CCM ina uchawi mkali, umma umelogwa


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 21 March 2012

Printer-friendly version
Tafakuri

NIMEJIPA fursa ya kufuatilia kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Arumeru Mashariki zilizopamba moto kwa wiki ya pili sasa.

Nimefuatilia pia hata kampeni za kujaza nafasi za udiwani katika kata mbalimbali zilizo wazi nchini, hususan Kirumba, Mwanza ambako hakika joto la kisiasa liko juu sana.

Ukisikia tambo za wanasiasa unaweza kupatwa ugonjwa wa moyo. Lakini ukiwaza kwa kina zaidi, unagundua kitu kimoja tu kwamba kwa kiwango cha juu kabisa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekamatika.

Nilijipa wasaa wa kujiuliza maswali mazito, hasa nilipoona Rais mstaafu Benjamin Mkapa akipelekwa mzobemzobe Arusha kuzindua kampeni Arumeru Mashariki. Naye kwa kuwa ni sehemu ya madudu ya CCM akaishia kuvuna janga ambalo sasa anakula yeye na wa nyumbani kwake.

Itakumbukwa kuwa uchaguzi mkuu ulifanyika mwaka mmoja na miezi michache iliyopita; kwa uhakika kabisa ni mwaka mmoja na miezi minne na siku chache hivi. Chama kilichoshinda uchaguzi ni CCM, kilimwaga ahadi ambazo hazina kipimo. Mtu mmoja alinikumbusha kuwa pale Mwanza mgombea urais wa CCM aliwaambia wakazi wa jiji lile lililozungukwa na mawe kuwa ataligeuza kuwa sawa na California ya Marekani.

Lakini akanikumbusha jinsi alivyoahidi kununua meli kubwa kwa ajili ya usafiri Ziwa Victoria, akaahidi pia Kigoma kuwa ataweka meli mpya kubwa Ziwa Tanganyika; nako Ziwa Nyasa akaahidi meli kubwa kama kwenye maziwa mengine makubwa.

Rafiki yangu akanikumbusha jinsi alivyoahidi habari ya kufufua reli ya kati, ujenzi wa viwanja wa ndege vya kisasa Mwanza, Kigoma na Bukoba. Hakuishia hapo tu akakikumbusha alivyowaahidi wakazi wa jiji la Dar es Salaam maji ya uhakika na kusisitiza kuwa tatizo la maji lingekuwa historia.

Alinikumbusha utitiri wa ahadi hadi nikashindwa kuziorodhesha. Lakini mwisho akaniambia, hata kule Igunga kwenye uchaguzi mdogo walikwenda na gia ya ahadi kubwa kubwa ya kujenga daraja, wakapewa kura, wakarejea zao Dar es Salaam wamewaacha wananchi na shida zao, kama walivyokuwa.

Safari hii kazi imekuwa kubwa na ngumu Arumeru Mashariki. Hali si sawa na Igunga, kilio cha Wameru tangu zama za akina Japhet Kirilo ni ardhi, ni mapambano ya wananchi dhidi ya walowezi wa kigeni kuhodhi ardhi yote yenye rutuba, nyingine ikiwa imeachwa tu, haiendelezwi, ilhali wananchi hawaruhusiwi kutia mguu.

Haya yalikuwa kichocheo cha mapambano ya kudai uhuru, kumpinga mkoloni, na ndiyo yaliwafanya Wameru wachange fedha na kumpeleka Kirilo Umoja wa Mataifa kudai ardhi ya Wameru. Ni historia ndefu.

CCM imetawala jimbo hili kwa miaka yote isipokuwa kati ya 1995-2000 tu mbunge wake alipotoka upinzani. Kwa maana hiyo, kwa miaka 50 ya uhuru, miaka yote 45 mbunge wa jimbo hili ametokana na CCM, tena kwa bahati nzuri, mwaka 2005-2010 mbunge wake akawa Naibu Waziri wa Fedha.

Ni sawa na kusema kuwa kama ni kufanya mtihani na kuurudia, CCM imekwisha kurudia mtihani katika jimbo hili mara nane hivi, ama jimbo likiwa moja au likiwa limegawanywa kama lilivyo sasa.

Lakini katika kufanya mtihani wote huo na kuujua vilivyo, imeshindwa kupata majibu ya wananchi. Ardhi! Ni katika mazingira hayo, Mkapa alikwenda Meru bila kujiandaa na kuishia kumtukana Mbunge wa Musoma Mjini (CHADEMA), Vincent Nyerere, kuwa si wa nasaba ya Baba wa Taifa, Julius Kambarage Nyerere. Alikosea sana. Amevuna haki yake na ataendelea kuivuna!

Niliorodhesha ahadi za CCM kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kuwakumbusha wasomaji wangu kuwa, hata hapo Meru ahadi zinazoshushwa hakika ni upuuzi tu kwa kuwa hakuna yeyote miongoni mwa hao wanaojinadi kwa hakika ana dhamiri ya kweli nafsini mwake ya kutekeleza lolote katika hayo. Ni ulaghai mwingine wa kusaka kura.

Ni katika kuangalia siasa za taifa letu katika picha hiyo, mtu anajiuliza maswali magumu kwamba hivi CCM walinunua uchawi wao wapi? Maana mwaka baada ya mwaka wanawaloga wananchi ambao wanashindwa kugundua hila zao na kuwambia hapana!

Ni nani anaweza kusimama hadharani na kusema kwa dhati ya nafasi yake kuwa CCM inaishi kwa ahadi zake? Wapi?

Nani ana ujasiri wa kusema kuwa matatizo yote ya nchi hii si kazi ya mikono ya CCM? Wizi wa mali ya umma, rushwa iliyojaa kila mahali, kushindwa kuwajibika kwa viongozi, lakini kwa jumla wake kushindwa kujua nchi inakwenda wapi.

CCM imejaa uoza. Inanuka. Imeshindwa kujisafisha, lakini bado viongozi wake wana ujasiri wa kusimama katika majukwaa ya kisiasa na kuomba kura. Aibu!

Nilibahatika kusikiliza kampeni za CCM katika kata ya Kirumba, Mwanza, ambapo Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM alimwagiza mkurugenzi wa Jiji la Mwanza ampe zawadi ya udiwani wa Kirumba. Yaani Rais Kikwete hawezi kutawala kwa amani, hawezi kupambana na rushwa, hawezi kuwaletea Watanzania maisha bora kama alivyowaahidi mwaka 2005, hawezi kujenga uchumi imara, hawezi kuwakemea wezi na wala rushwa walioizingira serikali yake, hadi mkurugenzi wa jiji la Mwanza aampe zawadi ya udiwani wa Kirumba!

Ni jambo la kushangaza kwamba wakati akiitamani kata ya Kirumba, ana nchi nzima, ameshinda urais, amepewa kata zaidi ya asilimia 70, ana wabunge zaidi ya asilimia 70, ana nchi mikononi mwake; lakini hawezi kuleta tija yoyote mpaka aipate Kirumba.

Ni kwa namna hiyo hiyo wanafikiri hata Arumeru Mashariki ni jambo la kufa na kupona,  wakati huo huo serikali yake ya awamu ya nne ikiwa imeshindwa kupiga hatua yoyote ya maana ya maendeleo.

Ukiutazama umasikini unaonyemelea watu wetu, wakati huo huo ukaangalia Arumeru ilivyo na shida zake za ardhi, unashindwa kujua ni nini hasa kimewapa wakazi hawa huruma ya kuwapa kura CCM mara zote hizi?

Je, CCM haijui kuwa ardhi ni jambo nyeti Meru? Kama wanajua kwa nini mwaka baada ya mwaka wanaomba kura na kupewa lakini hawachukui hatua za kuwatatulia wananchi shida hizo?

Jibu ni jepsi tu; kama Mwafrika, CCM wana uchawi mkali ambao umewapumbaza mno wananchi kiasi cha kuamini bila kulogwa na CCM basi maisha hakuna. Hii ni fedheha ambayo wananchi wanapaswa kujiuliza mara nyingi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: