CCM kimbilio la hata wahalifu wadogowadogo


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 22 July 2008

Printer-friendly version

'UKITAKA mambo yako yaende vyema ingia CCM,' alisema Waziri Mkuu wa Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye kwenye mkutano wa hadhara mkoani Singida mwaka 1997.

Pana ujumbe mahsusi, mzito na wenye dhamira makini unaolenga wafanyabiashara na Watanzania wengine wanaotafuta manufaa au ahueni fulani kutokana na matatizo yanayowakabili.

Inaeleweka wakishafanikiwa kibiashara, raia hawa ndio wachangiaji wakubwa wa fedha kwa CCM.

Nenda popote nchini. Tembelea miji mikubwa mikoani na wilayani. Ni nadra sana kukuta mfanyabiashara mkubwa asiyekumbatia CCM. Wengine wanajionyesha wazi wengine wanajificha.

Mfanyabiashara kuwa mfuasi wa chama tawala si dhambi wala jinai kwa sababu endapo chama hicho kitapoteza dola kwa kupokonywa na chama kingine, yumkini baada ya muda, watahamia bila ya taabu yoyote chama kitakachokuwa kimeingia. Lakini siyo akumbatie upinzani, huyu atasumbuliwa na kufuatwafuatwa kila wakati hadi biashara yake ife.

Nchini Zambia, wafanyabiashara wengi wakubwa waliokumbatia Chama cha UNIP wakati wa utawala wa Kenneth Kaunda, sasa wanakumbatia Chama cha MMD cha Rais Levy Mwanawasa.

Isipokuwa maovu hutokea iwapo mahusiano yao yatakwenda kinyume cha taratibu za halali za ufuasi wa vyama. Na matokeo yake ni kuzuka ufisadi katika ngazi za juu, hali inayosababishwa na uhusiano wa karibu mno kati yao na wakuu wa serikali. Ukwepaji wa kodi, zabuni zilizozidishwa bei, mikataba mibovu inayohujumu taifa na kadhalika.

Hata wafanyabiashara wadogo nao wameingia katika kutafuta kinga ya chama tawala katika shughuli zao zikiwemo zilizo chafu. Ila mara nyingi vyombo vya dola huwa haviwajali sana. Katika mtaa ninaokaa, kuna nyumba moja iliyokuwa inapepea bendera ya CCM ambayo ilivamiwa na polisi kwa kudaiwa mkiuzwa gongo.

Na wakati wa bomoabomoa ya vibanda vya biashara katikati ya jiji mwaka juzi, baadhi yake vilikuwa vinapepea bendera ya CCM ili viogopwe. Mtu anayedhamiria kupora kiwanja au eneo lililokatazwa utamkuta ametundika bendera ya CCM ili asibughudhiwe na mamlaka husika.

Haya yote yameanzia ulipokuja mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Wakati wa enzi ya utawala wa chama kimoja, wafanyabiashara wakubwa hawakuwa wanakitetemekea sana chama tawala. Ingawa walitakiwa kuwa wanachama kwanza ili kupata leseni, baadhi yao walikuwa wanakataa kutoa michango kwacho wala serikali na hawakuguswa.

Katika siasa za ushindani, ushindani wa kisiasa na kibiashara pia -- hali ni tofauti sana kwani wafanyabiashara wakubwa wenyewe wanaiendea CCM ili kuchangia kwa matarajio ya kupata upendeleo fulani wa kibiashara kutoka serikalini ili waweze kupiku wafanyabiashara wenzao.

Serikali, ikitafuta kuiwezesha CCM kupiku vyama vingine katika kuwania uongozi wa dola, hutunishia misuli wafanyabiashara wakubwa ili kuwashinikiza wachangie na kukidumisha madarakani kwa manufaa ya pande zote mbili.

Wakati wa mfumo songombingo, ulazima wa kuwa mwanachama ulikuwapo hasa kwa baadhi ya watu wa kawaida tu ? hasa wanafunzi wanaofukuzia masomo Ughaibuni, na pengine kwa wafanyakazi wa serikali na mashirika yake waliotumaini vyeo.

Isisahaulike kuwa baadhi ya watu, mbali na wafanyabiashara, wanaoikumbatia CCM hufanya hivyo kwa lengo maalum ikiwemo kusaka manufaa au ahueni fulani inayotokana na matatizo yao.

Tuchukue mfano wa matukio ya kweli: Miaka kadhaa nyuma, kuna kiongozi wa kimoja ya vyama maarufu vya michezo nchini alifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutafuna fedha za chama hicho.

Baada ya kesi kukamilika kusikilizwa, siku ya hukumu, mshitakiwa alifika mahakamani akiwa amevalia fulana yenye maandishi; 'CCM No 1'. Alihukumiwa kifungo cha jela miaka mitatu.

Wasomaji wanaweza kuhisi ujumbe wa katuni ulivyokuwa katika baadhi ya magazeti ya siku iliyofuata. Bila ya shaka alikuwa na sababu maalum ya kuvaa fulana hiyo na moja kubwa ni kumyumbisha hakimu.

Mfano mwingine: katika mpango unaoandaliwa wa usafiri wa mabasi yaendayo kwa kasi Dar es Salaam, iliamuliwa baadhi ya nyumba zilizokuwa za Shirika la Reli (TRC) ambazo baadhi ya wafanyakazi wake waliuziwa maeneo ya Kamata, zibomolewe ili kupisha ujenzi wa kituo cha mabasi ya mpango huo.

Baadhi ya wamiliki wa nyumba hizo walipinga ubomoaji huo ingawa mamlaka husika ilitangaza kulipa fidia. Waliunda umoja na kuandaa mkutano na viongozi wa Halmashauri ya Jiji.

Ulipofanyika, baadhi yao wamiliki wa nyumba waliosimama kuzungumza, walivaa fulana na kofia za kapelo zilizoandikwa 'Chagua CCM.' Lengo ilikuwa ni kujaribu kuyumbisha uamuzi wa serikali wa kuvunja nyumba zao.

Mifano hiyo miwili inaonyesha dhahiri kwamba hakuna garantii katika ule ujumbe wa 'Ukitaka mambo yako yaende vyema kumbatia CCM.'

Na tukizungumzia sare katika vyama vya siasa, hakika chama tawala kinaongoza kuzihamasisha. Kwa mfano, hata katika shughuli ambazo moja kwa moja ni za kiserikali, utaona watu na makada wa CCM wakizivaa. Rais anaporejea nchini kutoka safari za nje ya nchi baadhi ya wanaompokea huzivaa sare hizi.

Wanakumbuka vizuri historia, katika miaka ya 1930 baada ya chama cha Nazi cha Adolf Hitler nchini Ujerumani, kutwaa madaraka kidemokrasia, wafuasi wake walikuwa wanavalia sare za chama hicho. Siyo tu kwa shughuli za kisiasa, bali hata walipokuwa katika shughuli zao.

Wakati huo, sare hizo ndizo zilikuja kuwa kinga kubwa ya kutobughudhiwa na vyombo vya usalama na vya kijasusi vya Hitler hasa katika kubaini wapinzani wake.

Siamini kama hali imefikia hivyo Tanzania. Inawezekana hata inaanza kuwa hasi kwa chama hicho, hasa kipindi hiki cha tuhuma mbalimbali za ufisadi zinazoelekezwa kwa baadhi ya viongozi wakuu wa serikali na CCM.

Hivi karibuni baadhi ya magazeti yaliripoti kutoka mkoani Mbeya, kuwepo makada wa CCM waliovalia sare za chama chao ambao walizomewa na wananchi kwa kuwaita mafisadi.

Swali la kujiuliza ni je, inawezekana sasa wananchi wanaanza kujiweka mbali na chama hiki ambacho kinanuka tuhuma za ufisadi miongoni mwa viongozi wake wakuu?

Inaonyesha wenye chama hawana la kufanya kubadilisha hali. Viongozi wake kama vile wameshaamini haiwezekani tena kusafisha chama. Kwamba ni vigumu kushawishi Watanzania waamini tuhuma hizo ni majungu tu yanayolenga kuchafuana.

Wananchi wanaona CCM wanapiga porojo tu kama kawaida yao kila kunapokuja tuhuma kusema 'vuteni subira' au 'serikali inafanyia kazi tuhuma.'

Hivi kweli blahblah zao hazionyeshi kuwa baadhi yo ni wahusika wakuu ndio maana wananchi wanaanza kukitenga chama? Na hii kuwa kichochoeo kikubwa cha CCM, kupitia Katibu Mkuu wake, Yusuf Makamba, anayetangaza wanachama wapya wanaovikimbia vyama vya upinzani na kurudi CCM.

Mbinu hizi hazitasaidia na hazitaficha ukweli wa uozo unaokabili utawala wa CCM ? ni mbinu za kitoto na zilizopitwa wakati ? kwani siku hizi vyama vina wafuasi si wanachama. Tofauti ni kubwa mno Makamba.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: