CCM kinaweweseka?


Zaynab Turuku's picture

Na Zaynab Turuku - Imechapwa 09 September 2008

Printer-friendly version

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea kuweweseka. Kinahubiri isichokiamini na kinanena isichokitenda.

Alhamisi iliyopita, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, George Mkuchika, alisema chama chake hakitavumilia wanachama wake wanaoendesha vitendo vya rushwa katika chaguzi zinazoendelea katika jumuiya za chama hicho.

Mkuchika alisema chama chake kimepokea taarifa kutoka sehemu mbalimbali kwamba kuna baadhi ya wagombea wameanza kishiriki katika utoaji rushwa.

Alisema, “Kuna wagombea wanaozunguka mikoani wakati hata majina yao hayajapitishwa na vikao husika. Huko wanakutana na wajumbe na kutoa takrima kwa lengo la kushawishi kupigiwa kura.”

Anasema baadhi ya viongozi wanawatuma wapambe na kuwagharimia kwa kila kitu, ambao huzunguka nchini kote kwa niaba yao kwa ajili ya kwenda kuwanadi, kugawa bahasha au takrima kwa wajumbe.
 
Hapa najiuliza: CCM kimezaliwa upya, au kuna mtu kinamsaka? Hakuna asiyefahamu kuwa chaguzi yingi za chama hiki hutawaliwa na rushwa tena za wazi kabisa.

Hata uchaguzi uchaguzi mkuu uliopita madai haya yalikuwapo, Lakini CCM hakikuchukua hatua.

Kwa mfano, Andrew Chenge alitajwa hadharani na baadhi ya wanachama wenzake na ushahidi wa mazingira ukapatika kupitia moja ya akaunti yake ya benki ambayo katika kipindi cha uchaguzi huo, ilitawanya mamilioni ya shilingi kwa baadhi ya viongozi wa chama chake.

Mpaka hivi sasa si Chenge wala wale waliopewa fedha waliojitokeza na kusema “mgawano huo” ulikuwa kwa ajili ya nini?

Chenge huyohuyo ndie aliyerudi jimboni kwake baada ya kujiuzulu uwaziri kutokana na tuhuma za rushwa katika rada, akachinja ng’ombe kwa ajili ya kujisafisha. CCM haijamkemea, wala kumuuliza.

Wananchi walijipanga mabarabarani kumpokea. Hawakumpokea kwa sababu wanajua ni mtu msafi, hapana ni kutokana na umasikini walionao.

Mkuchuka anasema, “Baadhi ya wagombea wanapakana matope, mambo ambayo ni kinyume kabisa na maadili ya chama cha mapinduzi.”

Mkuchika ni mtu wa pili kukemea viongozi ndani ya CCM anaodai wanapakana matope. Kauli hii inalenga nani? Mbona hata Katibu mkuu wa chama hicho, Yusuph Mamba juzi amepaka matope Nape Nnauye katika kikao cha Baraza Kuu la Vijana.

Ili kupambana na rushwa Mkuchika anasema serikali ya awamu ya nne imeongeza vitendea kazi, watumishi, imetunga sheria mpya ambayo imeongeza makosa ya rushwa kutoka manne ya awali hadi kufikia ishirini na moja.

Anasema serikali imeajiri maofisa zaidi wa kupambana na rushwa. Je, ongezeko hilo lina faida gani kwa wananchi kama wala rushwa wanaendelea kutanua?

Hatua hizi zilizochukuliwa dhidi ya rushwa zina faida gani kama chombo chenye jukumu la kupambana na rushwa (TAKUKURU) bado kinaongozwa na Edward Hoseah.

Mkuchika hafahamu kwamba Hosea alitetea ufisadi na udanganyifu wa Richmond? Au hajui kwamba tuhuma zinazomwandama Hosea zinazidi kuiondolea hadhi na heshima TAKUKURU mbele ya wananchi?

Rushwa ndani ya CCM haiwezi kwisha kama serikali inayoisimamia itaendelea kukumbatia wala rushwa.

Rushwa ndani ya chama hicho, haiwezi kukatika kama viongozi wake wa juu wakituhumiwa waziwazi kufadhiliwa na wafanyabiashara.

Aidha, rushwa katika CCM haiwezi kukatika kama CCM kitaendelea kupata viongozi wake kwa njia ya ununuzi wa kura.

Njia pekee ya kumaliza rushwa katika CCM ni kutumia kwa vitendo ahadi ya mwanachama inayosema, “Rushwa ni adui wa haki.”

Kwamba wanachama na viongozi wao wanakuwa mstari wa mbele kupiga vita rushwa na si kupiga vita viongozi wanaokemea rushwa na ufisadi kwa manufaa ya taifa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: