CCM inaongoza nchi kwa chuki


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 04 April 2012

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

MATUKIO yanayoonyesha kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaongoza nchi hii kwa chuki ni mengi na yanathibitika.

Moja ya matukio ovu ni lile la mauaji ya watu watatu katika maandamano ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Januari mwaka jana.

CHADEMA waliokuwa wanatumia haki yao ya kikatiba, kupinga kwa njia ya maandamano uchaguzi wa meya wa jiji la Arusha, walipigwa na polisi, walijeruhiwa vibaya na kudhalilishwa wakati wao walikuwa hawajakanyaga hata sisimizi.

Serikali ya CCM, kwa ukatili kabisa, ilitetea mauaji yale hali ambayo imewapa polisi shahada ya juu ya udaktari wa falsafa (PhD) ya kufanya kazi kwa hasira, bila maadili, weledi wala busara.

Hivyo basi, wakitumia shahada ya PhD waliyopewa, tarehe 5 Januari 2011, polisi wakafanya mauaji yale na lugha pekee kwa wafuasi wa chama hicho na hata vingine madhubuti kama Chama cha Wananchi (CUF), kokote walikofanya mikutano na maandamano yao, ni kutembeza kichapo na kudhalilisha wafuasi wao.

Serikali na CCM inabariki hasira za polisi kwa kudai eti maandamano yao yana lengo la kupindua nchi. Uongo huu ni mkongwe kama CCM yenyewe. Uongo kama huo ndio waliutumia Januari 26 na 27 mwaka 2001 pale askari wa vikosi mbalimbali vya ulinzi vya serikali, walipoua wafuasi wa CUF waliokuwa wakiandamana kwa amani kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi mgombea urais wa CCM, Amani Abeid Karume mwaka 2000.

Ukweli katika maandamano yale yaliyofanyika nchi nzima, hakuna duka lililovunjwa, watu waliopigwa au ghala la silaha lililovunjwa na kuporwa. Viongozi wasiojiamini katika utawala wao waliagiza raia wauawe ili watu waishi kwa hofu.

Kwa serikali ya CCM, wafuasi wa vyama vya upinzani si miongoni mwa raia wanaostahili kupewa ulinzi wa polisi. Ulinzi uliopo nchini ni wa wafuasi wa CCM tu.

Katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Igunga, mkoani Tabora, mwaka jana, mfuasi wa CHADEMA alitekwa na wapinzani wao wakubwa kisiasa CCM na akauawa. Polisi hawakujishughulisha kusaka wauaji.

Katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Arumeru Mashariki, kada wa CHADEMA alitekwa akamwagiwa tindikali na wana-CCM. Polisi hawashughuliki. Tukio hilo limetokea siku chache baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kutangazia ulimwengu kuwa watapambana na wafuasi wa CHADEMA.

Matamshi kama haya yakitolewa halafu ukafanyika uhalifu, aliyetoa maneno hayo huwa mtuhumiwa namba moja. Polisi wetu wenye PhD ya hasira na ukosefu wa maadili, weledi na busara wamekaa kimya.

Lakini pale mfuasi wa CCM alipowekwa chini ya ulinzi na wapinzani, polisi wote wa Arusha, tena wakiwa na hasira kali, walikwenda kumwokoa.

Tukio jingine baya na linaloonyesha chama tawala sasa kinaongoza nchi kwa misingi ya chuki ni la kutekwa na kujeruhiwa vibaya Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia; Mbunge wa Ukerewe, Salvatory Machemli na wafuasi wengine. Polisi na serikali hawakulaani tukio lile.

Polisi, ambao hawatamani kuona wafuasi wa vyama vya upinzani wakifurahia mafanikio ya kuimarika kwa vyama vyao waliwatawanya kwa mabomu Songea mjini na Kiwira. Polisi wamekanusha.

Polisi waliokanusha kuua watu walioandamana mjini Songea miezi miwili iliyopita, lakini wakakiri baadaye eti walioandamana walikuwa wahuni, hawawezi kukubali uovu walioufanya Lizaboni, Songea na Kiwira. Akili zao ni kulinda uhai wa wana-CCM tu si wapinzani.

Mtu yeyote akifuatilia matukio ya wafuasi wa upinzani kupigwa, atagundua kuwa polisi huamua kutwanga virungu na risasi wakati raia hao wakifuaria hotuba au matokeo tu. Kwa polisi hawa, wanaotakiwa kufurahia ni CCM basi.

Tatizo la serikali ya CCM ni kuvimbiwa madaraka kiasi cha kushindwa kujua hata maana ya kaulimbiu ya Peoples Power. Hata watoto wadogo wanajua kwamba kaulimbiu hiyo haina maana ya fujo, tafsiri ya fujo inatolewa na dola na CCM.

Kama polisi wanadai intelejensia yao ina uwezo wa kubaini Al-Shabaab wanaowinda mikusanyiko ya wapinzani nchini, lakini intelejensia hiyo ikashindwa kubaini maharamia wa CCM wanaokata kwa mapanga wafuasi wa upinzani, kuna kila dalili CCM inawatuma wafanye fujo.

Haya yote yanafanyika kukipa uhalali chama hiki. Serikali inapodhalilisha upinzani na CCM inapumua.

Serikali ya CCM inawaona wapinzani kuwa ni wahalifu wa kudumu. Katika miaka ya 1990 hadi 2005, CUF ilipokuwa inajihamasisha kwa kaulimbiu ya ngangari, polisi walibuni yao ya ngunguri ili kuvunjavunja upinzani.

Matokeo yake polisi wakasingizia CUF waliingiza mapanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu 2005. Uongo huu uliinufaisha CCM.

Kwa kuwa polisi wana PhD ya kudhalilisha wapinzani, wameshindwa hata kumkamata na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria, kwa wiki tatu sasa, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele aliyepiga ndugu zake na kuwasababishia maumivu makali, wakati wa kikao cha kujadili mirathi. Angefanya hivyo kiongozi wa upinzani serikali ingekodi ndege na kumweka korokoroni.

Kiongozi yeyote anayedai kuna watu wanapandikiza chuki ili nchi hii isitawalike, awe mkweli asijifiche katika kivuli cha uongo. Hakuna gazeti, hata la MwanaHALISI wala chombo chochote cha habari kinachopandikiza chuki ili nchi isitawalike. Vyombo hivi vinaelimisha raia kutambua haki zao.

Hivi kuonyesha madhambi ya serikali ni chuki? Hivi kueleza namna CCM ilivyokengeuka misingi ya utawala bora ni kosa la jinai? Tangu lini CCM ya Mwalimu Julius Nyerere ililala kitanda kimoja na wahujumu uchumi (mafisadi)?

Hivi ni kupandikiza chuki vyombo vya habari vinapofafanua CCM inavyoishi kwa uongo? Tuwaeleze vipi wananchi, CCM ilieleza kwamba mafisadi wa EPA, Richmond, rada na maovu mengine watanyolewa, lakini imewaita, ikapiga nao soga huku ikiwasuka.

Nani alaumiwe, CCM iliyoamua kukumbatia wahalifu na uhalifu au vyombo vya habari vinavyoanika uhalifu huo? Maana kama kukosoa viongozi ni kukosa maadili, chombo chochote cha habari kinachoona uovu lakini kikanyamaza kinafanya kosa la maadili.

Tanzania ni yetu sote. Kama ni jehanamu iwe yetu sote na kama ni pepo iwe yetu sote. Ni utovu wa maadili ya uandishi kupamba tabaka fulani linaloneemeka kwa gharama ya tabaka jingine. Tuifanye Tanzania kuwa pepo yetu sote na si kwa kikundi kidogo cha watu. Madhara ya CCM kuongoza nchi kwa chuki, ndiyo haya sasa inakataliwa kila kona.

0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: