CCM kinamfuata Mugabe?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 08 April 2008

Printer-friendly version
Rais Robert Mugabe

KATIKA uhai wake, akiwa kiongozi wa TANU, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere hakuwahi kupeleka vikao vya chama chake nyumbani kwake, kijijini.

Mwalimu Nyerere alijua kutofautisha kazi za serikali, chama na familia. Aliweka mipaka ambayo ilimsaidia katika kujidhibiti na kuwadhibiti wengine.

Mipaka hii ni sehemu ya nguzo zilizosimamia maadili yake binafsi kama kiongozi wa serikali; na zilimpatia mamlaka makubwa na heshima kutoka kwa umma.

Viongozi wa sasa wanalilia sifa za Nyerere, lakini hawana hata chembe ya maadili aliyokuwa nayo. Hawana hata upeo na muono mbali katika mambo ya jamii. Na sasa wamegundua kwamba jamii imewachoka; na kila mambo yakiharibika jamii inamtaja Mwalimu kama mfano.

Kwa busara ndogo waliyo nayo viongozi wa serikali na CCM, wakadhani njia ya kuwahadaa wananchi kwa kujifananisha na Mwalimu Nyerere ni kufanyia vikao nyumbani kwake.

Wamekwenda, wamerudi; na wametusaidia kuona tofauti kubwa zaidi kati yao na yeye. Mtego waliouweka umewanasa wenyewe. Wananchi tumepona!

Ni katika unyenyekevu huo wa Nyerere, hakupenda kuifanya Butiama kuwa mji. Alijua adha na shida za maisha ya mjini zinapoingizwa kijijini. Alijua kuwa kama ni mahitaji ya mjini, yangepatikana katika vituo vilivyopo tayari, kama Musoma, Bunda na Kiabakari.

Na alijua kuwa kama Butiama ingefanywa mji, kwa kuzingatia historia yake binafsi, ingekuwa kivutio kwa watu kutoka sehemu nyingi, ambao wangepavamia na hatimaye 'kufuta' historia asilia ya Butiama.

Mwalimu Nyerere alikuwa msomi wa historia, hivyo alipenda kutunza historia ya kijiji chake. Kwa muda wote aliokuwa rais, kama angependa kuigeuza Butiama kuwa jiji asingeshindwa. Hakutaka kufanya hivyo kwa sababu aliona mbali.

Tazama hawa wasioona mbali, lakini wanaotaka kuvaa sifa zake. Eti wanataka kuifanya Butiama kuwa mji, makao makuu ya wilaya mpya, kinyume cha matarajio ya Nyerere. Kweli, Butiama ya Nyerere si ile ya Kikwete!

Onyo! Viongozi wa CCM achaneni na Butiama. Msitake kutumia kijiji cha Nyerere kisiasa,, maana imeshadhihirika mnakwenda kinyume cha maono yake.

Na yeyote aliyetoa pendekezo la kufanyia vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) Butiama ndiye amekuwa mwasisi wa aibu mpya ya CCM.

Ni bahati mbaya kwamba hata viongozi na wajumbe wa vikao hivyo hawakupata busara ya kutosha kukataa pendekezo hilo. Hata lilipopitishwa, hawakuwa na busara ya ziada ya kulitumia vema.

Butiama alikozaliwa na kuzikwa Nyerere hapakupaswa kuwa mahali pa CCM kubomoa misingi ya amani iliyasisiwa na Mwalimu.

Na ukweli kwamba wananchi wamekuwa wakiwaonya viongozi kuhusu azima ya kupeleka vikao hivi Butiama. Bahati mbaya waliamua kuziba masikio.

Wamepoteza sifa ya kiuongozi kama ilivyotajwa na Mwalimu mwenyewe. Alisema, "kuongoza ni kuonyesha njia." Wenzetu hawaoni njia, lakini wanataka kuendelea kuwa viongozi. Waliamua kwenda Butiama kumthibitishia Nyerere jambo hilo.

Wamekwenda na kurejea mikono mitupu. Jambo lile lile walilotaka kutumia kughilibu akili zetu ndilo sasa linageuka kuwa mgogoro mpya wa kisiasa unaokaribia kulipuka upya Zanzibar na nchi nzima.

Kwa kuwa viongozi wameshindwa kutumia busara, sasa wananchi wanajiandaa kutumia misuli. Hatuoni dalili kwamba watawala wanafanya lolote kuzuia hali hii kutokea. Hawana uwezo tena!

Lakini yote hayo ni kutokana na ukubwa wa jina Butiama linapohusishwa na siasa za nchi. Wananchi tunajiuliza, kama CCM walitaka kwenda mkoani Mara kufanya vikao, si wangefanyia kwenye ofisi za mkoa? Walifuata nini Butiama huku wakijua wana nia mbaya na taifa?

Hivi baada ya kutoka Butiama, CCM wanaweza kusimama leo na kuwaambia Watanzania kuhusu jambo hata moja la maslahi ya kitaifa walilojadili?

Maana kama ni ufisadi, hawakuugusa kabisa. Kama ni mwafaka wa kisiasa Zanzibar, hali imebaki kama ilivyokuwa kabla hawajaenda huko; na kimsingi imekuwa mbaya zaidi.

Hakika, kushindwa kwao kukubaliana na matokeo ya kazi ya Kamati ya Rais ya muwafaka kunaweza kutaleta ghasia kubwa ambazo wangeweza kuziahirisha. Na kama wameshindwa hili, tuwape lipi?

Inakuwaje chama tawala kinashindwa kugundua kwamba wananchi wamepoteza imani na serikali? Inakuwaje kinafanya uzembe mkubwa wa viwango hivi katika mazingira ambamo kilipaswa kuteka hisia za wananchi?

Tunajua fika kuwa walipokuwa wanakwenda Butiama, mojawapo ya nia zao ilikuwa kujaribu kufunika mjadala juu ya ufisadi. Walidhani wangeibua mjadala mpya kuhusu Zanzibar ili kuondoa mawazo ya wananchi katika ufisadi.

Hakika, hii ilikuwa nia mbaya kwa taifa, nan Mungu amesaidia; wamekwama zaidi. Tumerejea pale pale tulipokuwa.

Walikwenda vifua mbele, sasa wamerejea mikono nyuma; wameinama kwa aibu. Kazi iliyobaki sasa ni moja – kuwazomea.

Na sasa tutakuwa na hasira mchanganyiko – za Watanzania na 'mzimu wa Nyerere.' Huyo shetani aliyewaita na kuwapeleka Butiama ndiye aliyewavuruga akili ndani ya vikao, hata wakashindwa kukubaliana katika masuala nyeti, na walipokubaliana, mambo yakawa yameshaharibika!

Jeuri ya CCM inawapeleka viongozi wetu kule kule ambako viongozi wa vyama vyote vilivyopigania uhuru katika Afrika wamevipeleka vyama vyao baada ya kukaa madarakani kwa muda mrefu na kuishiwa hoja mpya na mikakati mipya.

CCM inaelekea kule kule vilikoelekea UNIP ya Zambia na KANU ya Kenya. Achana na hivyo, vimeshakuwa vyama vya upinzani, CCM sasa inaning'inia kama ZANU-PF ya Robert Mugabe wa Zimbabwe.

Wasioona mbali wanadanganyika kwa mbwembwe na propaganda za kisiasa wanazofanya kina Yusuph Makamba na Jakaya Kikwete. Wenye kuona mbali wameshaanza kutabiri anguko la CCM katika siku chache zijazo.

Katika mwenendo wa mambo, CCM inaweza kuanguka na Kikwete, kiongozi ambaye alitarajiwa kuinyanyua kutoka shimoni alikoikuta wakati anaingia madarakani mwaka 2005.

Lile tumaini lililorejea tuliloambiwa, limerudi kwao; na sasa umma ule ule uliomuunga mkono Kikwete yule yule umembatiza jina la 'msanii.' Sawa! CCM wamekuwa wakitawala kwa sanaa; na sasa ni zamu ya wananchi kuwafanyia usanii watawala wale wale.

Yaweza kuwa katika sanduku la kura au kwa mbinu nyingine zisizotarajiwa. CCM lazima iondoke, hasa baada ya kwenda Butiama kumuaga mzee. Wakubali wakatae, fursa ya Butiama ilikuwa murua kwa kuifufua CCM.

Sasa wametupa pa kuanzia upya. Tuanzie Butiama.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: