CCM isiporejea asili itajuta -Nkumba


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 08 February 2012

Printer-friendly version

MBUNGE wa Sikonge, Saidi Juma Nkumba ni mmoja wa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaokiri chama chao kimepoteza asili yake.

Nkumba, aliyeingia bungeni kipindi cha tatu mfululizo mwaka 2010, anasema, “CCM lazima irejee kwenye misingi yake ya asili.”

Anaitaja misingi hiyo kuwa ni kutetea wanyonge ambao amesema kuwa kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakilalamika kuachwa solemba.

Kwa sababu hiyo, anaonya iwapo chama hicho hakitarudi kwenye asili yake hiyo, itakapofika 2015, mwaka wa uchaguzi mkuu mwingine, “kinaweza kupata majuto yasiyo na kifani.”

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Nkumba amesema chama hicho kilianzishwa kwa kaulimbiu ya kuondoa shida za wafanyakazi na wakulima lakini hali ya mambo imebadilika.

Anasema kwa masikitiko kwamba CCM sasa kimezama katika kukumbatia matajiri hatua inayoleta picha mbaya kwa “wale waliolengwa kukombolewa kimaisha.”

Nkumba ni mmoja wa wabunge wachache nchini wanaoishi kwenye majimbo walikopigiwa kura. Anaishi kijiji cha More, kilichoko kilomita 30 kutoka Sikonge mjini.

Katika hili, anasema yeye haamini katika uongozi wa remote control.

“Mimi ni mwana Sikonge kindakindaki. Mazingira yake nayafahamu vema, makazi yangu yako huko. Nafuga na kulima huko pamoja nao nasimamia maendeleo yao nikiwa na wananchi.

“…Ndiyo maana hata huwezi kusikia vita ya wakulima na wafugaji ikipamba moto. Inapotokea mivutano, huwa nasimama katikati na serikali kutoa haki,” anasema.

Zaidi ya hapo, Nkumba anasema huko Sikonge ambako kuna makao makuu ya wilaya, CCM imejikita zaidi kwa kufuata misingi ya uanzishwaji wake hivyo upinzani kupoteza mwelekeo.

Pamoja na kujivuna kuwa karibu na wananchi, kuna tuhuma kuwa ubunge wake ulikuwa na nguvu ya Rostam Aziz, mbunge wa zamani wa Igunga na kada wa CCM mwenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya chama.

Nkumba anabeza tuhuma hizo. “Nimewahi kusikia madai hayo eti nilifadhiliwa na Rostam, lakini siri ya ushindi wangu ni heshima ya chama changu iliyojengeka Sikonge. Nasema waziwazi sikufadhiliwa kuwa mbunge.”

“Sina ufadhili wowote. Sina kundi eti la kutaka kuendelea au kutoendelea kuwa mbunge au kushika nafasi fulani ya uongozi. Wananchi wa Sikonge na Tabora ndio wanaojua nafanya nao kazi vipi na mrejesho wanauona.”

Anatamba kuwa watu wa Sikonge wanahitaji mtu aliye karibu nao kwa ajili ya kusaidiana kuharakisha maendeleo. Anasema, “Ndiyo maana wakubwa wanaoishi sehemu nyingine wanashindwa wanapokuja Sikonge.”

Nkumba kitaaluma ni mwalimu. Ameanza uongozi tangu ngazi ya wilaya ambako amekuwa mjumbe wa mkutano mkuu.

Mbunge huyo anasema wilaya ya Sikonge ilianzishwa mwaka 1995 wakati Urambo, wilaya jirani, ilianzishwa mwaka 1975.

Anataja matunda ya kujikomboa akianzia na umeme. Anasema Sikonge ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata umeme mwaka 2003. “Umeme ulichochea harakati za maendeleo Sikonge; ulizalisha ajira nyingi kwa vijana,” anasema.

Alipotwaa kiti cha ubunge jimbo la Sikonge lilikuwa na shule tatu tu za sekondari ikiwemo inayomilikiwa na Shirika la kidini la Moravian.

Akiitaja sekondari ya Ngulu, Nkumba anasema ndiyo shule ambayo viongozi kadhaa wa ngazi ya juu serikalini walisoma.

Wanaotajwa kunufaika nayo ni Samwel Sitta ambaye ni Waziri wa Afrika Mashariki na spika wa zamani. Mwingine ni Profesa Juma Kapuya, mbunge wa Urambo Magharibi.

“Ngulu inafanyiwa mabadiliko. Itakuwa sekondari kwa ajili ya kidato cha tano na sita tu maana sasa kila kata ina sekondari. Tuna kata 17 wilayani Sikonge.”

Shule za msingi zipo 83; kila kijiji kina shule yake. Amekiri kuwa tatizo la uhaba wa walimu, nyumba zao na vifaa linazidi kukua.

Maendeleo mengine aliyochangia kuyafanikisha ni kiwango kikubwa ikiwa ni pamoja na barabara kuu itokayo Tabora kupitia Sikonge, Ipole, Mpanda, Rungwa mpaka Mbeya.

“Barabara hii tayari imetengewa bajeti ya kuwekwa lami kwa urefu wa kilomita 71 kutoka Tabora hadi Sikonge, kabla ya kumalizia kilomita 26 kutoka Sikonge hadi Ipole,” anasema huku akitambia barabara mbili kupandishwa hadhi kutoka halmashauri kuwa za mkoa.

Barabara hizo ni kutoka mji mdogo wa Tutuo, Ubumba, Izimbili hadi Usaka. Nyingine ni Sikonge, Mibono mpaka Kipili ambazo zitafunguliwa wakati wowote.

Nkumba anajua tatizo la uhaba wa maji yatokayo mto Utyatya. Anasema kuna mpango wa kujenga bwawa la Ulianyama linalochimbwa kabla ya serikali kuombwa fedha za kusambaza mabomba ya kugawa maji hayo.

Kuhusu kilimo, Nkumba anasema wilaya yao ndiyo ya kwanza kupata mbolea ya ruzuku kutoka serikalini. “Upatikanaji wa ruzuku uliongeza uzalishaji wa mazao ya chakula kama mahindi, maharage kama mazao ya chakula, na tumbaku ambalo ni zao la biashara.”

Nkumba anachukia makada wenzake wa CCM wanaopanga mikakati ya kusaka urais kwa sasa akisema, “Sijamsikia hata mmoja akitamka hadharani kama anataka.”

Hapendi mtindo ulioibuka wa wana-CCM wenzake wa kuota urais ingali mapema.

“Mimi ninavyojua urais ni mamlaka ya wananchi. Mtu kutafuta urais inataka dhamira ya kweli. Kwanza ajipime anazo sifa za urais,” anasema.

Nkumba anahofia makada wanaotumia fedha nyingi kutafuta uongozi. Anasema, “wanasiasa wanaoshiriki vikao vya harambee katika makanisa ni wa kuogopwa.

“Si kila mwenye fedha hafai kuwa kiongozi, lakini yule anayetumia fedha zake kuwa kiongozi wa ngazi yoyote ile katika chama au serikali, huyo ni wa kuogopwa,” anasema.

Saidi Juma Nkumba alizaliwa 17 Aprili 1962 katika kijiji cha More, wilayani Sikonge.

Alisoma shule ya msingi Uhuru (zamani Aga Khan) na kumalizia shule ya Isike 1981. Alichaguliwa kujiunga sekondari ya Moshi Tech ambako alihitimu mwaka 1985.

Alijiunga na Chuo cha Ualimu Bunda na alipomaliza mwaka 1987 kwa kuhitimu kozi ya diploma, alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria. Mwaka 1990 aliajiriwa kama mwalimu na kupangiwa shule ya msingi Sengerema, mkoani Mwanza.

Mwaka 1993 alihamishiwa Tabora alikofundisha shule za Imaramihayo, Ugowola alikoanza kuwa mwalimu mkuu, Kigwa, Mbirani. Nkumba, muumini wa dini ya Kiislamu, ana wake watatu na watoto wanne.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: