CCM imeshindwa kulea Muungano


editor's picture

Na editor - Imechapwa 28 July 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

HAKIKA sasa serikali mbili za Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zimeshindwa kulea Muungano wa maridhiano.

Zinafokeana. Zinatishiana. Zinalaumiana. Zinatuhumiana. Zinatiliana mashaka. Karibu zitashikana "uchawi."

Upande mmoja ukianza kwa kauli nzito, mwingine unajibu kwa kauli za maudhi. Kwa bahati mbaya, malumbano yao sasa yameingia hata ndani ya vyombo vya kutunga sheria – Baraza la Wawakilishi (BLW) na Bunge.

Matukio mawili yanatosha kueleza kiwango cha malumbano. Kwanza, suala la iwapo Zanzibar ni nchi au laa. Pili, hatua ya SMZ kutangaza kuondoa shughuli za utafiti na uchimbaji mafuta na gesi asilia katika orodha ya mambo ya Muungano.

Hili la hadhi ya Zanzibar ndani ya Muungano, lilianzia bungeni mwaka jana na hatua ya SMZ kuhusu shughuli za utafiti na lile la uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, lilianzia BLW.

Moto mkali umewaka kwa njia ya kauli za viongozi; na moto huu haujazimika, hata kama moshi umepungua.

Yote haya yanatokana ukosefu wa uvumilivu wa kisiasa miongoni mwa viongozi na kutokuwa na nia njema katika kutatua matatizo ya msingi yanayokabili Muungano.

Tukipima maoni ya Watanzania, tunaona kila upande unataka Muungano uendelee. Bali wote wanapenda kuona Muungano wa maridhiano na unaonufaisha pande zote.

Tume ya Nyalali ya mwaka 1992 ilionyesha matakwa ya wananchi juu ya Muungano.

Hatima ya Muungano ilichukua nafasi kubwa katika maoni ya Tume. Kuondokana na matatizo kulihitaji kuimarishwa Muungano.

Lakini viongozi wameshindwa kuchukua hatua zifaazo. Badala yake, wanaendeleza uhusiano wa "paka na panya." Kutegana na kutegeana. Hali ya sasa ni matokeo ya udhaifu wao. Kila upande unalalamika na kuona una haki zaidi.

Muhimu ni kuendesha Muungano kwa kila upande kujali makubaliano na maslahi ya mwingine. Hapana sababu ya kiburi wala jeuri.

Wakati tunajua ni haki kulalamika, tunataka wajadiliane na kumaliza tofauti zao. Lakini mijadala lazima iwe ya wazi, ya kuheshimiana na hatimaye ilete majibu endelevu.

Mijadala isiyoisha haijengi. Inabomoa. Inakomaza matatizo. Inatishia amani, umoja na mshikamano uliokusudiwa kujengwa kupitia Muungano.

Hii ndiyo changamoto nzito kwa CCM na serikali zake. Afadhali marafiki waishio jirani kwa upendo kuliko wandani waparuranao kila kukicha.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: