CCM isitumie dola vibaya


editor's picture

Na editor - Imechapwa 09 March 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinatapatapa. Hili Mwalimu Nyerere aliliona kabla hajaenda London na kufia huko mwaka 1999.

Aliwahi kusema ametoshwa na CCM kutokana na mwenendo mbaya wa viongozi wake wakuu. Wanadharau maoni ya wananchi; na akaahidi anaweza kukiacha ingawa ndiye muasisi na mtu aliyetumia sehemu kubwa ya uhai wake kukijenga.

Mwalimu alitamka hadharani kwamba chama kisichozingatia maoni ya wananchi, kitapotea tu. Hapo ndipo hasa ilipo CCM. Ilianza na sasa inaingia nchani katika kupotea. Si chama cha wakulima na wakwezi.

Horace Kolimba, alipokuwa katibu mkuu wa CCM, alisema chama kimepoteza dira. Ingawa aliwashiwa moto na ukamdhuru, yaliyokuja baada ya hapo na yanayoendelea kukisibu chama hiki, yanathibitisha aliyoyasema Mwalimu Nyerere na Kolimba.

Chama hiki hakina tena wapiganaji mahiri. Bali kinao wapenda mabavu. Zile jumuiya zilizozoeleka kukisaidia, zenyewe zimeathirika na kinachotokea ndani ya CCM. Ni kwa kuwa viongozi waandamizi wa jumuiya ni pia wajumbe wa vikao vya juu vya chama. Walewale, hata wawe vijana au wakongwe. Ni walewale.

Sasa hakina mbinu za kisayansi za kukabiliana na matatizo ya wananchi. Sera zake zimegonga mwamba. Kilishindwa kuhimili matatizo ya wanachama wake; hakina ujanja wa kushinda nyoyo za Watanzania walio wengi. Huku ni kupotea.

Kilichobaki ni matumizi mabaya ya serikali. Kinategemea dola kuishi. Kinaomba huruma kila kinapofikwa na wajibu wa kujibu hoja. Masikini CCM. Na hii ni hatari. Chama tawala kuchungulia kaburi ni hatari. Lakini tufanyeje?

Tumejaribu kushauri viongozi wake wajirudi ili wakirudishe chama chao kwenye mstari, tukabezwa. Tukatishiwa maisha. Vile kukikosoa kwa hili na lile, ina maana kushinikiza wajirekebishe. Wakapuuza.

Leo, wanasingizia wasiohusika. Wanadai amani na hatari ya kuivunja. Wanasahau amani hudumu kwa haki kustawi. Tunaona ilivyo kazi ngumu kuipata haki Tanzania. Hili kila mtu analijua.

Woga mtupu. Walisema mwisho wa uchaguzi ndio mwanzo wa maandalizi ya uchaguzi ujao. Wao wanajiandaa, hawataki wengine wajiandae, bali walale. hatujawahi kusikia wanasiasa wanalala ndani ya njaa na umasikini.

Dawa hatuioni isipokuwa CCM itatue haraka shida za watu – wafanyakazi, wakulima, wavuvi, wafugaji, wenye viwanda, wasafirishaji, wawekezaji. Kutuma dola ifyatuke; kupiga na kutisha watu na wanasiasa pinzani, ni kupotea.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: