CCM imetikiswa ikatikisika je, itanusurika?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 20 April 2011

Printer-friendly version
Gumzo

HIVI nyoka akijivua gamba anakuwa mjusi au kenge? Kijana mdogo wa darasa la tano jijini Dar es Salaam, amesaidia kujibu swali hilo. “Nyoka anabaki nyoka.”

Amepata. Nyoka huendelea kubaki nyoka yuleyule, lakini akiwa amekuja kwa gamba changa. Wala sumu ya nyoka aliyejivua gamba haiwezi kuwa maji au asali. Ni sumu ileile.

Kuamua kuwataja Edward Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge, ambao viongozi wapya wa CCM – katibu mkuu, Wilson Mukama, naibu katibu, John Chiligati na katibu mwenezi, Nape Nnauye – wanataka wafukuzwe kutoka katika chama hiki, hakufanyi chama kuwa safi. 

Ukimwondoa Nape ambaye anaonekana kucheza ngoma asiyoijua, hakuna kiongozi yeyote ndani ya CCM anayeamini kuwa chama hicho kweli kimedhamiria kupambana na ufisadi. Hata mwenyekiti wa chama hicho hawezi kuaminika katika hili.

Hii ni kwa sababu, kama Kikwete alikuwa na nia ya kuwaondoa katika chama swahiba zake hawa, mkutano wa NEC wa Dodoma ambao watuhumiwa wenyewe walikuwapo, usingeisha kama ulivyoisha.

Mkutano ungeisha kwa azimio na mapendekezo kwa Mkutano Mkuu kwamba hawa siyo wasafi na kwamba inapendekezwa wasimamishwe uongozi na hata kufukuzwa uanachama. Mkutano mkuu hufanyika kwa ajenda za Halmashauri Kuu (NEC, isipokuwa kwa ajenda maalum. Hayo hayakuwepo.

Pili, Kikwete anajua nguvu ya marafiki zake. Naye wanamjua. Anajua kuwa kila dakika ambayo Rostam ataipata ataitumia kujiimarisha ili kujinasua kutoka katika kitanzi cha kufukuzwa katika chama. Hivyo si kazi rahisi kutekeleza mpango huu katika siku za usoni.

Ni wazi basi kuwa viongozi wengi wa ngazi ya juu wa CCM wanajua kuwa “kujivua gamba” ni mchezo unaochezwa ndani kwa ndani na kwa kuviziana. Maana kama ni ufisadi, umewanufaisha wote. Je, nani awezaye kukata mti aliokalia Abunwasi?

Kwa mfano, kama mabilioni ya shilingi yalikwapuliwa mahali na kunufaisha chama, basi yamenufaisha pia wanachama mmojammoja.

Ni mabilioni hayohayo ambayo yanaweza kuwa yalitumika kupata  wabunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Ni mabilioni hayo yanayoweza kuwa yalitumika kumuingiza madarakani rais; na yaliyotumika kuchafua baadhi ya wenzake katika chama na nje ya chama chake.

Hata ndani ya serikali, maamuzi mengi ambayo yamefanywa na wale walioamua kuwaita mafisadi na labda kuwatoa kafara, yanawahusu hata wale ambao hawakutajwa na hata wakubwa zao. Mfano hai ni mkataba tata wa Richmond.

Pamoja na Lowassa kuonekana kutumia madaraka yake kutoa kushawishi au kupendelea kampuni ya kufua umeme ya Richmond na hivyo kuipa mkataba wakati haikuwa na sifa, lakini Kikwete hawezi kusema “sikujua” kilichokuwa kinatendeka.

Kuna madai kuwa kuna uthibitisho kuwa Lowassa alikuwa akijulisha bosi wake kila kitu kilichokuwa kikitendeka. Hata ujio wa Dowans nchini unadaiwa kufanywa waziwazi.

Hapa inatarajiwa minyukano: Hivi Dowans ilipewa kazi hiyo bila kibali cha baraza la mawaziri? Kama ndivyo, basi tuhuma na shutuma ni nzito zaidi ya ilivyokuwa inaeleweka. Je, mkuu wa kaya alipoona hivyo alichukua hatua gani? Ni mzigo.

Tatu, ukiacha hilo, uchaguzi wa majuzi wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho kutoka miongoni mwa wabunge wake, umethibitisha kuwa hakuna mwenye dhamira njema ya kukitaka chama.

Miongoni mwa wajumbe saba waliopenya katika kinyang’anyiro hicho, ni Samwel Sitta pekee ambaye angalau anaonekana mwenye nafuu, ukilinganisha na baadhi ya wenzake walioshinda.

Kwa mfano, Abass Mtevu na Livigstone Lusinde, ambao hata chama hawakifahamu, wameshinda uchaguzi huo kwa kuwatupa nje ya kinyang’anyiro wanachama mashuhuri kama Christopher ole Sendeka na Brigedia Hassani Ngwilizi (!).

Wakati waliotajwa hawajasimama hadharani kukanusha ufisadi, lakini baadhi yetu tunaona kuwa hakuna tofauti yeyote kati ya waliobaki ndani ya chama na wale wanaotakiwa kutoka.

Mathalani, katibu mkuu mpya wa chama hicho, Wilson Mukama sidhani kama anaweza kusimama hadharani na bila kigugumizi kulaani wanaoitwa mafisadi wakati ni yeye anayedaiwa kumpa Kingunge Ngombale-Mwiru mradi wa kukusanya ushuru wa maegesho ya magari jijini Dar es Salaam uliokumbwa na tuhuma kedekede.

Kampuni ya Kingunge ya Smart Holdings, ilianza kazi hiyo wakati Mukama akiwa mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam na kabla haijasajiliwa kisheria. 

Hata Pius Msekwa hawezi kuwa shupavu katika kupambana na ufisadi. Mara kadhaa amekataa kuwa hakuna ufisadi ndani ya CCM. Hata baada ya mke wake, Anna Abdallah kuteleza na kukosana na mafisadi, alipoteza umaarufu wake baada ya mafisadi kumshughulikia kupitia mgongo wa Kikwete.

Naye Chiligati mara kadhaa amesikika akikebehi wale wanaopinga ufisadi. Ushahidi upo. Kuna wakati Chiligati alisikika akisema, “wanaopinga ufisadi ni genge la wahuni au wapinga ufisadi hawana tofauti na kikundi cha vichekesho cha ze komedi.”

Nne, kuondoa watuhumiwa wa ufisadi kwenye NEC pekee hakutoshi. Ufisadi unaosemwa umefanyika serikalini, si katika chama. Hivyo basi, huwezi kutaka kuondoa watuhumiwa wa ufisadi serikalini, lakini ukashindwa kufanya hivyo katika chama.

Lakini kuna hili pia: Watuhumiwa wote watatu – Lowassa, Rostam na Chenge, ni wabunge wa Bunge la Muungano. Bunge ni zaidi ya vikao vya CCM.

Ndani ya Bunge, Lowassa ameshika nafasi nyeti ya mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Ni mjumbe wa Kamati ya maadili. Ni kamati hizo zinazopanga ratiba na shughuli za kila siku za mikutano ya bunge.

Pamoja na kazi nyingine, bunge lina kazi ya kuishauri na kuisimamia serikali. Sasa kama CCM kweli kina dhamira ya kuondokana na watuhumiwa wa ufisadi, basi inapaswa kufika mbele zaidi kwa kuwaondoa mafisadi bungeni.

Ni jambo lisiloingia akilini, CCM iwaondoe mafisadi katika chama, lakini iwabakize kwenye bunge. Katika mazingira hayo, usafi wa chama utakuwa wapi? Nani anaweza kukiamini chama ambacho kimepeleka mafisadi bungeni?

Kimsingi hakuna anayepinga CCM kutaka kujisafisha. Kinachoelezwa hapa ni aina ya usanii unaotaka kutumika kuhalalisha kile kinachoitwa, kujivua gamba.

Kwa mfano, nani asiyefahamu ushiriki wa Zakia Meghji katika wizi wa Kagoda, angalau kwa njia ya kufumbia macho? Lakini ni aliteuliwa kuwa mbunge na ujumbe wa Kamati Kuu. Nani hafahamu kuwa alikuwa ni Meghji aliyetetea Kagoda hadi dakika za mwisho, kwamba ilipewa fedha hizo kwa ajili ya matumizi ya usalama wa taifa.

Kama Rostam anatolewa katika uongozi ndani ya chama kwa kuwa ni mchafu aliyeiba fedha za Kagoda, wachunguzi wanajiuliza Meghji anawezaje kupata utakaso wa kuingia Kamati Kuu?

Tano, hadi sasa wakati Kikwete anajitapa anataka kusafisha chama chake, NEC haijaeleza kuwa Dowans ni kitu haramu na serikali isikikaribie. Badala yake, kinachoonekana ni kumuondoa Rostam katika chama, huku serikali ikiomba kesi iliyofunguliwa iishe ili fedha zilipwe.

Sita, wizi mkubwa uliofanyika serikalini ulitokea wakati wa utawala wa Benjamin Mkapa. EPA ililipwa wakati wa Mkapa. Rada ililipwa wakati wa Mkapa. Ndege ya rais ilinunuliwa wakati wa Mkapa. Sasa kama yote haya yalifanyika wakati wa Mkapa, nini hatima ya Mkapa katika vikao vya CCM?

Kama Rostam alikutana na Mkapa kwa mujibu wa nyaraka zilizopo na kupanga jinsi ya kujichukulia mabilioni ya umma ndani ya benki, vipi Rostam aonekane anakichafua chama, lakini Mkapa awe anakitakasa?

Kutokana na hayo yote, ni wazi kuwa mabadiliko yanayotakiwa kufanywa ndani ya CCM, si kuwaondoa Rostam, Chenge na Lowassa pekee. Ni lazima Kikwete ahakikishe kuwa chama chake kinaweza kujitenga na wale wote wanaokichafua, vinginevyo mabadiliko yanayotajwa yatasababisha kuibuka kwa makundi mapya katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Hivi ni mtu gani anaweza kuamini kuwa CCM imejivua gamba kama kilichofanyika ni kuwahamisha abiria na kuwafanya wawe madereva na kuwachukua madereva kuwafanya abiria kwenye gari lilelile linaloelekea korongoni?

Chochote kilichofanywa na CCM ni jaribio la kujinusuru tu mbele ya macho ya wananchi. Ni kujaribu kujipa nafasi ya kuonekana kiko makini. Kama jambo hilo litabadilisha mioyo ya watu ni suala jingine. Kwani kuna watu wengine ambao hawaridhishwi na mabadiliko ya kimapambo.

Wengi wanaotaka mabadiliko ya kweli ndani ya CCM wanaangalia mabadiliko ya Katiba, sera, mfumo na muundo wake ili matatizo yaliyotokea hadi hivi sasa yasije kutokea tena huko tuendako.

0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: