CCM siku hizi inasema wananchi wakikosewa na chama nambari wani wasilalamike maana kulalamika ni kuhatarisha amani na upendo. Gamba kwa CCM.

Na wanaohubiri injili hii ni Mwenyekiti wa CCM, mawaziri na wabunge karibu wengi wao wakituhumiwa kuiba kura.

Sisahau gamba la kumi: Matusi ya UVCCM. Watoto wa viongozi hawa lakini wanatukana wakubwa bila kujali umri na nyadhifa zao. Wanatukana viongozi wastaafu. Gamba la matusi haliwatoki CCM.

Vijana wa CCM wanakutana Bagamoyo na kutangaza siasa za kibaguzi eti kanda fulani nchini isahau kabisa kutoa rais 2015. Hivi vijana hawa walikuwa wapi wakati ufisadi ukifanyika kwenye maeneo mbalimbali? Si wangetukana mafisadi!

Lipo pia gamba nene la CCM kuwa chama dola, cha mapolisi na majenerali wa jeshi (siyo wanajeshi wa kawaida) wenye uwezo wa kupiga ramli na kutabiri vyama vitakavyopinga matokeo ya uchaguzi kabla ya uchaguzi wenyewe kufanyika.

Mbele ya macho ya wananchi, CCM ni chama cha Polisi chini ya IGP Said Mwema mwenye uwezo wa kiintelijensia wa kujua nani ataandamana kwa amani na nani atafanya fujo kesho. Polisi hawapatikani wakitakiwa kuongoza maandamano lakini hupatikana ghafla tena kwa wingi ukilazimisha kuandamana.

Hatujasahau ya IGP Omar Mahita ambaye siku moja kabla ya uchaguzi alionesha waandishi visu vyenye rangi ya CUF na kudai kimepanga kuvuruga uchaguzi lakini baada ya uchaguzi na mpaka leo hakuwapeleka wenye visu vile mahakamani wala kuwataja.

Haya ni magamba machache tu. Mbona yangalipo mengi? Kwa vingozi wanavyotenda, itachukua karne kuyavua.

0785788727 Kicheere@yaho.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: