CCM imevuruga vita dhidi ya ufisadi


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 06 June 2012

Printer-friendly version

MATUKIO mawili makubwa yalifanyika hivi karibuni. Jijini Dar es Salaam Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilifanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya Jangwani, huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikifanya mikutano ya ndani wilayani Misenyi mkoa wa Kagera.

Wingi wa watu waliohudhuria mkutano wa CHADEMA, binafsi sijapata kuushuhudia kabla ya hapo, ukiacha ujio wa Baba Mtakatifu Yohanne Paulo wa pili mwaka 1990. Chama kilichoshindwa katika uchaguzi mkuu kupata wafuasi wengi kiasi kile ni ishara mbaya kwa chama tawala.

Wazungumzaji katika mkutano ule, uliotumika kupokea mamia ya watu wanaojivua gamba la CCM na kuvaa gwanda, waliutumia vizuri fursa ile kuwaeleza mambo ya msingi kama vile kipi wahoji wakati wa kutoa maoni yao kwenye tume ya katiba na hasa yale yanayowagusa katika maisha yao ya kila siku.

Wakati hayo yakijiri Dar es Salaam  kule Kagera katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Nape Nnauye alikuwa anafanya mkutano wa ndani. Katika mkutano ule Nape aliwaambia wasikilizaji wake kuwa ni bora wanachama wanaotaka kukihama chama wafanye hivyo ili wabaki wachache halafu wakiimarishe. Akasisitiza, “…hata nikibaki peke yangu CCM haitakufa.”

Chama ni wanachama, Nape ataimarisha viupi CCM peke yake ikiwa itakuwa imekimbiwa na wanachama wote? Au ana maana CCM ikifa, itafufuka?

Bila shaka hata Nape hajabaini tatizo lao kubwa na la msingi linalowaangusha, kwamba ina viongozi wengi wadandiaji wa siasa za kubahatisha. Wanashindwa kujua kwamba zamani siasa ilikuwa kazi ya wapiga blaablaa, lakini sasa nyakati zimebadilika zinahitaji watu makini na wenye upeo wa hali ya juu. Nape asipolijua hili naye atachujuka na kufilisika kisiasa kwa kasi ya ajabu.

Baada ya mkutano wa CHADEMA kuna maoni kutoka kwa baadhi ya watu kwamba CCM nayo ijibu mapigo kwa kuitisha mkutano mkubwa zaidi ikiwezekana palepale Jangwani na kuwaeleza wananchi mambo yanayogusa maisha yao.

Hata hivyo mashaka yao ni kwamba walipowafikisha wananchi, nani atatokea Jangwani? Lakini kama wananchi hawatatokea, Jangwani basi huo ni ushahidi tosha kuwa CCM haitakiwi, iondoke kwa amani!

CCM ndiyo iliyounda serikali inayoongoza wananchi. Hivyo kuiandika CCM siyo majungu wala fitina! Ni kutokana na nafasi yake katika uongozi wa nchi hii.

Hapa hakuna upuuzi wa kushabikia chama wala mtu. Tunajadili mustakabali wa taifa letu. Hapendwi mtu wala chama kama ambavyo hachukiwi mtu wala chama.

Lazima tuwekane sawa kwa sababu nchi hii ni yetu sote tuliyopewa na Mwenyezi Mungu.

Keki ya taifa lazima tugawane wote kwa usawa. CCM itatajwa kwa wema kutokana na mema yake na kitatajwa vibaya kutokana na mabaya kinayoyaifanyia jamii.

Kama ilivyolazimishwa kuingia katika mchakato wa kuandika katiba mpya  bila kutaka, ndivyo serikali ya CCM ilivyolazimishwa kuingia katika vita dhidi ya ufisadi.

Katiba mpya kama ilivyo vita dhidi ya ufisadi siyo sera za CCM. Havijawahi kupewa kipaumbele chochote wala kuwekwa katika ilani yao ya uchaguzi.

Kutokana na shinikizo kubwa la wapinzani, vyombo vya habari, wanaharakati na wananchi kwa ujumla, CCM imeilazimisha serikali yake ikubali uandikwaji wa katiba mpya.

Mchakato unaendelea licha ya vikwazo vya hapa na pale. Katiba mpya itapatikana lakini kwa mapambano kama alivyosema Profesa Issa Shivji.

Baada ya CCM kupoteza mwelekeo, imeiweka nchi rehani. Utaratibu wa kuwa na mtu mmoja, huyohuyo mwenyekiti wa chama na huyohuyo rais wa nchi madhara yake ndiyo yanaonekana sasa. Chama kimepoteza mwelekeo, serikali nayo imepoteza mwelekeo. Hapa ndipo tulipofikishwa!

Ufisadi umeingia kila mahali katika chama na hivyo kukifanya kiwe na serikali iliyojaa ufisadi. Hivi sasa kumtafuta kiongozi asiyefisadi ndani ya CCM na ndani ya serikali yake ni mtihani mgumu. Kibaya zaidi wao wenyewe wanaifurahia hali hii.

Ufisadi umekuwa kama sehemu ya utamaduni wa CCM. Ndiyo maana mmoja akifanya ufisadi wenzake wanamlinda kwa kujua kuwa na wao ni hivyo hivyo! Wanalindana.

Mfano hai ni kwamba baada ya ufisadi wa kutisha kufichuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), na kamati za bunge wabunge karibu wote wa CCM walikuwa radhi mawaziri wao wanane waliotuhumiwa waendelee na kazi na ufisadi wao kama vile hakuna kilichokuwa kimetokea.

Christopher ole Sendeka, mmoja wa mitume, manabii wa upambanaji katika vita dhidi ya ufisadi alisema watuhumiwa ni wanadamu hivyo wasamehewe! Hii ni kwa sababu mlengwa wao hakuwemo katika orodha.

Mbunge wa Musoma vijijini, Nimrod Mkono na wenzake watatu – Kangi Lugora (Mwibara), Said Kessy (Mpanda Kusini) na Deo Filikunjombe (Ludewa) walijitofautisha wakatia saini fomu ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.

Mkono anasema alisukumwa na wizi uliofanywa mgodini Buhemba. “Kama kuna jambo zuri ni vizuri tukaliunga mkono bila kujali kama limetolewa na CCM au na CHADEMA,” alisema.

Akaongeza, “Kama wapinzani wana hoja nzuri ni vema tukawaunga mkono. Nawakilisha wananchi wapiga kura wa Musoma vijijini, wao ndio walionichagua, nina wajibu wa kuwatumikia na kuhakikisha wanasaidiwa na serikali yao ikiwa ni pamoja na kulinda raslimali za nchi.”

Mkono anasema alisikitishwa kuona polisi waliopewa jukumu la kulinda mali za mgodi wa Buhemba ndiyo hao hao waliogeuka na kuwa wezi na kuwasaidia wezi wengine kupora mali zote.

Anasema, “…hata ungekuwa wewe ukiona ile hali ya Buhemba na kisha ukaambiwa usaini fomu ya kutaka mawaziri wajiuzulu, ni lazima ungesaini”

Tujiulize, manabii, mitume na makamanda wa ufisadi Samul Sitta, Harrison Mwakyembe, Stella Manyanya, Ana Kilango na wenzao walikuwa wapi wakati Mkono akinyosha mkono kutia saini fomu ile ya kushinikiza hatua zichukuliwe?

Hatukuwahi kumwona Mkono akipanda na kuteremka kutoka jukwaa moja kwenda jukwaa lingine kwa kisingizio cha kupigana vita dhidi ya ufisadi. Taifa halijamsikia akiongea upuuzi wa gamba. Lakini ilipotokea vita ya kweli dhidi ya ufisadi alikuwa pale na akasaini fomu.

Watanzania wawajue viongozi wao walioko CCM, nani kiongozi mkweli na nani mnafiki. Saa ilipofika ya wao kuthibitisha uzalendo na uadilifu wao wote walifyata mkia. Lakini wakija kwa wananchi wanadai ni wazalendo na waadilifu! Chui hao waliovaa ngozi ya kondoo! Waogopeni kama ukoma!

Wanafiki wote wafunge midomo yao. Wananchi mabwege wamebaki wachache sana, watajizulia balaa! Waacheni watu wa Mungu wahangaike na dhiki yao ila Siku hazigandi mtakutana nao mbele ya safari. Kama siyo hapahapa duniani basi mbele yake YEYE aliye juu, kwa maana Muumba wetu ni mmoja!

0713 334239
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: