CCM na kisa cha King Oedipus


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 09 March 2011

Printer-friendly version
Mtazamo

BAADHI wanaweza kuwa wamesoma kitabu cha King Oedipus (The Sophocles) katika saikolojia na wengine katika fasihi. Kisa hicho, ni mfano mzuri kwa watu wanaohaha kukwepa janga, lakini wakashindwa kuzuia janga hilo kutokea.

KING Oedipus, mchezo wa kuigiza uliotungwa Ugiriki na kuigizwa mwaka 429 kabla ya kuzaliwa Yesu, unafanana na kitendo cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutaka kukwepa vurugu kwa kuanzisha vurugu.

Oedipus alikuwa mtoto wakiume wa Mfalme Laius na Malkia Jocasta wa kabila la Thebes. Mfalme Laius aliambiwa na watabiri kuwa utawala wake utakabiliwa na matatizo makubwa na kisha utang’olewa madarakani na mtoto wake yaani Oedipus.

Alichofikiria haraka Mfalme Laius, ni kumuua Oedipus akiwa bado kichanga. Akamfunga kwenye ‘rambo’ kisha akamwamuru mkewe Jocasta afanye kazi hiyo. Lakini alipata hofu akamwambia ‘hausigeli’ akafanye kazi hiyo porini.

Hausigeli naye alisita, badala yake akamchukua Oedipus hadi mlimani ambako alimwacha ili afie huko. Mungu mkubwa, akapita mchungaji mifugo akamwokota akampa jina la Oedipus yaani aliyevimba miguu.

Oedipus alipelekwa kwa Mfalme Polybus wa kabila la Corinth ambako alilelewa.

Baada ya kukua na kuwa mkubwa, alisikia fununu kwamba yeye si mtoto wa kuzaliwa na Mfalem Polybus na mkewe Merope. Lakini kila alipowahoji walezi wake hao, walikataa. Hata alipouliza watabiri, hawakumueleza ukweli.

Kwa kuwa utabiri ulionyesha atamuua baba yake na kumuoa mama yake, Oedipus aliondoka nchi ya Corinth kukwepa mkasa wa kumuua ‘baba’ yake Polybus na kumuoa ‘mama’ yake Merope. Hao ndio aliamini kuwa ni wazazi wake halisi.

Akaenda Thebes. Njiani akakutana na Laius (ambaye ni baba yake), wakakorofishana. Mfalme Laius akapigwa akauawa.

Akiwa Thebes alifanikiwa kutegua kitendawili cha “kiumbe gani hutembea kwa miguu minne asubuhi na miwili mchana na mitatu jioni.” Utenguzi huo ukampa tuzo ya kuwa mtawala wa Thebes na kumuoa mjane wa Mfalme Laius.

Ni hadithi ndefu. Hivyo ndivyo viongozi wa CCM walivyokaa, wakafikiria wakaona kuwa inafaa kutumia njia ya kukwepa kuua kwa kutuma polisi waanzishe vurugu za kuzuia maandamano ya wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) huku wakijua watu watauawa.

Viongozi wa chama hiki wameiagiza serikali ya Rais Jakaya Kikwete iachane na uvumilivu, njia ya kuepusha wananchi wasimwagiwe elimu ya uraia juu ya hatima ya nchi yao ni kumwaga polisi mitaani wazuie maandamano na mikutano ya CHADEMA kwa risasi za moto.

CCM wanadhani kwamba huko si kuua ila ni kuzuia tu sumu inayowaingia taratibu wananchi kuhusu udhaifu wa serikali yao.

CCM hawajafurahishwa na amani na utulivu ulioonyeshwa na maelfu ya wananchi wanaofurika kusikiliza “mitume wapya” walioshushwa kuikomboa nchi kutoka serikali inayolea mafisadi.

Kisingizio chao eti CHADEMA wanamwaga sumu mbaya dhidi ya serikali. Wanadai kama ni masuala ya ufisadi, CHADEMA walinadi sera hiyo, lakini wakashindwa katika uchaguzi.

Kwa hiyo, wakasingizia kuwa CHADEMA wana mkakati wa kuiangusha serikali ya rais Kikwete. Kwa bahati mbaya, na hasa kwa vile umaarufu wake umeshuka kwa kasi tangu umalizike uchaguzi, Kikwete naye amelaani maandamano ya CHADEMA akidai wanataka kumwondoa nje ya sanduku la kura.

Steven Wasira, John Chiligati, msajili wa vyama vya siasa, John Tendwa na mwanasiasa mchovu Augustine Mrema nao wakaibuka kukadandia mikutano ya CHADEMA.

Kinachoonekana hapa, CCM wanataka kukwepa maandamano na mikutano wanayodai inatishia amani kwa kuanzisha vurugu. Wamechoka kuona mshikamano mkubwa wa wananchi wa Mwanza, Musoma, Kahama, Bukoba na maeneo mengine.

Wanashauku ya kushuhudia yale yaliyotokea 5 Januari 2011, jijini Arusha, ambapo polisi waliua watu watatu na kujeruhi makumi wengine.

Wanachosahau CCM ni kwamba hawana ubavu wa kumiliki siasa; au kupangia vyama vingine ajenda; wala kukilazimisha CHADEMA kuwa chama cha msimu kinachosubiri uchaguzi ndipo wafikie wanachama wao.

Kama wanataka vyama visubiri muhula wa uchaguzi, kwanza sharti wafanye hivyo wao kwanza? Lakini kwa kuwa wao wanapita kuhamasisha wanachama wao na kupanga mikakati ya mwaka 2015, kwa nini wanataka upinzani ulale kusubiri uchaguzi?

Inaonekana CCM imeamua kuchuma janga la vurugu. Je, wamewaalika nani wa kula nao? 

0789 383 979
0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: