CCM itaazima wapi shoka lenye makali?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 11 August 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

UKIMSIKILIZA Yusuf Makamba, katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kauli zake kuhusu tuhuma za rushwa katika mchakato wa kura za maoni za ubunge na udiwani ndani ya chama hicho, huwezi kukwepa kujenga hisia kwamba huenda anafunulia umma kujiandaa kwa hitimisho moja juu ya tuhuma hizi. Funika kombe mwanaharamu apite!

Kauli kama ‘kila mmoja alitoa rushwa, ila walizidiana dau” au ‘hatuwezi kuwahukumu watu bila kupata uthibitisho’ au ‘malalamiko ya walioshindwa kura kwamba rushwa ilikithiri ni visingizo vya mbaazi zikikosa maua husingizia jua’ zinazotoa mwelekeo mmoja; rushwa si lolote wala chochote ndani ya mchakato huo, wote walitoa na kifo cha wengi ni harusi.

Ingawa kuna jambo la kwanza, ambalo linapaswa kuwekwa wazi juu ya tuhuma dhidi ya yeyote, kwamba katika taifa letu, kila mtuhumiwa ni kiumbe asiye na hatia hadi atakapotiwa hatiani na mahakama, kuna mambo mengine katika jamii yanahitaji kafara kubwa zaidi ili kuponya wengi.

Kwa maana hiyo, tunaposema kwamba kuna rushwa ilitembea ndani ya mchakato wa kura za maoni za CCM, na hata pale Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ilipokamata watuhumiwa ama wakitoa au kugawa au kuandaa mazingira ya rushwa, bado kamata hiyo kisheria haiwezi kuthibitika bila kwanza kwenda mahakamani. Lakini je, kupona kwa taifa kunategemea mahakama tu? Je, hatua za kiutawala, kikanuni na kimazingira nazo hazifai?

Hali hii ilifungamanishwa na mfumo mzima wa kuendesha mashitaka katika nchi hii ili sasa hawa waliokamatwa na Takukuru watiwe hatiani kwa maana ya ‘kuthibitika’ kama anavyotaka Makamaba ni sawa na kutarajia yasiyokuwepo na ambayo labda hayatatokea kabisa.

Ni kweli mashitaka dhidi yao yanaweza kuundwa na wao kufikishwa mahakamani, kesi zao zikasomwa, kesi zikasikilizwa kwa kuwasilisha ushahidi na vielelezo mbalimbali ili mahakama sasa iamue kama kweli uhalifu wa rushwa ulitendaka au la. Lakini ni kwa jinsi gani basi mchakato huo wa kimahakama utaepusha watu wachafu kushika ofisi za umma za kuchaguliwa kwenye udiwani na ubunge?

Kwa kutambua uwezo wa mahakama zetu, na kwa kutambua kasi ya kuendesha kesi hizo, ni dhahiri miaka mitano inaweza kuwa michache kwa kesi hizo kumalizika na mtu ajulikane kuwa ni mtoa rushwa au la. Yaani athibitike kwa msimamo wa Makamba.

Ni katika mazingira kama hayo, ingawa kwa sasa kuna baadhi ya makada wa CCM wanakabiliwa na kesi za jinai mahakamani, bado wanahesabika kuwa ni watu safi, na wamejitosa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge na udiwani, na CCM haina tatizo lolote katika hilo kwani wapo wengine ambao wana tuhuma nzito zaidi na ni wajumbe wa kamati kuu na wanatumainiwa katika kukisaidia chama hicho kijisafishe!

Sasa anapoibuka Makamba na kauli zake za kutaka ‘uthibitisho’ ili watu wawajibishwe, wenye akili zao wanajua wazi kwamba ni muhali kwa CCM kuwawajibisha watoa rushwa katika uchaguzi. Na kama ikifanyika itakuwa ni kwa mtindo ule ule wa ‘kufanyiziana’ maarufu kama mizengwe.

Naomba kurejea nyuma kidogo. Kuna wabunge waliomaliza muda wao katika Bunge la tisa (2005-2010) waliothibitika kwa vielelezo kuwa wana vyeti vya kughushi kuhusu elimu yao, wengine wanatumia majina yasiyokuwa yao kwa maana ya kutumia sifa za kielimu za watu wengine kupata ubunge; lakini wote hawa taarifa zilipopelekwa mbele ya Bunge na hata pale viongozi wenye nafasi ya kuchukua maamuzi, hakuna kilichofanyika, kulindana kama jadi!

Hakuna mwalimu mzuri kama historia; inatukumbusha tulikotoka, tulifanya nini, wapi tulikosea na wapi tulipatia, hutupa mwanga wa kutambua uwezekano wa matokeo ya jambo fulani mbele ya safari; ni kwa kumtambua mwalimu huyu ni rahisi kuhitimisha mambo ya mbele ya safari.

Kwa kumtumia mwalimu historia, si uchimvi wala uchuro kusema kungali mapema kwamba kazi iliyofanywa na Takukuru kwenye kura za maoni kwa CCM si jambo la kuwanyima usingizi. Ni aina nyingine ya juhudi za kutaka kuaminisha jamii kwamba kuna vita ya kuwashughulikia waliotoa rushwa, lakini ndani ya mioyo yao huo ndio utaratibu uliokubalika.

Katika safu hii hivi karibuni nilihoji inakuwaje wabunge wanahakikisha wanalipwa kiinua mgongo chao hata kabla ya Bunge kuvunjwa kisheria? Kwa nini wahakikishe wanalipwa mapema? Jibu ni ili kujihakikishia uwezo wa kifedha wa kuingia kwenye mchakato wa kura za maoni.

Kwa bahati mbaya, kile wanachotaka CCM ndicho kinatokea katika nchi hii. Bunge ni la CCM kwa maana kwamba wamejaa zaidi ya asilimia 80, Spika Samuel Sitta ni kada wao, na serikali iliyoko madarakani ni ya CCM. Kwa hiyo, CCM ilitaka na kuagiza kwamba fedha hizo zipatikane mapema kwa ajili ya kufanikisha mchakato wa kura ya maoni.

Mipango, nia na matendo ya wagombea wa CCM katika mchakato wa kura za maoni wameonyesha dhahiri kwamba kuhongana si jambo la bahati mbaya, ndiyo sera kimatendo, ndio mwelekeo na nia ya kudai mafao mapema kabla hata Bunge kuvunjwa; ndiyo hakikisho pekee la kushinda kura. Bila hongo hakuna anayeamini kwamba atashinda.

Makamba amethibitisha kwa kauli isiyokuwa na ukakasi wowote kwamba “kila mmoja alihonga, walizidiana tu dau.” Kama hiyo ndiyo imani ya katibu mkuu wa CCM, mtendaji mkuu wa chama tawala, nani basi anaweza kusimama kama mgombea msafi ndani ya CCM?

Je, kauli hii si ni uthibitisho kwamba hakuna wa kutupwa, hakuna wa kuenguliwa, hakuna wa kulaumiwa kwa kuwa wote walicheza mchezo mmoja, rafu za kufanana? Kilicholeta fadhaa ni ‘kuzidiana kete’ lakini kila mmoja alisukuma kete hiyo hiyo ya rushwa.

Kwa maana hii, umma usijisumbue kwamba eti CCM wana mpango wa kushughulika na yeyote kati ya hao waliokamatwa na Takukuru, kwa sababu kuhongana ni mchezo unaokubalika ndani ya chama. Na kama watu watashikilia bango wakitaka kuona hatua zikichukuliwa, basi wataombwa wasubiri kesi zifike mahakamani ili uthibitisho anaoutaka Makamba upatikane. Hii yaweza kuwa ni baada ya miaka mitano na ushei ijayo!

Wakati huo ukiwa ndio ukweli wa maamuzi yatakayofikiwa na vikao vya juu vya CCM mwishoni mwa wiki hii, pengine wengi watabaki na bumbuwazi kwamba sasa mwelekeo wa nchi hii katika kupambana na rushwa ni upi kama chama tawala kinafunika na kukubali uchafu kama huu? Hili ni swali litakalobakia bila majibu hadi hapo CCM itakapokataa na kuikana rushwa kwa udhati wa moyo.

Mpaka hapo uswahiba, kulindana, usanii na kila aina ya mbinu za kufunika ukweli zitakapoachwa; ni mpaka hapo dhana ya cheo ni dhamana itakapotambuliwa na kuenziwa; ni hadi hapo uwajibikaji na kuwajibishwa vitakapokuwa moja ya silaha za kulinda na kuenzi ofisi za umma; ni hadi hapo tutakaporejesha misingi ya kupata uongozi kwamba ni kutakiwa na watu na si kuwanunua watu.

Ni hadi hapo tutakapokomaa kiasi cha kutosha na kuamini kwamba tuhuma pekee zinatosha kumweka mtu kando akisubiri uthibitisho wa Makamba, ili pamoja na mambo mengine tuhuma zake zisiamshe taharuki mbaya ya kisiasa ndani ya jamii.

Hatutaki kufika hatua ya jamii kuasi, tunaweza kutengeneza mambo, na njia nzuri ya kuanza ni sasa, hebu tuone basi shoka lenye makali likishuka juu ya wote waliohonga kura za maoni!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: