CCM JANA NA LEO: Acha tu, kitanda hakizai haramu


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 25 January 2011

Printer-friendly version

WIKI mbili zijazo, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitatimiza miaka 34 tangu kuzaliwa. Huu ni uzao wa muungano wa vyama vya Tanganyika African National Union (TANU na Afro Shirizi Party (ASP).

Baada ya miaka 34 sasa, bila shaka yoyote, naweza kusema kuwa mtoto CCM hafanani na wazazi wake. Bali kwa kuwa kitanda hakizai haramu, tunakubaliana na hali tusiyoweza kuibadilisha.

Umri wa miaka 34 ni wa mtu mzima na kiukweli, wanachama karibu wote wa umoja wa vijana wa chama hicho (UV-CCM), hawakuwepo wakati CCM kinazaliwa 7 Julai 1977.

Wanaosoma historia na kuandika mitihani katika somo la uraia, wanafahamu kuhusu kuzaliwa kwa chama hicho na yaliyojiri wakati ule.

Wale tuliobahatika kuwa wanachama wa TANU Youth League (Umoja wa Vijana wa TANU) na hatimaye UV-CCM kabla umri haujatuacha, tunapatwa na kihoro kila tunaposikia umoja huo ukitamka chochote hadharani kuhusiana na hali ya siasa ya taifa letu kwa sasa.

Hii ni kwa sababu kwanza, wanachelewa mno kuchukua nafasi yao. Pili, hata wanapochukua nafasi yao kwa kuchelewa wanapwaya.Tatu, wanaonekana wazi kuwa na bei inayofahamika kirahisi.

Kwa kuwa sasa taifa limegeuka kuwa  la “Jamhuri ya Muungano ya Matamko,” UV-CCM nao wameibuka wiki iliyopita na tamko lililosheheni masuala kadhaa ya kitaifa.

Kama ilivyo ada, ni rahisi kubaini mara moja kwa nini walisemea hayo na kuacha mengine. Kwa mfano, ni rahisi sana kubaini kwa nini UV-CCM walijikita katika suala la Dowans, mgongano wa kauli za mawaziri na suala zima la bodi ya mikopo.

CCM iliyogawanyika kwenye msingi, haiwezi kupona kugawanyika kwenye matawi – vijana na jumuia nyingine. Tamko la UV-CCM linaonyesha wazi mgawanyiko huo ulio katika chama mama.

Tamko lile halikuwa na kauli juu ya haja ya kuandika katiba mpya, hali mbaya ya uchumi na mfumuko wa bei; vilevile halikugusia maandalizi ya taifa katika kuadhimisha miaka 50 ya uhuru.

Ninapoyataja haya ambayo hayakutajwa na tamko la UV-CCM, si nia yangu kuwachagulia mambo ya kuzungumzia, bali nalenga kuonyesha dalili za ukame wa fikra pevu katika jumuia hii ambayo tangu mwanzo ilikuwa ni tishio kwa chama chenyewe kwa jinsi ilivyokuwa imebobea katika uzalendo.

Baadhi yetu tunapopita hata mbele ya jengo la makao makuu ya UV-CCM tunazongwa na simamzi maana mahali pale kilikuwa ni kituo kilichosheheni fikra na katika hili, kiliheshimika ndani na nje ya nchi.

Jumuia ile ilikuwa na wawakilishi hata nje ya nchi kama Algeria, Addis Ababa na katika nchi zote za ukombozi Kusini mwa Afrika. Siku hizi hata ofisi za mikoa za jumuia hii si rahisi kuzibaini unapofika katika ofisi za CCM za mikoa.

Lakini kubwa ni hili: Tamko la UV-CCM lilimjadili Dk. Willibrod Slaa, katibu mkuu wa Chadema, kuwa ni mtu hatari kwa taifa hili. Tamko likawaonya Watanzania wajihadhari sana naye pamoja na chama chake.

Hatari ya Dk. Slaa ikaelezwa kuwa ni kwa vile “ameiba” mke wa mtu na kuishi naye hata baada ya kufikishwa mahakamani.

Vijana “wasomi,” viongozi wa jumuia muhimu ya CCM, wakatumia muda wao mwingi kuona na kujadili hatari ya taifa letu kuwa inaletwa na Dk. Slaa kwa sababu tu ya tuhuma kwamba “kaiba mke wa mtu.”
 
Hii ni propaganda chafu kwa maana kuwa haina tija kwa CCM, kwa taifa na wala kwa Dk. Slaa na chama chake. Propoganda hutumika ili kumnufaisha anayeipiga au kuinufaisha jamii; lakini kwa sasa hakuna mwananchi anayeamini kuwa Dk. Slaa ni mtu hatari kwa taifa.

Niliwahi kusema huko nyuma, Dk. Slaa anahitajika CCM kuliko hata anavyohitajika ndani ya Chadema. Kwa hiyo propaganda ya UV-CCM ni ya hatari kwa CCM kuliko ilivyo kwa Dk. Slaa.

Wakati wa harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika, masuala ya propaganda yaliachwa kwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na idara ya propaganda ya chama.

Kwa kufanya hivyo, sisi wana TANU Youth League na baadaye UV-CCM tulipata muda wa kuchambua masuala ya msingi kwa uyakinifu unaohitajika.

Haikutokea hata siku moja makada wa chama au jumuia yake, kupoteza muda katika kucheza na zipu za makaburu au hata kujifanya tunahesabu vizibo vya chupa za bia wanazokunywa ili tupate cha kuandika katika makala mbalimbali za majarida ya siasa ya wakati huo.

Hatua hii mpya ya UV-CCM kujiingiza katika propaganda nyepesi inaishushia hadhi jumuia na kimsingi UV-CCM; inasababisha watu wasiichukulie kwa uzito unaotakiwa. Hii ndiyo sababu hata CCM inaipuuza jumuia yake.

Angalia sasa, UV-CCM wanasema Dowans isilipwe, lakini hata kabla ya kauli yao haijafika chini, Kamati Kuu (CC) inasema Dowans ilipwe.

Ikiwa suala la maisha binafsi ya Dk. Slaa linakuwa ajenda katika kikao cha baraza la utekelezaji la vijana, ni wazi basi ilikuwa hivyo pia ndani ya CC. Ndiyo maana CC imekuja na tamko la kubariki chote kilichosemwa na vijana wake.

Sasa tujiulize, katika utitiri wa matatizo yanayokikabili CCM, masuala binafsi ya Dk. Slaa yana uzito na nafasi gani katika vipaumbele vya chama hicho na jumuia zake?

Inatia shaka wanaume wazima na wanawake katika CC ya chama kujadili masuala ya ndani ya shuka za watu kana kwamba wao hawana masuala ya ndani ya mashuka yao.

Hali kadhalika, ni kukosa adabu kwa kiwango cha juu, vijana wale wa UV-CCM ambao wengi wao wana umri sawa na watoto wa Dk. Slaa, kuanza kujadili habari za maisha yake binafsi.

Lakini shaka inakuwa kubwa zaidi pale ambapo karibu wote waliozungumza, pamoja na wale waliowatuma, wakiwa ni walewale wanaokabiliwa na tuhuma lukuki za ngono, nyingine zikiwahusu hata wasaidizi wao na wafanyakazi wao wa ndani.

Baadhi yao hawaaminiki hata kuachiwa watoto waliowazaa wao wenyewe.

Tabia hii ndiyo imekifikisha CCM katika hali mbaya kiliyo nayo sasa, baada ya vijana wadogo kama Martine Shigela, Mary Chatanda, Amos Makalla, Ridhiwani Kikwete na Nape Nnauye kuanza kujibizana na wazee wenye heshima kama akina John Malecela, Joseph Warioba na hata viongozi wa dini wakiwamo masheikh na maaskofu.

Tabia hii ya kujadili zipu za watu badala ya kujadili masuala ni dalili ya tatizo kubwa na zito ndani ya CCM.

Hivi sasa taifa limeachwa yatima na halina kiongozi (auto piloting), lakini hakuna anayediriki kuhoji ndani ya chama kwa hofu ya kujadiliwa zipu yake.

Mwandishi wa makala hii, amejitambulisha kuwa msomaji wa MwanaHALISI na kiongozi mwandamizi ndani ya Chama Cha Mapinduzi ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa – UV-CCM.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: