CCM kweli wanachonga vinyago


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 13 June 2012

Printer-friendly version

AKIHUTUBIA mkutano wa hadhara, alipokuwa katika mji mdogo wa Makambako mkoani Njombe, Katibu wa Uenezi na Itikadi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye aliuliza wananchi, “Nani yuko upinzani ambaye hakutoka CCM?”

Swali hilo lilionekana kiwasisimua wafuasi wa chama hicho, nao wakamjibu kwa mbwembwe, “Hakunaaaaa.”

Akaona amepatia. Akawauliza tena, “Sasa itakuwaje kinyago nichonge mwenyewe halafu kinitishe?” Hapo kikasikika kicheko.

Tunawajua wachonga vinyago. Mchongaji kabla ya kuchonga kinyago chake, hujenga dhana akilini mwake ama ya kutisha, kuchekesha au kushirikiana.

Baada ya hapo atayafunua mawazo yake kupitia vinyago kwamba sasa atachonga kinyago cha kuchekesha watu pamoja na yeye au kinyago cha kutisha kila mtu pamoja na yeye mwenyewe.

Kama CCM ilikuwa inajua kuwa inachonga vinyago vya kutisha halafu kwa mshangao wake, vinyago vyake havimtishi mtu, pamoja na yeye mwenyewe, basi ni ushahidi usio acha shaka kuwa, hata kazi ya kuchonga vinyago CCM imeshindwa pia!

Katika mkutano wake wa Jangwani Jumamosi iliyopita kulikuwa na burudani nyingi, lakini hakukuwa na chochote kilichoonyesha madhumuni hasa ya mkutano ule yalikuwa ni yapi kama si kuonyesha “hofu ya vinyago”.

Uwepo wa mawaziri katika mkutano ule ulileta hisia za udhaifu wa viongozi wa CCM kushindwa kuukabili ushindani bila msaada wa serikali. Kama CCM ingetaka isionekane kinyago pale Jangwani ingekuwa yenyewe kwa maana ya viongozi wake bila kuomba msaada wa mawaziri wanaolipwa mishahara kutokana na kodi ya Watanzania wote.

Hakuna waziri ambaye hakutoa ahadi, tena kwa namna ileile wanavyofanya wakati wa kampeni. Kwa nini, hawa watu wa CCM hawataki kuamini mabwege waliobaki kuamini ahadi za wanasiasa kuwa ni wachache sana?

Mkutano ulifanana kwa kila hali na mikutano mingine yote inayofanyika wakati wa kampeni za uchaguzi. Nape anamwambia John Komba weka wimbo huu, Komba anaweka wimbo ule! Anaimba kuwa mchagueni kada yule pale mnamwona, Jakaya Kikwete! Je, CCM walikwenda Jangwani kufanya kampeni za uchaguzi wa mwenyekiti wao au kuchonga vinyago?

Uhodari wa baadhi ya mawaziri wetu katika kujieleza unajulikana. Nani hajui kuwa Waziri wetu wa Ujenzi John Pombe Magufuli kuwa ni mzungumzaji mzuri? Sina kinyongo na mtu huyu, lakini ukweli lazima usemwe kuwa Jumamosi pale Jangwani alifanana na kinyago anachochonga Nape!

Magufuli bado ana fikra mgando kuwa kuna Mtanzania wa leo ambaye ana shida na uwingi wa kilomita za barabara za lami! Wakati wa uhuru kulikuwa na kilomita chache za barabara zenye lami ni kweli lakini je, ni barabara ipi ilikuwa na msongamano wa magari?

Leo kuna kilomita nyingi za barabara zenye lami, ni kweli lakini je, ni barabara ipi isiyo na msongamano wa magari? Benjamin William Mkapa amemaliza miaka kumi ya urais Magufuli akiwa waziri wa barabara, Kikwete naye anamaliza miaka kumi yake, bado barabara ya kusini imeshindikana! Hiki siyo kinyago?

Tumshukuru Mwenyezi Mungu ndugu yetu Harrison Mwakyembe amepona. Lakini hatasahauliwa namna alivyowaundia “ugonjwa” maskini wa nchi hii alipoficha ukweli katika ripoti yake kuhusu Richmond, unaozidi kuwatesa watu wa Mungu!

Sasa wanavuja damu kama jasho! Mwenzetu anaufaidi uwaziri kwa kazi aliyoifanya! Mungu ndiye mwenye kuhukumu!

Kama ukweli waliouficha hautawadhirika  hapa duniani, mbele ya Muumba kitakwenda kueleweka! Tesekeni watu wa Mungu, siku hazigandi. Hapa duniani wote tunapita tu.

Woga walionao baadhi ya wananchi wetu siyo kilema kusema watakufa nacho. Ole wao utakapowatoka! Nawaambieni siku hiyo wanafiki hawa watatamani ardhi ipasuke, iwameze nayo itakataa!

Wataiomba milima iwafukie, nayo haitakubali! Adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa waliowadhiki watu wake ni kali tena inatisha! Ole wao watu hawa, kwa maana ingelikuwa bora kwao kama wasingezaliwa!

Mara tatu Jangwani, nilimsikia Steven Wasira akitoa ahadi ya kufungua mashamba makubwa Kilombero ya kilimo cha mchele. Wasira anajua kuwa mchele haulimwi bali mpunga, lakini kwakuwa alichokuwa akikisema kilikuwa hakitoki kifuani mwake bali mdomoni tu, akawa anasema chochote tu. Kinyago!

Abdulrahman Kinana, mlezi wa CCM mkoa wa Dar es Salaam aliyekuwa mgeni rasmi alisema, “Msiwasikilize wapinzani. Hawamwamini mtu yeyote. Hawajiamini hata wao wenyewe! Hawa hawafai kuongoza serikali!”

Hizi ni propaganda zinazofanywa na mtu aliyekomaa kisiasa ; kusema na kuchambua udhaifu wa mpinzani wako. Mchambue mpaka mwisho.

Kwa wenzetu waliostaarabika hufikia hata kuwaambia wapiga kura kuwa msimchague mpinzani wangu kwa sababu akili yake ni ndogo hata mbwa wangu anamshinda kufikiri. Propaganda zinazompa msikilizaji nafasi ya kufikiria na kuyachambua yaliyozungumzwa. Siasa siyo ugomvi!

Tuliwasikia CHADEMA wakiwaelekeza Watanzania wote bila kujali vyama vyao jinsi ya kushiriki katika mchakato wa kutoa maoni kwenye tume ya katiba. Wakawafundisha mambo ya kuhoji. Wakawajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu na kwa nia njema kabisa katika kuujadili Muungano.

Ni kipi CCM waliwafundisha wananchi kuhusiana na masuala hayo au hata wanachama wao tu?

Mkutano wa CHADEMA ulikuwa na sura ya kitaifa kichama. Siyo lazima CCM wafanye kama walivyofanya CHADEMA hata kama ilileta maana kubwa, lakini mkutano wao ulitoa sura gani?

Walionekana kama kundi la watu waliolazimika kufanya mkutano ili nao waonekane wamefanya mkutano, basi!  Hivyo ikawalazimu kutumia pesa nyingi. Walisahau ule usemi usemao ‘Ni bora ukae kimya watu wakudhanie kuwa u mjinga, kuliko useme na kuthibitisha ujinga wako!’.

CCM ingetumia vizuri sana mkutano ule kama wangeufanya uwe mahsusi kwa mlezi wao wa mkoa Kinana, kutoa mrejesho kwa wananchi, kwa yale aliyoyakusanya kufuatia ziara yake muhimu aliyoifanya katika mkoa wa Dar es Salaam kuanzia tarehe 26-1-2012 hadi tarehe 4-2-2012.

Ziara ile ilijenga matumaini mapya kwa wananchi,  wanachama wao na hata wa vyama vingine na kwa sisi tusio na vyama!

Bahati mbaya akilini walikuwa na picha na kinyago na wakakichonga Jumamosi, kughilibu akili za wananchi kwa ahadi, kufuta matumaini na kurudia upuuzi uleule!

Kinana ana deni kubwa kwa wananchi wa Dar es Salaam, na kwa Watanzania wote! Warejeshee mrejesho mliowaahidi ili mjitofautishe na watu wakutofautishe na wengine. Maana kilichofanyika na wewe ni kama u mmoja wa  wachonga vinyago.

Wako wapi katibu mkuu mstaafu, Philip Mangula, mzee Job Lusinde, wazee wa CCM, Peter Kisumo, Profesa Sarungi? CCM ya leo inadai ni ya wachonga vinyago!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: