CCM inaringia kikombe cha mateso


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 14 March 2012

Printer-friendly version

UKITAKA kujua raha wanayopata wafuasi wa chama tawala, tazama tabu wanayopata wanachama wa kambi ya upinzani – kupigwa, kujeruhiwa na kuuawa.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetengeneza kikombe hicho cha mateso kwa miaka 20 na inahaha kuhakikisha hakishikwi na upinzani.

Hata Mungu alipowaambia wana wa Israel waondoke Misri, ni Mungu huyo huyo aliyewapa Mafarao wa Misri moyo mgumu. Siku ya mwisho ilipofika Mafarao walipata pigo, jeshi lao liliangamia baharini huku Waisrael wakienda zao.

Ndivyo itakuwa kwa CCM tena katika kipindi ambacho inashikilia kikombe cha mateso. Je, nani aliyekabidhiwa fimbo ya kugawa maji ya kuangamiza CCM?

Mwaka 1995 matumaini yalijengwa kwa chama cha NCCR-Mageuzi. CCM wakawa na moyo mgumu kama Wamiri, waliingiza Usalama wa Taifa wakasambaratisha na kisha wote, isipokuwa Mwenyekiti Augutine Mrema alitimukia TLP ambako usalama wa taifa unaofanya kazi za CCM ulimfuata na kumdhoofisha.

Najua wengi watanipinga, lakini mgogogoro wa Chama cha Wananchi (CUF) wakati huu kikiwa ikulu upande wa Zanzibar kuna mkono wa Usalama wa CCM.

Mwaka jana CCM walimbeba Hamad Rashid aunde kambi ya pili ya upinzani bungeni; lakini Spika Anne Makinda alishtuka. Ghafla Hamad akaota pembe na kutaka kiti cha Katibu Mkuu, wake Maalim Seif.

Akafukuzwa, mara makundi ya wanachama wakaanza kujitoa na kuanzisha chama na wanamkaribisha Hamad. Maana yake nini? Usalama wa CCM utakuwa unatafuta mzizi uliobaki wa upinzani – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Usalama wa CCM hulenga wanachama wachanga kwa kuvumisha kwamba kigogo fulani anataka kurudi CCM au fulani alikuwa na kikao na CCM usiku. Wanachama wachanga wa upinzani na wasiojua kuwa propaganda hizo au uvumi huo ni moja ya silaha za maangamizi za CCM, huamini na kuvunjika moyo.

Pamoja na hayo yote, CCM wanajua wameshikwa pabaya. Wanajua kuwa kasi ya mageuzi ni kubwa na nguvu ya mageuzi haidhibitiki kwa kauli rejareja.

CCM wanaposhindwa kuwabana wapinzani kwa kauli rejareja, huingia katika ghala la ‘silaha’ na kuwatwanga kwa lengo la kuua kwa kisingizio ni wahuni.

  • Wanachama wa mtandao wa wakulima walipoamua kumpongeza rais ikulu, polisi waliwasindikiza wapite kwa amani.
  • Wakulima wa korosho wa mikoa ya Lindi na Mtwara waliapoamua kuandamana kulaani serikali kufungia wanunuzi wa korosho bila kutoa njia mbadala, polisi hawakufanya kazi ya kulinda maandamano yao isipokuwa kupiga na kutawanya kwa madai ni wahuni.

Kwa hiyo, hapa ni rahisi tu kujua ni nani anatoa amri kwamba yule asindikizwe na polisi na yule akong’otwe na polisi haohao.

Kuandamana kudai haki mazao kununuliwa ni kosa kwa serikali hii; na kuandamana kudai haki ya kulindwa kama walivyofanya Songea ni kosa kubwa kuliko uhaini. Watuhumiwa wa uhaini wa mwaka 1983 walikamatwa, wakashtakiwa; walioshinda waliachiwa huru na wengine walifungwa.

Miaka takriban 30 tangu kesi hiyo itoe mwanga kuwa si kila mtuhumiwa ana hatia, CCM inawaona watu wote wanaoandamana kuwa wana hatia na adhabu yao ni kuuawa.

Hivyo ndivyo ilivyofanya serikali ya CCM Songea, Dodoma, Arusha na Mbeya ambako lilitumika Jeshi la Wananchi. CCM inasema kila anayeandamana ni mhuni na ili kudhibiti ni kuua. Halafu kesho yake viongozi wa CCM wanatoa kauli kupongeza serikali kuua – mshikamano wa uhalifu.

Serikali hiihii inasema kila mtu hana hatia isipokuwa mbele ya sheria, lakini polisi wakitumwa kukandamiza upinzani, hujipa haki ya kuua. Serikali inaua inaowaita wahuni lakini inafunga wezi wa kuku. Serikali inaua wahuni, lakini wahaini wanashtakiwa.

Hili litawasaidia. Mshikamano wa uhalifu haukuanza leo ndani ya CCM. Kilichomfanya Mrema ajiuzulu vyeo vya naibu waziri mkuu na waziri wa kazi na ajira mwaka 1995 ilikuwa kukataa kuwa sehemu ya fungamano la uhalifu.

Alipinga ndani ya Baraza la Mawaziri wizi wa mabilioni ya shilingi yaliyotolewa kwa ajili ya kufufua zao la mkonge. Badala yake akapewa mtu mmoja VG Chavda akala.

Mrema alijitoa na akajaribu kuwaeleza wananchi wizi unaofanywa na serikali yao. Lakini kwa vile uelewa wa wananchi ni mdogo (juzi, jana na leo), wakaja kuamini madai ya serikali eti Mrema alijiondoa kwa sababu ya uroho wa madaraka.

Hata katika mgomo wa madaktari Februari mwaka huu, serikali ikadai haijui kama kiongozi wa mgomo ule Dk. Stephen Ulimboka alifaulu. Yaani Muhimbili isomeshe, imwajiri halafu serikali inasema hawajui kama alifaulu.

Serikali, kwa miaka mingi imewafanya watu waamini uongo na uzushi wake badala ya ukweli uliowekwa wazi. Haya yote ni mambo ambayo hayajatumiwa ipasavyo na wananchi kuiadhibu CCM.

Watanzania walipoteza fursa muhimu ya kuiwajibisha CCM kwa ufisadi uliofichuliwa na Mrema mwaka 1995 na madhara ya kupuuza uoza wa serikali ya CCM, mwaka 2005 fedha za wizi wa EPA zimekuja kutumika kuingiza watu madarakani. Ndiyo maana:

Tunashuhudia ufisadi ukishamiri na watoa taarifa wanakong’otwa; majina ya wauza unga hayafanyiwi kazi japo yalipelekwaa na kuhifadhiwa kwenye mashubaka ikulu.

Watuhumiwa ufisadi wanaitwa ikulu na wanapigiwa magoti warejeshe fedha walizoiba; na waliopatikana kwa makosa ya rushwa ndio wanapitishwa na chama kuwania ubunge.

Watuhumiwa ufisadi kupitia Richmond sasa wanataka kusafishwa; halafu mwana CCM mwenye namba 0757032733 anaona raha kusema, “Tumwogope Mungu, hakuna msafi chini ya jua. Nchi ni yetu kwani rais kupewa suti tano ni ajabu?”

Hapo ndipo tulipofika; wana CCM hawaoni ubaya mkuu wa nchi kuingia katika tope la rushwa. Kwa hiyo, wapinzani wanapowafumbua macho wananchi wa aina hii kwamba nchi hii inaliwa na waliopewa madaraka, wanafurahia polisi wakitumwa kupiga na kuua kwa madai ni wahuni.

CCM inaongoza wanachama wa CCM na wahuni – kwamba kama huko CCM wewe ni mhuni.

CCM inakandamiiza haki za msingi za raia kwa kisingizio cha maneno ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwamba “bila CCM imara nchi itayumba”

Ile ndiyo ilikuwa kete ya mwisho ya Mwalimu kuiokoa CCM mwaka 1995 kwa vile alishaona inazolewa na wimbi la mageuzi.

Jiulizeni, mbona Zambia haikuyumba UNIP ya Kenneth Kaunda ilipoondolewa? Mbona Kenya haikuyumba KANU ya Jomo Kenyatta na baadaye Daniel arap Moi ilipoondolewa? Mbona UPC ya Milton Obote ilipoondolewa na baadaye serikali ya CCM kuwasaidia kina Yoweri Musevuni Uganda kuna utulivu mkubwa? Kwanini nongwa iwe kwa Tanzania?

CCM inafuata sera za Chamama cha Kikomunisti cha China (CPC) ambacho kimeweka utaratibu kwa vyama vya upinzani. Kwa hiyo vyama vya upinzani vinafanya kazi chini ya maelekezo ya CPC na hicho ndicho CCM inataka. Lakini fimbo yao inakuja.

0789 383 979
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: