CCM inanengua midundo ya CHADEMA


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 13 June 2012

Printer-friendly version
Tafakuri

NAFURAHISHWA na siasa za Tanzania sasa kwa maana moja kubwa, kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM), mbali ya kujigamba kuwa hakuna kiongozi wa chama vya upinzani ambaye hakutokana nacho, kwa vitendo, kimethibitisha kuwa sasa kinafundishwa siasa na vyama vya upinzani.

Mwaka 2007 Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilipoanzisha operesheni sangara, CCM ilitoa kejeli dhidi ya CHADEMA. Operesheni ile iliendelea kuweka msimamo wa kufufua matumaini ya wananchi juu ya mageuzi ya kisiasa hadi uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ulipofanyika ndipo CCM waliposhtuka kuwa kama hawatafanya juhudi nchi ilikuwa imeondoka mkononi mwao.

Ukitafakari alichosema Katibu mkuu, Wilson Mukama katika ripoti yake juu ya CCM kupoteza mvuto kwa wananchi, ambayo ilisababisha kuvunjwa kwa kamati kuu ya chama hicho na kutupwa sektretariati iliyokuwa ikiongozwa na Yusufu Makamba, siyo kitu kingine zaidi ya kukiri kuwa operesheni sangara ilikuwa imewaacha hoi, hivyo wakati ulikuwa umefika wa kutafakari nyendo za CHADEMA na kutenda kama CHADEMA.

Hakuna ubishi kuwa hoja ya ufisadi haijapata kuwa ya CCM, na hakuna ubishi pia kwamba CCM tangu kuondoka kwa Mwalimu Julius Nyerere katika uongozi wa chama hicho mwaka 1987, haijawahi kujitangaza kwa wananchi kwa maana ya kusikiliza kero zao na kujiimarisha kama chama cha siasa.

CCM inakwenda kwa wananchi kama kuna uchaguzi tu. Mikutano na ziara za kujenga chama, haikufanywa na mwenyekiti aliyepokea mikoba ya Mwalimu Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, wala mrithi wake, Benjamin Mkapa na hata sasa Jakaya Kikwete hajafanya kazi hiyo, labda amemwagiza Nape Nnauye amfanyie. Matokeo yake Nape analikoroga!

Baada ya kuondoka kwa Mwalimu Nyerere, mbali ya kujigeuza kwa nguvu zote kuwa chama dola, iliongeza kasi ya kufungamana na dola baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi.

CCM ilifanya hivyo ikiamini kwamba ikishawatumia watu wa usalama, polisi na hata watumishi wengine wa umma kama wakuu wa wilaya na mikoa na wengineo, na ikitumia kodi za wananchi kwa mlango wa nyuma kujiendesha na kutisha wapinzani, basi itaendelea kusalia madarakani.

Katika kipindi kifupi sana, CCM imejikuta katika kona mbaya ikijibu mapigo ya wapinzani badala ya kuanzisha mapigo.

Kuna maeneo mengi sana CCM imelazimika kuachana na sera zake na kutekeleza za kambi ya upinzani, husasan CHADEMA. Mambo hayo ni kama suala la Katiba Mpya, kuanzishwa Chuo Kikuu Cha Dodoma, kupambana na mafisadi kwa staili inayoonekana sasa ya kuchukua hatua japo kidogo kuwafikisha mahakamani baadhi ya watumishi wa umma wa sasa na waliokuwako hapo kabla.

Katika mchakamchaka huu, ambao CCM inaendeshwa, bila kutaka, imejikuta ikikaa na kutazama CHADEMA wanafanya nini ili nao wafuate.

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnaye ameanzisha operehseni kama  ya sangara. Anajitahidi kufanya kile wataalam wa kompyuta wanasema  ‘copy and paste’ yaani kunakili kila kitu kama kilivyo.

Nape anajitahidi aonekane anafanya kazi ya CCM, lakini masikini anazidi kusaidia upinzani ama wa ndani ya CCM au nje.

Ipo mifano mingi, nitataja miwili tu. Akina Andrew Chenge na Edward Lowassa walipokataa kujiuzulu ndani ya CCM, walisema wazi kwamba wao siyo magamba.

Hawakuishia hapo, walimshitaki Nape na John Chilagati (Naibu Katibu Mkuu Bara) kwamba wanachafua chama na kuendekeza majungu dhidi yao. Si Nape, Chiligati wala Wilson Mukama (Katibu Mkuu wa CCM) walioweza kujitetea ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC).

Tambo na kejeli za Nape dhidi ya Chenge na Lowassa ambazo pia kwa kiasi fulani zilishabikiwa  na Mukama,  ziliwarudi kwa kuwa utaratibu wa kuwajibishana wakubwa siyo utamaduni wa CCM, anaiga kutoka kwa CHADEMA.

Pili, malumbano kati ya aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige (mbunge wa Msalala) na Nape ni aina nyingine ya kukosekana msimamo wa pamoja wa kichama wa kuwajibishana. Maige anamwona Nape kama mtu anayevuruga chama kwa ziara na kampeni zake mikaoni.

Mfano mwingine wa copy and paste ya CCM kwa operesheni sangara ni huu. Jumamosi iliyopita walifanya mkutano mkubwa wa hadhara katika viwanja vya Jangwani. Nia ya mkutano huo ilikuwa kuwaeleza wananchi kile ambacho kinafanywa na serikali katika sekta mbalimbali.

Mkutano ule, pamoja na watu wengine, ulihutubiwa na mawaziri  watano; Prof. Jumanne Maghembe (Maji), Steven Wasira (Ofisi ya Rais-Mahusiano), Prof. Ana Tibaijuka (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Dk. Harrison Mwakyembe (Uchukuzi) na Dk. John Magufuli (Ujenzi).

Kauli za mawaziri hao, hakika hazikuhitaji mkutano wa hadhara kueleza kinachofanyika katika ofisi zao. Fikiria kauli ya Wasira kwamba eti zitalimwa heka 100,000 katika bonde la Kilombero ili taifa lijitosheleze kwa mchele; au kulima mahindi ili kujitosheleza kwa chakula, hakuna ubishi kwamba ni mwendelezo wa masihara ya watumishi wa umma.

Wasira hakuweza kusema, kwa mfano, tangu mkakati wa Kilimo Kwanza uanze ni kwa kiwango gani miaka miwili na ushei sasa suala la uhakika wa chakula limepatiwa ufumbuzi?

Wasira hawezi kusema hayo kwa sababu ugumu wa maisha na bei ya chakula ilivyo nchini unahitaji aina ya kiongozi kama Wasira kutaka kubadili giza liwe mwanga tena bila kupepesa macho.

Ni jambo la kushangaza kuona mawaziri wakijisumbua kujinadi Jangwani wakati mtihani wao halisi unaanza Juni 12 mjini Dodoma mkutano wa bajeti utakapoanza.

Kwa hali ilivyo, na kwa uzoefu wa bajeti ya mwaka 2011/12 ya Sh. trilioni 13.5 ambayo hadi sasa imeacha mapengo mengi katika utekelezaji wake, haitarajiwi bajeti ya Sh. trilioni 15 kuleta mabadiliko yoyote,.

Ushahidi ni moto ambao tayari umekwisha kutangazwa na madaktari na walimu nchini juu ya haki zao. Wamekwisha kunusa na kubaini bajeti ijayo ni debe tupu!

Lakini tukiweka kando kauli za mawaziri hawa na tukisubiri kama kutakuwa na lolote la maana kwenye bajeti zao, itoshe tu kusema kuwa mkutano wa CCM Jangwani, Jumamosi iliyopita siyo kitu kingine chochote ila ni harakati za CCM kufuata nyao za CHADEMA; kufanya kama CHADEMA, kujibu mapigo ya CHADEMA’ kuonyesha kwamba nao wanaweza kuitisha mkutano wa hadhara na kuvutia watu wengi.

Ni jambo la kufurahisha kuona kuwa hatimaye CCM imeiachia nafasi CHADEMA ya kile kinachoitwa kwa kimombo ‘agenda setting’. CCM imejikuta ikihangaika kuziba mapengo yanayofunuliwa na CHADEMA na kwa kufanya hivyo inakosa mkakati wa maana yenyewe na serikali yake.

CCM imekubali kuchezeshwa kwata na inafuata mapigo na mirindimo ya CHADEMA. Katika mazingira kama haya ni vigumu kukwepa hitimisho kwamba CCM ni chama tawala kinachocheza mchezo wa upinzani.

Kwa kasi hii inakuwa vigumu kuelewa ni kwa jinsi gani watakwepa kuchapana bakora hadi mwaka 2015 na kushuhudia majeruhi wengi wa kisiasa watakaosaidia kuandika historia mpya ya chama hiki kikongwe nchini.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: