CCM: Kutema tamu, kumeza chungu


mashinda's picture

Na mashinda - Imechapwa 12 September 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi

KAMPENI za uchaguzi mdogo katika jimbo la Igunga, mkoani Tabora zinatarajiwa kuanza mjini humo Alhamisi wiki hii. Tayari viroja vya wanasiasa vimeanza na anayetegemea kuona au kusikia matumizi ya akili huko Igunga anajisumbua. Huu utakuwa mwezi wa kupumzisha akili na ukweli, kisha kutumia unafiki na uwongo ili kunogesha siasa za nchi yetu.

Kwa hali ilivyo ni mchuano kati ya CHADEMA na vyama vingine. Nasema hivi kwa sababu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), pamoja na kwamba kila chama kimesimamisha mgombea wake, lakini kimsingi ni rahisi vyama hivyo kuachiana kuliko CUF kukiachia CHADEMA.

Kimantiki CCM imesimamisha wagombea wawili – Leopold Mahona na Dk. Peter Kafumu. Baada ya raundi mbili za kampeini, vyama hivyo vitaundwa mkakati mpya wa kuunganisha nguvu ili kuhakikisha CHADEMA hakishindi katika uchaguzi huo. Haiwezekani vyama vilivyoweza kuunda muafaka serikali, vikashindwa kusaidiana kwenye ulingo wa kisiasa.

Uchaguzi mdogo wa Igunga unafanyika kufuatia kujiuzuru kwa Rostam Aziz kwa madai ya CCM kujivua gamba, lakini kwa Rostam mwenyewe kudai amechoshwa na siasa za uchwara na kuchafuana zilizojiri ndani ya chama chake.

Hii haina maana kuwa kujiuzuru kwake kunaondoa uchwara wa CCM au kupunguza kuchafuana. Bali, kwa mtizamo wa ndani zaidi, kujiuzuru kwa Rostam kunaifanya CCM iwe dhaifu zaidi kuliko awali.

Hoja hii inadhihirishwa na ukweli kuwa CCM kupitia mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete, kimesikika kikimuomba Rostam akisaidie katika uchaguzi huu ili kiweze kushinda. Taarifa hizi zinathibitisha madai ya muda mrefu ya waziri mkuu mstaafu, Joseph Sinde Warioba kuwa CCM kimegeuka chama cha viongozi na siyo tena chama cha wanachama.

Haiwezekani katika hali ya kawaida, chama kianzishe mpango wa kujisafisha kwa kauli-mbiu ya kujivua gamba, kisha kifanikiwe kumfanya mtuhumiwa mmoja ajivue gamba, na muda mfupi baadaye mtuhumiwa huyo huyo atumike kukinadi chama hicho kwa ombi maalum la mwenyekiti wa chama!

Kuna kila dalili kuwa habari hizi ni za kweli kwa sababu hata Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa amedai yuko tayari kwenda Igunga ikiwa tu Rostam atakubali kuambatana naye. Na ikiwa huu ndiyo ukweli wenyewe, basi CCM haimtaki Rostam, lakini matunda yake inayataka kwa udi na uvumba.

Hii inaonyesha CCM haiwataki mafisadi, lakini inautaka ufisadi. Kwa maana nyingine hii ni vita ya watu iliyojaa chuki binafsi zinazotokana na kupunjana maslahi, na kamwe si vita ya ufisadi ikiwa mafisadi wanaweza kuondolewa kwenye uongozi, lakini wakatumika kukitafutia chama ushindi.

Katika mgongano huu wa kimantiki na kimtizamo, CCM inajikuta iko njiapanda ya hatari. Kwa upande mmoja, ushindi wa Igunga inautaka sana, lakini haina uwezo wa kubeba gharama za ushindi huo zinazotokana na kuwatumia mafisadi.

Na mafisadi nao wanajikuta katika kona ya uamuzi mzito wa ama kukataa wito wa kuisaidia CCM katika kampeni hizo na kuchukuliwa hatua zaidi za kidola, au kukubali shingo upande kuisadia CCM ili mbele ya safari utengenezwe muafaka wa kutoshughulikiana. Kwa hili la pili, CCM imeshika mpini na mafisadi wameshika makali.

Matokeo ya uchaguzi mdogo wa Igunga yatakuwa ya kihistoria ndani ya chama hiki. Ikiwa CCM kitashinda, ushindi huu utakuwa na maana tatu kubwa.

Kwanza, kuwa ilitegemewa kwa sababu jimbo hili lilikuwa mikononi mwake kwa muda mrefu. Pili, jimbo halikuwa mali ya Rostam bali mali ya CCM na kwa hiyo Rostam ni mtu tu wala hana dalili za kuwa taasisi kama ambavyo imekuwa inadaiwa na baadhi ya vyombo vya habari na baadhi ya marafiki zake.

Tatu, pamoja na udhaifu na migawanyiko iliyomo ndani ya CCM, bado ni chama dola, komavu na chenye uwezo wa kuwaaadhibu wanachama wake bila kujali matokeo ya hatua hiyo. Hili la tatu likifuatiliwa linaweza kukisaidia chama kurejesha nidhamu.

Lakini CCM ikishindwa Igunga, anguko hilo litakuwa pia na maana tatu kuu. Kwanza, madai ya ufisadi yana ukweli na yanakiathiri sana chama kuliko inavyoweza kufahamika.

Pili, vyama vya upinzani pamoja na uchanga na udhaifu wake, vimeimarika na vinaweza kutumia fursa za migawanyiko ya CCM kunyakua majimbo yaliyo mikononi mwa chama hicho. Hili ni kubwa kwa sababu, baada ya kunyakua jimbo lililo, kitakachofuata ni upinzani kunyakua dola iliyo mikononi mwa CCM.

Tatu, kwamba si ufisadi tu unaokidhoofisha CCM, bali ni kukosekana kwa uongozi thabiti. Hii ina maana kuwa ufisadi ni mbaya, lakini udhaifu wa uongozi ni mbaya zaidi na wa hatari katika chama kinachoshika dola.

Kushinda au kushindwa kwa CCM huko Igunga kunaweza kusilete unafuu wowote kwa chama hicho kutokana na udhaifu wa uongozi uliomo kwa sasa. Hoja yangu ya msingi hapa ni kuwa, ikiwa CCM itashinda inaweza kwa ujinga uliozagaa ndani ya chama kwa sasa, kupelekea hatua za kuwaadhibu wanaodaiwa kuwa ni mafisadi.

Hatu hii inaweza kuchukuliwa ili kuwakomoa hao mafisadi kwa kuwa sasa ushindi umepatikana hata baada yao kujiuzulu ubunge. Wapo wanaosema, adhabu kwa mafisadi haitibu kansa ya uongozi na ulegelege.

CCM ikishindwa Igunga, wanaoitwa mafisadi na wafuasi wao wanaweza kuwabeza wana wenzao kuwa kushindwa huko kumetokana na hatua yao ya kuendekeza majungu na fitina. Hili linaweza kuwa tishio kwa chama na itawaogopa mafisadi ili wasipoteze majimbo zaidi.

Hofu hii imeishawakumba vigogo wengi wa chama hiki akiwamo Kikwete mwenyewe. Mantiki ya hofu hii inaashiria kuwa chama kinathamini sana majimbo yaliyo mkononi mwake kuliko ubora wa viongozi wanaoyashikilia.

Kwa maneno mengine, CCM kiko tayari kuabudu ufisadi ili kuendelea kushikilia majimbo na dola. Fikra za kwamba CCM ikubali kupoteza majimbo hayo kwa gharama za kujisafisha na kuwa chama kinachotetea maslahi ya wananchi maskini, zinabezwa na kupuuzwa sana.

Ushindi wa CCM utakaopatikana Igunga kwa gharama ya CCM kukumbatia na kuunyamazia ufisadi, utakuwa ni ushindi bandia usiokisaidia chama wala kuongeza thamani yake mbele ya wananchi. Ni ushindi wa kushinda vita bila kushinda mapambano. Ni ushindi wa kuruka mkojo na kukanyaga kinyesi.

Kimya cha CCM kuhusu ufisadi katika kampeni za Igunga utakigawa zaidi chama hicho na kukifanya kisiwe na uwezekano wa kuungana. Ombwe la kiitikadi linalokitesa chama hicho, likiungana na ombwe la uongozi linalolalamikiwa na wengi, vitakimaliza chama badala ya kukiimarisha.

Je, nini kifanyike? Kwa kuwa ni wazi Rostam haiwezi kusimama katika jukwaa na kuulaani ufisadi; na kwa kuwa pia Rostam hawezi kusimama jukwaa moja na wale wanaoulaani ufisadi katika kampeni hizo, ni bora CCM ifanye uamuzi wa busara mapema kabla ya kampeni kuanza. Uamuzi huo unahitaji ujasiri wa kiuongozi aliokuwa anaufundisha sana Benjamin Mkapa. CCM iamue kuachana na Rostam na wenzake kule Igunga na iwe tayari kubeba gharama za kutokuwa nao – chungu au tamu.

Kwa upande wake Rostam na wenzake, kama kweli wanakipenda CCM, basi wanalo jukumu moja kwa sasa – kukiacha kijijenge, badala ya kuking’ang’ania huku wanakidhoofisha.

Pamoja na kwamba baadhi yetu tulio wanachama wa CCM, watazamaji na wachambuzi, tunajua kuwa tatizo la CCM ni zaidi ya ufisadi, ni zaidi ya Rostam Aziz na wenzake, lakini hatua yao ya kukaa pembeni inaweza kukijenga japo kwa muda.

Vinginevyo, CCM kitaendelea kuumwa na hatimaye kitakufa. Je, nani yuko tayari kufufua chama mfufu?

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: