CCM inanufaika na umaskini wetu


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 18 April 2012

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

SIKUSHANGAA kusikia habari zilizoandikwa kwenye magazeti wiki iliyopita zikieleza kuwa mtu mmoja kajinyonga kwa kutumia fulana ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Huu ni ushahidi kuwa mtu huyo ni maskini kiasi kwamba hana uwezo wa kununua kamba ya katani ya kujinyongea.

Yaelekea bwana yule aliyejinyonga, hana shuka na kwamba usiku yeye hulala bila kuvua hiyo fulana ya njano ya CCM aliyohongwa wakati wa uchaguzi mkuu wa 2010.

Bwana huyo angekuwa na shuka angeitumia kujinyonga kwani shuka, kanga na kitenge vinafaa kujinyongea kuliko fulana.

Kwa watu wenye kujua mambo, namaanisha waelewa, hawashangai wanapotembelea maeneo ya Tanzania yaliyokithiri kwa umaskini kukuta fulana na kofia zinazogawiwa na CCM kama hongo ili wahusika wachague wagombea wa chama hicho tawala.

Utakuta mahakamani, mnadani, sokoni hata kanisani na msikitini na kwingineko watu wamevaa kofia za kapelo za CCM, fulana za njano za CCM na hata skafu za CCM si kwa sababu wanakipenda chama hicho, bali ni kwa sababu hawana nguo nyingine za kuvaa siku hiyo ila hizo walizopewa wakati wa uchaguzi.

Kutokana na hali hiyo fulana na kofia zinazotolewa na chama tawala nyakati za kampeni ndizo maarufu sana katika maeneo maskini katika mikoa ya Morogoro, Tabora, Pwani, Singida, Mtwara, Ruvuma, Lindi na Dodoma.

CCM hushinda kirahisi katika mikoa hiyo kwa sababu hunufaika na umaskini wa wananchi ambao, kwa kutofahamu huona kuwa chama hicho kina upendo (kwa kuwagawia fulana na kofia) badala ya kukilaumu kwa kuwarudisha nyuma kimaendeleo hata wakashindwa kununua nguo.

Kutokana na ukweli huu, CCM haiwezi kuwaletea watu maendeleo kwa sababu maendeleo yatafanya wananchi wasikitegemee chama hicho tawala kwa fulana, kofia na skafu za kuvaa wakati wa sikukuu, kusali makanisani na misikitni na hata sokoni.

Kwa hiyo, si kila anayevaa kofia na fulana ya CCM ni mpenzi, shabiki au mwanachama wa chama tawala bali wengine na ambao kwa kweli ndio wengi hufanya hivyo kwa kukosa mavazi mazuri ya kutokea.

Ushahidi mwingine wa jinsi CCM inavyonufaika na umaskini wa Watanzania ni biashara ya shahada nyakati za uchaguzi. Biashara ya shahada ambapo mabalozi na wenyeviti wa CCM wa mitaa na kata huranda huku na kule kununua shahada hushamiri sana katika maeneo maskini.

Ndiyo maana CCM ambacho ni mtuhumiwa mkuu wa ununuzi wa shahada za kupigia kura mara zote hushinda uchaguzi katika maeneo ambayo wakazi wake ni maskini wa kutupwa kama vile mitaa ya Dar es Salaam iliyojaa wabwia unga.

Siyo siri kwamba biashara ya shahada za kupigia kura haiwezekani Tarime, Arumeru, Mwanza, Shinyanga, Iringa, Mbeya, Arusha, Moshi, Ukerewe au Kasulu, Kibondo na Mpanda. Katika maeneo haya CCM huambulia patupu kwani hakuna wa kuuza shahada ya kupigia kura. Habari nilizopata kutoka Tarime ni kwamba katika uchaguzi mdogo uliofanyika katika jimbo hilo baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wake, Chacha Wangwe, CCM walijaribu kununua shahada wakashindwa baada ya kuombiwa kila shahada Sh 100,000 au kwa chini kabisa Sh. 50,000.

Kwa vyovyote vile, hakuna chama hata kingekuwa na fedha nyingi kiasi gani, hakiwezi kununua shahada kwa shilingi elfu 50, watanunua ngapi!

Najua wapo watu watabisha hili wakidai eti mbona CCM ilishinda Tarime mwaka 2010. Hawa napenda kuwambia kuwa pale Tarime ndugu zetu wa magamba walishinda baada ya kunufaika na mgawanyiko uliotokea baada ya mbunge aliyekuwapo Charles Mwera Nyanguru kujitoa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA) baada ya kutoswa kwenye kura ya maoni.

Mwera alipojiengua alifuatwa huko alikohamia yaani Chama cha Wananchi (CUF) na madiwani watatu na wanachama kadhaa. Lakini huko alipata kura zaidi ya 7,000, CHADEMA zaidi kura 26,000 na CCM wakashinda baada ya kuzoa zaidi ya kura 28,000.

Mwera asingepata tamaa akajiengua, CCM wangetafuta pa kujificha wasipapate.

Pia kuna madai kwamba chama tawala ni maarufu kwa kugawa fedha shilingi elfu mbili mbili, tatutatu au elfu nne nne ili kipigiwe kura iwe kwenye uchaguzi mkuu au uchaguzi mdogo.  Madai haya yanapata nguvu kutokana na ukweli kwamba wapo wana-ccm wamekamatwa wakiuza au kununua shahada za kura.

Mahali ambapo watu wanakabiliwa na umaskini wa kutupwa kama mitaa ya Manzese, Temeke, Kigamboni, Mbagala, Tabata, Mwananyamala na kwingeneko ndiko CCM hushinda lakini mahali ambako hawakabiliwi na umaskini wa kutupwa kama Mbeya, Iringa, Arumeru Tanga CCM haishindi.

Kwa ufupi, CCM inanufaika sana na umaskini wa kutupwa. Bila umaskini wa kutupwa fulana za njano, kofia za kijani na skafu zisingeonekana makanisani na miskitini. Watu wanahudhuria mikutano ya hadhara ya CCM ili kuambulia ‘kiwalo’ tu na si mapenzi na chama.

Pia watu wanahudhuria kwa wingi mikutano ya hadhara ya CCM ili waweze kuambulia shilingi elfu tatu za kununulia unga wa muhogo wakasogeza siku mbele na si kwa kukipenda chama hicho kikongwe cha siasa nchini. Umaskini ni kete kubwa kwa CCM.

Huenda basi, nchi hii haitapata maendeleo kamwe au daima dumu kwa sababu chama kilichopo madarakani hakitaki maendeleo kwani kuleta maendeleo ni sawa na kujipalia makaa. Watu walioendelea na wasiokabiliwa na umaskini watachagua kutokana na utashi wao na si ili wapate fulana au kofia ya kijani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: